Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Suzana Chogisasi Mgonukulima

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA aliuliza:- Lengo la Serikali ni kuingiza fedha zote za kodi kwenye mfuko mmoja na baadaye asilimia fulani ya fedha hizo zirudishwe kwenye Halmashauri:- Je, kwa nini isitungwe sheria ya kuibana Serikali ikiwa haitarejesha fedha hizo kwenye Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji?

Supplementary Question 1

MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya majibu ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali ya nyongeza mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, makusanyo ya kodi za majengo katika Manispaa ya Iringa katika mwaka wa fedha 2015/2016, TRA iliweza kukusanya shilingi milioni 800. Katika upangaji wa bajeti wa Halmashauri ya Manispaa Iringa fedha za kodi ya majengo zilikuwa zimekadiriwa zisaidie miradi ya Manispaa ya Iringa. Hadi navyozungumza hapa hakuna hata senti tano iliyorudishwa. Je, nia ya Serikali ni kutaka kukwamisha maendeleo ya Manispaa ya Iringa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa vikao vya RCC. Halmashauri saba za Mkoa wa Iringa zilipeleka barua ya maombi maalum kama sheria inavyotaka, kuomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya. Wilaya ya Kilolo imefanikiwa kupewa shilingi bilioni moja na point, Wilaya ya Iringa vijiji imefanikiwa kupewa milioni moja na point, Wilaya ya Mufindi imefakiwa kupewa shilingi bilioni moja na point, Mafinga Mjini imefanikiwa kupewa shilingi milioni 400; Manispaa ya Iringa ilikuwa imeomba kibali maalum cha shilingi milioni 700, haikuweza kupewa fedha hizo. Je, fedha hizi zinalipwa kisiasa hasa ukizingatia Majimbo yaliyopewa fedha ni ya CCM na Jimbo la Manispaa ya Iringa ni la CHADEMA? (Makofi)

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Suzana Chogisasi Mgonukulima, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, napenda kumwambia kwamba siyo nia ya Serikali kukwamisha maendeleo ya Halmashauri yoyote ile na ndiyo maana tarehe 5 Mei, 2018, Serikali imezindua Mpango Mkakati wa Kuziwesha Halmashauri kubuni miradi ya maendeleo itakayo-generate mapato kwa ajili ya Halmashauri husika na hatimaye kuhakikisha shughuli zote za maendeleo zinaendelea kutekelezwa ndani ya kila Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, napenda kwanza kumshukuru kwa kuweza kusema ndani ya Mkoa wa Iringa, Wilaya nne ndani ya miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli zimepewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya. Hilo ni jambo la msingi, naamini angetupongeza kama Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swaIi lake la pili amesema kwamba pesa zinatolewa kisiasa. Napenda kumwambia Mheshimiwa Mgonukulima kwamba Mheshimiwa Msigwa Mbunge wa Iringa Mjini yeye mwenyewe amekiri mbele ya Mheshimiwa Rais kwamba miradi mingi ya maendeleo inapelekwa kwenye Majimbo yote. Kwa hiyo, hakuna siasa kwenye utelekelezaji wa miradi ya maendeleo. (Makofi/Kicheko)

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA aliuliza:- Lengo la Serikali ni kuingiza fedha zote za kodi kwenye mfuko mmoja na baadaye asilimia fulani ya fedha hizo zirudishwe kwenye Halmashauri:- Je, kwa nini isitungwe sheria ya kuibana Serikali ikiwa haitarejesha fedha hizo kwenye Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali imechukua baadhi ya vyanzo vya mapato katika Halmashauri na kurudisha Serikali Kuu na vilevile imechukua baadhi ya watumishi kama watumishi wa Idara ya Ardhi na sasa watumishi wa Idara ya Maji. Je, Serikali haioni kwa kufanya hivyo inakwenda kinyume na sera yake ya D by D na mwisho wake ni kuziua kabisa hizi Halmashauri? (Makofi)

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la Mheshimiwa Selesini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kumwambia kwamba, uchukuaji wa vyanzo vile vya mapato ilikuwa kwa lengo moja na Bunge lako Tukufu liliridhia kwamba vichukuliwe ili ufanisi uonekane kwenye makusanyo na hatimaye fedha hizi ziweze kutekelezwa kulingana na bajeti za kila Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili la kuchukua watumishi, tuitendee haki Serikali yetu ya Awamu ya Tano, hakuna mtumishi aliyehamishwa kutoka Halmashauri moja kupelekwa kwenye Wizara yoyote. Watumishi wamebaki kwenye Halmashauri husika, lakini wanatakiwa kuripoti kwenye Wizara zao za kisekta. Kwa hiyo, hakuna mtumishi yeyote aliyeondolewa ndani ya Halmashauri. Tunachokifanya kama Serikali ni kuboresha tu utendaji kazi wa watumishi hawa kwa manufaa mapana ya Taifa letu wananchi wetu kwa ujumla.

Name

Alex Raphael Gashaza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Primary Question

MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA aliuliza:- Lengo la Serikali ni kuingiza fedha zote za kodi kwenye mfuko mmoja na baadaye asilimia fulani ya fedha hizo zirudishwe kwenye Halmashauri:- Je, kwa nini isitungwe sheria ya kuibana Serikali ikiwa haitarejesha fedha hizo kwenye Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji?

Supplementary Question 3

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ni miongoni mwa Halmashauri ambazo ziliendelea kuruhusiwa kukusanya kodi ya majengo lakini Mkurugenzi wa Halmashauri yangu ya Wilaya ya Ngara amekuwa akienda tofauti na kinyume na kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana ilielekezwa kwamba majengo yote itakuwa ni flat rate Sh.10,000, ghorofa Sh.50,000 kwa floor, lakini katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Rulenge sasa hivi kuna mtafaruku mkubwa, nyumba ambazo hazijakamilika…

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi kuna nyumba za tope zinatozwa kodi, kuna nyumba za wazee wa zaidi ya miaka 70 zinatozwa Sh.200,000 mpaka Sh.300,000. Naomba Serikali itoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngara kwa sababu ni usumbufu na anawatishia kwamba atawapeleka Mahakamani wakati anakiuka sheria na kanuni ya makusanyo ya fedha hizo za property tax. (Makofi)

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la Mheshimiwa Gashaza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa maelekezo ya Serikali na sheria iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu ilikuwa kwamba majengo yote ambayo hayajafanyiwa tathmini yatatozwa flat rate ya Sh.10,000 kwa majengo ya kawaida na kila ghorofa litatozwa Sh.50,000, kama tu halijafanyiwa tathmini. Kwa majengo yanayotozwa zaidi ya pesa hiyo ni majengo yaliyofanyiwa tathmini, ndiyo sheria iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu inavyosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri tajwa kwamba kama anakwenda kinyume na hivyo, anatakiwa kuwashirikisha wananchi wake kwamba tathmini imeshafanyika na kinachotozwa ni kodi stahiki. Kama tathmini haijafanyika, hatakiwi kutoza kodi hiyo anayoitoza. Pia sheria iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu, iliainisha ni nyumba za aina gani. Kwa hiyo, namwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri husika aweze kufuata sheria na taratibu.