Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE (K.n.y. LAMECK O. AIRO) aliuliza:- Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Rorya ilianzishwa mwaka 2007 na ina ukubwa wa kilometa za mraba 9,345 na idadi ya watu wapatao 400,000, lakini inakabiliwa na tatizo la uhaba wa watumishi katika Mahakama za Mwanzo za Kineri, Ryagoro, Obilinju na Shirati; hadi sasa Wilaya ya Rorya inatumia Mahakama ya Wilaya ya Tarime hali inayosababisha kesi kuchelewa kusikilizwa kwa wakati:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Mahakama ya Wilaya kwenye Jimbo la Rorya?
Supplementary Question 1
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nadhani sasa umefika wakati kwa Serikali kuamua kuangalia haya mambo ya majengo ya Mahakama kwa sababu duniani kote haki ndiyo inajaaliwa, lakini kumekuwa tu na mazoea ya kujibu kwa sababu nimemuona Mheshimiwa Lameck Airo akiwa na hoja hii miaka mitatu iliyopita na ni miaka 11 sasa toka Wilaya hii ianzishwe. Sasa uhakika ni upi? Kila mwaka anauliza wanasema mwaka unaofuata, kila mwaka anauliza anaambiwa mwaka unaofuata. Sasa Waziri atuthibitishie kwamba ni kweli bajeti inayokuja hiyo Mahakama itajengwa kwa Wilaya ya Rorya.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Jimbo la Bunda kuna Mahakama ya Nyamswa, imekuwepo muda mrefu sana hiyo Mahakama ilijengwa na Mtemi Makongoro miaka hiyo mpaka leo, ni lini sasa Serikali itaenda kukarabati ile Mahakama na kuifanya iwe ya kisasa kwa ajili ya kusaidia watu wa Jimbo la Bunda? (Makofi)
Name
Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilosa
Answer
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimhakikishie Mbunge aliyeuliza swali kwamba Mahakama hiyo itajengwa katika mwaka huo wa 2019/2020 na siyo Mahakama hiyo tu bali Mahakama zote ambazo zimepangwa kujengwa katika mwaka huo kwa Mkoa wa Arusha ikiwa ni Arumeru na Ngorongoro; kwa Mkoa wa Dodoma ikiwa Bahi; kwa Mkoa wa Geita ikiwa Geita; kwa Mkoa wa Kagera ikiwa ni Muleba, Bukoba, Ngara, kwa Mkoa wa katavi ikiwa ni Mpanda na Tanganyika; na kwa Mkoa wa Kigoma ikiwa ni Uvinza na Buhigwe.
Vile vile kwa Mkoa wa Kilimanjaro ikiwa ni Same; kwa Mkoa wa Lindi ikiwa ni Nachingwea; kwa Mkoa wa Manyara, Babati, Hanang’, kwa Mkoa wa Mara ni Rorya na Butiama; kwa Mkoa wa Mbeya itakuwa Rungwe; kwa Mkoa wa Morogoro Gairo, Mvomero, Morogoro, Malinyi; kwa Mkoa wa Mtwara, Newala, Mtwara, Tandahimba; kwa Mkoa wa Mwanza, Kwimba; zote hizo ni Mahakama ambazo zitajengwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 na fedha yake inatokana na mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo vyanzo vya fedha vipo na bado zipo Wilaya nyingine nyingi ambazo Mahakama zitajengwa mwaka huu wa 2019/2020. Kwa hiyo ningependa nimhakikishie hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mahakama ya Nyamswa, kabla ya Bunge hili kuanza nilifanya ziara ya Mkoa wa Mara na mahali ambapo nilipita pia ni Nyamswa. Hili ni jengo la zamani ambalo linahitaji kukarabatiwa na hilo litatafutiwa fedha katika mpango wa dharura, itakapopatikana ili Mahakama hiyo ya Nyamswa iweze kukarabatiwa. (Makofi)
Name
Selemani Moshi Kakoso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Vijijini
Primary Question
MHE. BONIPHACE M. GETERE (K.n.y. LAMECK O. AIRO) aliuliza:- Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Rorya ilianzishwa mwaka 2007 na ina ukubwa wa kilometa za mraba 9,345 na idadi ya watu wapatao 400,000, lakini inakabiliwa na tatizo la uhaba wa watumishi katika Mahakama za Mwanzo za Kineri, Ryagoro, Obilinju na Shirati; hadi sasa Wilaya ya Rorya inatumia Mahakama ya Wilaya ya Tarime hali inayosababisha kesi kuchelewa kusikilizwa kwa wakati:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Mahakama ya Wilaya kwenye Jimbo la Rorya?
Supplementary Question 2
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Wilaya ya Tanganyika ni Wilaya ambayo haina Mahakama ya Wilaya, sambamba na Mahakama za Mwanzo ni zile ambazo zimechakaa na hazina watumishi wa kuzifanyia kazi hizo Mahakama. Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa Mahakama za Mwanzo sambamba na Mahakama ya Wilaya na ujenzi wa Mahakama ya Wilaya? Ahsante. (Makofi)
Name
Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilosa
Answer
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Tanganyika itajengwa mwaka 2019/2020 na kama nilivyosema fedha imepatikana kwa hiyo tuna uhakika kwamba Mahakama hiyo itajengwa kwa kipindi hicho huko Tanganyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu watumishi wa Mahakama, ningependa kusema kwamba upo upungufu wa watumishi wa Mahakama ya Mwanzo 3,000 kwa sababu sasa hivi wako watumishi 6,000 na wanahitajika watumishi wengine 3,000. Wizara inaendelea kuwasiliana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupata vibali vya ajira. Mara vibali hivyo vitakapopatikana miongoni mwa Mahakama ambazo zitapewa kipaumbele ni Mahakama za Mwanzo naamini pia zitagusa Wilaya ya Tanganyika. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved