Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itapitia upya Sera ya Michezo nchini?
Supplementary Question 1
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii.
Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini hapo utaona amesema kwamba muda mfupi ujao watakuwa wamekamilisha ukusanyaji wa maoni ya wadau.
Swali langu la kwanza, je, wadau ambao ni Waheshimiwa Wabunge na ambao ni wawakilishi wa wananchi mpaka sasa naona bado hatujashirikishwa, haoni kwamba kuliacha kundi kubwa kama hili kunaweza kukaweka matobo tena kwenye sera ambayo inarekebishwa?
Swali la pili, je, ni kwa kiasi Serikali itachukua wajibu hasa kuhakikisha kwamba michezo ya kubahatisha inakuwa sehemu katika sera hii mpya ili kutanua mfuko wa michezo na kuweza kutoa udhamini wa kutosha katika michezo ili hata hawa wanamichezo wasiwe wanajiandaa wenyewe na wakati wakileta sifa za Taifa tunazipokea kama nchi? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba rasimu ya sera imejadiliwa na wadau mbalimbali, lakini hatujaleta Bungeni na siyo kawaida. Kutokana na umuhimu wa Bunge hili na vilevile mchango ambao kwa kweli mara nyingi unakuwa umefanyiwa kazi na Waheshimiwa Wabunge tutaangalia uwezekano wa kabla ya kufikia mwisho tuweze kupata mawazo ya Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, pili kuhusu michezo ya kubahatisha ni kweli kabisa katika sera tuliyonayo sasa hivi ya mwaka 1995, michezo ya kubahatisha siyo sehemu ya michezo na tumechukua hatua ya kuingia katika mabadiliko ya sheria mbalimbali ambayo yatawasilishwa leo Bungeni hapa tunafanya mabadiliko ya sheria hiyo ili michezo ya kubahatisha nayo iwe sehemu ya michezo na iweze kuchangia katika maendeleo ya michezo nchini.
Name
Ally Abdulla Ally Saleh
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Malindi
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itapitia upya Sera ya Michezo nchini?
Supplementary Question 2
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, pamoja na sifa nyingi Mheshimiwa Waziri alizozimimina kwa bondia Hassani Mwakinyo, kama ulivyosema ni kwamba hajulikani, hata nchi ilikuwa haijui kama anapigana mpaka jana usiku baada ya kutoka matokeo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia katika Kombe la Dunia mchezaji mwingine kutoka Tanga alijitokeza akichezea timu ya Denmark tukabaki tunauma vidole tu, hatukujua kwamba mchezaji yule yupo na anaweza kuisaidia Tanzania.
Mheshimiwa Spika, je, Mheshimiwa Waziri haoni sasa kuna haja ya kuwa na kanzi data endelevu ili kufuatilia vipaji vya watoto wetu wanaozaliwa nje, kuwashawishi kuja kuchezea Tanzania katika timu mbalimbali? kanzi data endelevu? (Makofi)
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, naomba tu nimtaarifu Mheshimiwa Ally Saleh kwamba mwanamasumbwi Mwakinyo katika tasnia ya michezo tulikuwa tunamfahamu kabla ya ushindi wake mkubwa, alikuwa Bingwa wa WBA Bara la Afrika sasa huyu mtu Bingwa wa Afrika, usipomjua sasa na wewe lakini tulikuwa tunamtambua.
Mheshimiwa Spika, lingine nimeeleza kwamba katika Wanamasumbwi 1,854 wa Welterweight katika dunia alikuwa wa 174, hapo pia siyo padogo ni pakubwa. Kwa hiyo, tumpongeze tu huyu kijana na tunachukua hatua kweli sasa hivi kuhakikisha kwamba vijana wetu wengi wanaofanya vizuri katika michezo duniani tunawatambua na tunaendeleza vipaji vyao.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Ally Saleh kwamba hatua hizo tumeshachukua na utaona baada ya muda siyo mrefu kwamba tunawakusanya wote kuweza kuchangia maendeleo ya michezo hapa nchini.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved