Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Innocent Sebba Bilakwate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyerwa

Primary Question

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itafungua Ofisi za TANESCO Wilayani Kyerwa ili kuwafikishia karibu wananchi huduma zitolewazo na TANESCO, kama vile kununua umeme, kubadilisha mita na huduma nyingine?

Supplementary Question 1

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya umeme kwa Kyerwa ni makubwa sana, yako maeneo mengi ambayo hayafikiwa kabisa kama Kata ya Bugomola, Kibale, Businde na Bugara na maeneo mengine mengi hayajafikiwa. Ni kwa nini Wizara isiruhusu TANESCO, REA wanapomaliza kupitisha line kuu, Wizara isiruhusu TANESCO wakaanza kuwafungia umeme wananchi ambao wanahitaji umeme?
Swali la pili, REA Awamu ya Pili ambayo kwetu Kyerwa ni REA Awamu ya Kwanza kwa sababu ndipo umeme ulipopelekwa huyu Mkandarasi amesuasua sana mpaka sasa ameshindwa maeneo mengi, wako wananchi wengi ambao wamelipia mpaka sasa hawajafungiwa miaka miwili.
Je, ni hatua zipi zinachukuliwa kwa Mkandarasi huyu ambaye inaonekana ameshindwa kufanya kazi? (Makofi)

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bilakwate naye pia nimpongeze kwa namna ambavyo amefuatilia masuala la nishati katika Jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza lilijielekeza kwenye mahitaji ya umeme, kwa nini TANESCO isiendelee kuwaunganisha wananchi wa maeneo hayo wanaopenda umeme. Napenda nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli katika Mkoa wa Kagera, Mkoa ambao pia ulikuwa haujaunganishwa kwenye gridi ya Taifa tumeunganisha Wilaya za Ngara mpaka Muleba na tunatarajia kukamilisha mpaka Bukoba Mjini.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uunganishwaji wa gridi ya Taifa katika maeneo hayo kumejitokeza mahitaji na tumeendelea kuwapa maelekezo TANESCO kwamba inapotokea fursa siyo lazima kusubiri miradi ya REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, kama kweli wapo wananchi wa Wilaya ya Kyerwa wanahitaji umeme na wao hoja siyo kusubiri umeme wa REA ambapo una bei nafuu wako tayari kulipia hata gharama za kuunganishwa umeme na TANESCO, naielekeza TANESCO ifanye upembuzi yakinifu na iwapelekee umeme wananchi hao kwasababu wao kwao umeme hawaangalii hoja kwamba ni wa REA au ni umeme kupitia TANESCO.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, natambua Kata alizozitaja Mheshimiwa na ni kweli mpaka sasa hivi hazijasambaziwa umeme. Natambua uwepo wa Mkandarasi Makuroi katika Mkoa wa Kagera, lakini ni ukweli nakiri kwamba katika Wilaya zingine mkandarasi yule hajafanya vizuri, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tulimuita Makuroi kwa sababu anafanya pia na Mkoa wa Rukwa, na mimi nilipata fursa ya kutembelea Mkoa wa Rukwa nikaona ni namna gani anavyolegalega lakini kwa sasa ameshaagiza magari na nimeyathibitisha ana magari mengi tu ya kusambaza nguzo na tulithibisha order ambazo amezitoa katika viwanda mbalimbali vya nguzo vya Mkoa wa Iringa, kwa sasa hivi kwa kweli tumemuelekeza na wakandarasi wote wa miradi hii kwamba lazima kila Wilaya kuwe na genge lake na wasijielekeze sehemu moja.
Kwa hiyo, naomba nimthibitishe Mheshimiwa Mbunge baada ya jibu au baada ya kikao hiki tukutane ili tuendelee na mikakati yakuwasimamia wakandarasi wote. Ahsante.

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itafungua Ofisi za TANESCO Wilayani Kyerwa ili kuwafikishia karibu wananchi huduma zitolewazo na TANESCO, kama vile kununua umeme, kubadilisha mita na huduma nyingine?

Supplementary Question 2

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Tarime Mjini, Kata za Nkende, Kenyemanyori, Kitare, Nyamisangura na Turwa pamoja na Nyandoto hazina umeme kabisa, Bunge lililopita niliuliza swali kama hili na Naibu Waziri akaahidi atatembelea Tarime ili kuweza kuona wakandarasi wa REA ambao tangu mwaka 2016 walitakiwa watekeleze huu mradi, lakini mpaka leo ni Kata ya Nyandoto ndiyo tumeona sasa wameanza kufanyakazi.
Je, ni kwa nini Naibu Waziri hukuweza kutekeleza ile ahadi ambayo uliahidi kwa wana Tarime ili waweze kupata huu umeme?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru kwa kutambua kwamba kazi imeanza ka Kata ya Nyandoto kama alivyoitaja, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kuwa ahadi yangu ya kutembelea Jimbo la Tarime Mjini na Mkoa wa Mara iko pale pale ila kutokana tu muingiliano wa ratiba, lakini kwa kuwa kazi zetu ziko site naomba nimthibitishie baada ya Bunge hili nitatembelea Wilaya hiyo ya Tarime na Wilaya zingine za Mkoa wa Mara kuhamasisha na kukagua miradi hii na kuwapa shime wakandarasi wafanyekazi kwa haraka na kama inavyokusudiwa. Ahsante.

Name

Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Primary Question

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itafungua Ofisi za TANESCO Wilayani Kyerwa ili kuwafikishia karibu wananchi huduma zitolewazo na TANESCO, kama vile kununua umeme, kubadilisha mita na huduma nyingine?

Supplementary Question 3

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nami naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kigoma tuko off grid, kuna mradi wetu mkubwa sana wa Malagarasi ambao tuliambiwa ungeanza quarter hii ya kwanza ya financial year hii. Ningependa kujua kutoka kwa Waziri ni lini mradi sasa wa Malagarasi mini-hydro utaanza ili tuanze kuwa na chanzo cha uhakika cha umeme katika Mkoa wa Kigoma?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ameuliza ni lini mradi huu wa Malagarasi utaanza. Kama ambavyo tuliwasilisha kwenye bajeti yetu ya Bunge hili na ikaidhinishwa na Bunge lako tukufu kwamba mradi huu utaanza kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019, lakini jambo kubwa hapa amelizungumzia kwamba Mkoa huu upo off grid, naomba nilitaarifu Bunge lako tukufu, hivi karibuni Benki ya Dunia imetoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa line inayotoka Iringa – Mbeya - Sumbawanga lakini pia kipande cha Nyakanazi - Kigoma kimepata ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, kwa hiyo, kwa vyovyote vile Mkoa huu tunaanza kuingia kwenye gridi kutokana na miradi hiyo, wananchi wa Kigoma niwathibitishie kwamba kwa kweli Serikali ya Awamu ya Tano inafanyakazi kuhakikisha Mkoa huu unaingia kwenye Gridi ya Taifa. Ahsante. (Makofi)