Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Primary Question

MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, Serikali itapeleka lini gari la wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Chiwale kwani ni zaidi ya miaka miwili sasa baada ya gari lililokuwepo kuungua moto?

Supplementary Question 1

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze tu kuweka taarifa sahihi kadri ya majibu ya Mheshimiwa Waziri hapa, kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ina Vituo vya Afya vinne tu ambapo viwili ni vya Serikali na viwili ni vya mission ya Wakatoliki vikiwemo Kituo cha Namombwe na Lukuledi na siyo vituo 33.
Mheshimiwa Spika, suala la gari la wagonjwa la Kituo cha Afya cha Chiwale ambalo liliungua moto mwaka 2010, wananchi waliunguza moto pale na walioliunguza moto gari hilo siyo wananchi wote wa Chiwale isipokuwa ni watu wachache ambao hawakuwa na nia njema wakati huo, lakini Serikali inaonekana kwamba imekuwa ikitumia jambo hili kama adhabu kwa ajili ya watu wa Chiwale.
Mheshimiwa Spika, sasa nataka kupata kauli ya Serikali na tunafahamu kabisa kwamba mapato ya Halmashauri sasa hivi yamechukuliwa na Serikali Kuu, kwa hiyo, isingekuwa rahisi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kuanza kutenga pesa ukizingatia pia ahadi ya Waziri Mkuu wakati tunafanya uzinduzi wa wodi ya akina mama kwenye Hospitali ya Chiwale…
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu, Serikali, pamoja na hili inalolieleza, vipi, inaweza kutekeleza ile ahadi ya Waziri Mkuu ya kuweza kuleta gari kwenye zahanati ya Chiwale?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama utakumbuka mwaka 2017 kwenye bajeti iliyopita, Serikali ilitenga shilingi milioni 70 kutoka kwenye basket fund kwa ajili ya kudhamini ujenzi wa Kituo cha Afya cha Lukuledi ambapo mpaka sasa hivi naongea hapa, wananchi wako pale wakijitolea pamoja na nguvu ya Ofisi ya Mfuko wa Mbunge. Sasa swali langu ni je, ni lini ahadi ya shilingi milioni 70 ya basket fund itapelekwa Lukuledi kwa ajili ya kuwasaidia na kuwaunga mkono wananchi wale? (Makofi)

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, katika majibu yangu ya msingi nimesema kuna vituo vya kutolea huduma za afya vitatu, sijasema vituo vya afya. Kwa hiyo, nilikuwa niko sahihi katika jibu nililokuwa nimetoa.
Mheshimiwa Spika, katika maswali yake mawili, kwanza anasema Halmashauri yake haina uwezo wa kutenga fedha kwa ajili ya kununua ambulance ambapo lengo la fedha hizo ni kwa ajili ya kusaidia wananchi wanaohitaji huduma ya afya.
Mheshimiwa Spika, ni jana tu nilikuwa naongea na Mkurugenzi wa Halmashauri; uwezo wa Halmashauri wanakusanya jumla ya shilingi bilioni 2.7. Nia ya dhati ikiwepo wakati inasubiriwa ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kutenga pesa kwa ajili ya kununua gari kwa ajili ya wagonjwa kutoka kwenye shilingi bilioni 2.7 inawezekana kabisa.
Mheshimiwa Spika, ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu itatekelezwa kwa kadri pesa zitakavyopatikana, lakini siyo vibaya kama wakatenga kutoka kwenye bilioni 2.7 kwa ajili ya ambulance.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, anasema kwamba walishaanza ujenzi na tayari kuna ahadi ya shilingi milioni 70 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa zahanati au kituo cha afya.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge; ni azma ya Serikali inayoongozwa na CCM kuhakikisha kwamba huduma za afya zinaboreshwa na kusogezwa kwa wananchi. Kwa hiyo, avute subira. Azma yetu ndani ya miaka mitano ambayo ndiyo ahadi yetu na sisi kwa wananchi, tutatekeleza.