Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ally Abdulla Ally Saleh
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Malindi
Primary Question
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:- Mchezo wa chess au sataranji unakuza akili, uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi na ni mzuri sana kwa vijana ambao wanakulia na kuingia hasa katika masomo ya sayansi na ufundi. (a) Je, mchezo huo umejikita kiasi gani hapa nchini hadi sasa? (b) Je, kunaweza kuwa na mipango ya kufanya juu ya mchezo huo kuwa wa lazima na sehemu ya mtaala kwa kuiga hasa nchi za Ulaya ya Mashariki?
Supplementary Question 1
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mchezo wa chess unachezwa na karibu watu milioni 800 duniani kote, lakini pia katika hali ya ushindani wa hali ya juu unachezwa na karibu watu milioni 20. Pia kuna chess olympia yaani olympic ya chess peke yake. Kwa jibu hili la Serikali, sioni nia yao kama wanataka mchezo huu ukue ufikie katika huo ukubwa (magnitude) ambayo nimeielezea kwa sababu wanasema kwamba ukuzwe na wadau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali iko tayari; kwa sababu mchezo huu hauna gharama kubwa katika kuuwekeza, ipo tayari kuwashawishi Cooperate Tanzania iuchukue mchezo huu, iukuze na uweze kuchezwa katika upana mkubwa angalau tuwakute wenzetu Kenya, Uganda na Zambia majirani zetu ambao wapo mbele?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba mchezo huu unakuza akili na ufikiri, lakini mchezo huu maumbile yake unafundisha namna ya kujihami na namna ya mbinu za kijeshi. Je, Serikali iko tayari kutumia nafasi yake kuona kwamba mchezo huu unachezwa katika hali ya kukuza vyombo vya ulinzi? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba tu nisisitize kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi kwamba kwa kweli hakuna mchezo wowote hapa nchini uliokuzwa na Serikali bila wadau, haitawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Ally Saleh ajitahidi kwa nafasi yake ya Ubunge kuhimiza wadau mbalimbali waweze kuubeba huu mchezo kama michezo mingine inavyofanyika na Serikali tupo tayari kutengeneza miundombinu sahihi na mazingira ya kuweza kuhakikisha kwamba mchezo huu unakua kwa kasi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mchezo wa chess ni kweli kabisa nakubaliana naye kwamba ni mchezo ambao unahitaji akili, kama vilevile ambavyo mchezo wetu wa utamaduni wa bao unavyohitaji akili katika kuucheza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nimefurahi sana wadau wa bao wameamua sasa huu mchezo uende Kitaifa. Nampongeza sana mwanabao mashughuli hapa nchini Mandei Likwepa na wenzake waendelee na sisi tutawasaidia kuweza kuuhamasisha huu mchezo ambao ndiyo chess ya Kiafrika. Nina uhakika tukiuongezea vilevile manjonjo mbalimbali unaweza kuwa pengine bora kupita hata huo wa chess kwa sababu hatujaufanyika kazi vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalizie tu kwa kusema kwamba tunakubali mchezo wa chess ni muhimu, ni mkubwa na unahitaji akili hata kwa majeshi ungefaa sana, lakini hata kwa wanafunzi wetu kutoka shule ya msingi mpaka Vyuo Vikuu unafaa sana, lakini naomba wadau wawe mstari wa mbele badala ya kuisubiri Serikali ndiyo itangulie mbele katika mchezo huu.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved