Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:- Tanzania inayo makabila yapatayo 124 yanaongea lugha tofauti na yanazo mila tofauti ambazo wamekuwa wakiziheshimu tangu enzi za mababu:- (a) Je, ni lini Serikali itaandika lugha za makabila hayo ili yasiweze kupotea kwenye uso wa dunia? (b) Je, ni lini Serikali itaandika historia kwa kila kabila nchini ili vijana wanaokua waweze kujua tamaduni za makabila yao?

Supplementary Question 1

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mila na desturi za makabila yetu ya Tanzania zinaendelea kupotea kwa kasi kubwa; na kwa kuwa vijana wetu wameingia kwenye utandawazi wa kuiga mila za kigeni mpaka wanaiga mambo ambayo sio utamaduni wetu. Kwa mfano, kumekuwa na wimbi la vijana wa Tanzania kutaka mabadiliko ya ndoa za jinsia moja, mwanaume kwa mwanaume au mwanamke kwa mwanamke ambazo siyo desturi na mila zetu za Tanzania kama jinsi tunavyoishi na makabila yetu yalivyo. Je, ni lini Serikali itawatambua rasmi Machifu na Watemi ili waweze kutoa mchango wao kwenye jamii kurekebisha na kufundisha mila na desturi zetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa mikoa mingi ya Tanzania haina nyumba za makumbusho za kuhifadhi hizo kanzidata za mila na desturi za makabila tofauti. Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za makumbusho kwenye mikoa yote ya Tanzania? (Makofi)

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Restituta Mbogo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ametaka kujua ni lini Serikali itawatambua rasmi Machifu pamoja na Watemi. Niseme kwamba si kwamba Serikali haiwatambui Machifu pamoja na Watemi ambao tunao na ndiyo maana katika shughuli mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali watu hawa wameendelea kualikwa ikiwepo shughuli ya Mwenge. Kwa hiyo, ni kwamba Serikali inawatambua na itazidi kuwatambua Machifu na Watemi kwa sababu ni njia mojawapo ya kuendelea kuenzi na kudumisha mila pamoja na tamaduni zetu.
Mheshimiwa Spika, swali la pili anataka kujua kwamba ni lini Serikali itajenga maeneo ya makumbusho kwa ajili ya kuhifadhi mila na tamaduni. Kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi kwamba sisi kama Serikali ni waratibu pamoja na wasimamizi wa sera na sheria zinazohusiana na masuala mazima ya utamaduni, wamiliki wakubwa wa utamaduni ni jamii kwa maana ya wananchi. Kwa hiyo, ni jukumu letu sisi sote kuhakikisha kwamba tunashirikiana pamoja na Serikali kujenga na kudumisha mila na tamaduni za Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, pia kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi, nitoe wito kwa mashirika yote ya umma na ya kiserikali na watu binafsi kuhakikisha kwamba tunashirikiana kwa pamoja kudumisha mila pamoja na tamaduni ikiwepo suala ambalo ni muhimu sana la kujenga makumbusho kwa ajili ya kuhifadhi mila pamoja tamaduni zetu. Ahsante.

WAZIRI HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO:
Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kunipa fursa hii. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda tu niongeze kwamba wiki iliyopita nilipata bahati kubwa ya kuhudhuria Maadhimisho ya Kituo cha Kumbukumbu ya Utamaduni wa Kabila la Wasukuma huko Bujora, Mwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kilichonifurahisha sana ni ushiriki mkubwa wa Machifu wa Kisukuma, wote walikusanyika pale. Wana Umoja wao unaitwa Bubobatemi-Babusukuma. Waliweza hata kunipa cheo pale kuwa Manji Mkuu wa ngoma moja pale na ni cheo kikubwa sana hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka tu kusisitiza kwamba nafasi ya Machifu katika kudumisha utamaduni wa Tanzania tunaiona. Nadhani hili suala tutaendelea kuliangalia kwa umakini na kulileta lipate mjadala mpana tuweze kuiona nafasi yao kabisa ambayo itaweza kujikita hata kisheria.
Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kusema kwamba Waheshimiwa Wabunge wametoa mchango mkubwa sana katika hili eneo hasa tukizingatia ukuzaji wa utamaduni Mkoa wa Songea, Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya, Tamasha la Utalii Nyasa; Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro, Majimaji Selebuka; Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson ambaye kila mwaka naye anaazimisha ngoma za kiutamaduni Mkoa wa Mbeya. Ningeoomba Waheshimiwa Wabunge wote tuingie katika kuhamasisha utamaduni katika maeneo yetu. (Makofi)

Name

Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Primary Question

MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:- Tanzania inayo makabila yapatayo 124 yanaongea lugha tofauti na yanazo mila tofauti ambazo wamekuwa wakiziheshimu tangu enzi za mababu:- (a) Je, ni lini Serikali itaandika lugha za makabila hayo ili yasiweze kupotea kwenye uso wa dunia? (b) Je, ni lini Serikali itaandika historia kwa kila kabila nchini ili vijana wanaokua waweze kujua tamaduni za makabila yao?

Supplementary Question 2

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona, naomba niulize swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Balozi wa Namibia alifanya ziara katika Tarafa ya Kwamtoro na kukutana na Wazee wa Kabila la Kisandawe. Moja kati ya maelezo yake ni kwamba lugha wanayoongea Wasandawe inafanana na lugha wanayoongea watu wa Kusini mwa Namibia halikadhalika na watu wa kabila la Xhosa kule Afrika ya Kusini. Alisema yuko tayari kuwachukua Wazee wa Kisandawe kwenda kule Namibia kwa ajili ya kutambuana na ndugu zao. Je, Serikali haioni kwamba upo umuhimu sasa wa kuangalia baadhi ya makabila ya Tanzania na makabila mengine Afrika ili kujenga mahusiano?

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Nkamia, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mkamia Serikali inaona kwamba kuna umuhimu mkubwa kwa sababu tunatambua kwamba lugha zote ambazo zipo hususani lugha za Kiafrika ni lugha za Kibantu ambazo zina mwingiliano mkubwa sana. kwa hiyo, sisi kama Serikali tunatambua kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuangalia hizi lugha ambazo zipo katika nchi yetu ya Tanzania namna ambavyo zinahusiana na lugha zingine ambazo zipo kwenye nchi zingine. Kwa hiyo, niseme kwamba wazo lake ni zuri na sisi kama Wizara tumelipokea na tunaahidi kwamba tutalifanyia kazi. Ahsante.