Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. OMAR A. KIGODA) aliuliza:- Kumekuwa na utekelezaji hafifu wa kusaidia akinamama na vijana kutoka kwenye ile asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri:- Je, Serikali ina tathmini yoyote ya jinsi gani agizo hilo limetekelezwa kwa kila halmashauri?
Supplementary Question 1
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa, Serikali imenyang’anya vyanzo vya mapato vya halmashauri lakini pia imeshusha asilimia za mazao hasa ya kibiashara kutoka asilimia 5 mpaka 3, hivyo halmashauri nyingi kushindwa kutoa hii asilimia 10. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kusaidia kuongeza ruzuku katika eneo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa, zipo halmashauri ambazo zinategemea mazao ya kilimo pekee, kwa mfano Halmashauri ya Lushoto, Halmashauri ya Handeni na nyinginezo na zipo halmashauri ambazo zina rasilimali kama madini, hivyo mfuko huu unakuwa hauna ulingano kwa maana kwamba yapo maeneo ambayo wanapata mapato makubwa na mengine wanapata mapato kidogo sana. Hatuoni kwamba kwa kufanya hivi tunaleta misingi ya ubaguzi katika pato la Taifa? Ahsante.
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Shangazi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza amesema kwamba, kuna baadhi ya vyanzo vya mapato halmashauri zimenyang’anywa. Nataka nimhakikishie kwamba, utaratibu wa Serikali ni mzuri. Katika baadhi ya vyanzo ambavyo vimechukuliwa, kwa mfano, vinavyokusanywa na TRA, bajeti ya halmashauri inakuwa iko palepale na baada ya ukusanyaji bajeti ambayo ilitengwa huwa inarudishwa kwa halmashauri. Kuhusu kwamba kwa nini tusiweke ruzuku maalum ili kufidia, nadhani ni wazo ambalo tunaweza tukalifanyia kazi kwa mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili kwamba baadhi ya halmashauri mapato ni kidogo ukilinganisha na halmashauri nyingine. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi na Waheshimiwa Wabunge kwamba katika ukokotoaji ambao tutaufanya hivi karibuni, kama sehemu ya kuweka utaratibu mzuri zaidi wa kuziangalia hizi halmashauri zetu. Tutaangalia utaratibu ambao ni mzuri zaidi ili kusudi halmashauri ambazo zina uwezo mkubwa na halmashauri ambazo hazina uwezo kabisa tuangalie namna ya kutekeleza agizo hilo.
Name
Emmanuel Adamson Mwakasaka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. OMAR A. KIGODA) aliuliza:- Kumekuwa na utekelezaji hafifu wa kusaidia akinamama na vijana kutoka kwenye ile asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri:- Je, Serikali ina tathmini yoyote ya jinsi gani agizo hilo limetekelezwa kwa kila halmashauri?
Supplementary Question 2
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na taarifa mbalimbali kuhusu baadhi ya halmashauri kutoa mikopo hii ya vijana na akina mama kwa upendeleo. Serikali imewahi kulifanyia uchunguzi jambo hili na inasema nini kuhusu suala hili kama kweli lipo katika baadhi ya halmashauri?
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ngazi yetu sisi ya Wizara hivi karibuni hatujawahi kupokea malalamiko ambayo ni ya msingi kabisa kutoka katika halmashauri yoyote, kwamba kuna upendeleo katika utoaji wa mikopo. Kwa sababu utaratibu uliopo kila halmashauri inatakiwa iwe na Kamati ya Mikopo ambayo ndiyo hupitisha mikopo ile na miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ya Mikopo ni Waheshimiwa Madiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nijibu tu kwamba, kwa kweli utaratibu uliopo inawezekana kuna baadhi ya vikundi vikawa havijaguswa kwa mwaka ule husika kwa sababu fedha zenyewe zinakuwa hazitoshi, ni kidogo. Kwa mfano, unaweza ukawa na shilingi bilioni moja ukataka kutoa mikopo kwa vikundi 80 katika halmashauri, lakini halmashauri ina vikundi 600 kwa hiyo ni wazi kwamba kuna baadhi ya vikundi vitakosa. Kwa hiyo, jambo la msingi ambalo nataka nishauri halmashauri ni kwamba wasirudie kuvipa mikopo vikundi ambavyo vilipata mikopo mwaka jana na mwaka huu vikapata, bali vipate ambavyo mwaka jana havikupata. Huo ndiyo utaratibu mzuri zaidi na hiyo ni kupitia Kamati ya Mikopo ya Halmashauri.
Name
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Kigoma Mjini
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. OMAR A. KIGODA) aliuliza:- Kumekuwa na utekelezaji hafifu wa kusaidia akinamama na vijana kutoka kwenye ile asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri:- Je, Serikali ina tathmini yoyote ya jinsi gani agizo hilo limetekelezwa kwa kila halmashauri?
Supplementary Question 3
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ilipitisha Sheria Ndogo ya Nyongeza ya Tozo mbalimbali katika Halmashauri na sheria ile ikasainiwa na Waziri mwenye dhamana wa TAMISEMI. Katika hali ya kushangaza, Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi alikuja Kigoma Machi, 2018 na kutangaza kwamba sheria ile isitekelezwe. Mpaka sasa watendaji wa halmashauri wanaogopa kukusanya ushuru kwa sababu ya agizo la Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi. Serikali inasema nini kuhusu jambo hili?
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kabwe Zuberi Zitto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ambazo tunazo katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI ni kwamba Baraza la Madiwani lilipitisha viwango vya tozo kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, hizo taarifa ndizo tulizonazo na hata Mkuu wa Wilaya ya Kigoma anazo taarifa hio na ametuarifu. Kwa hiyo, hizi taarifa ambazo Mheshimiwa Zitto amezileta ni mpya na yeye ni rafiki yangu, hajawahi hata kuja ofisini kuniambia. Kwa hiyo, tutafuatilia baada ya kuwa amezitoa hapa ili tuone zina ukweli kiasi gani.
Name
Dr. Raphael Masunga Chegeni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. OMAR A. KIGODA) aliuliza:- Kumekuwa na utekelezaji hafifu wa kusaidia akinamama na vijana kutoka kwenye ile asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri:- Je, Serikali ina tathmini yoyote ya jinsi gani agizo hilo limetekelezwa kwa kila halmashauri?
Supplementary Question 4
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami napenda tu kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa halmashauri nyingi kwa sasa hivi ziko taabani, kwa maana kwamba kimapato nyingi zinasuasua; na kwa kuwa Serikali imeendelea kuchukua baadhi ya vyanzo vingi vya halmashauri na hivyo kufanya halmashauri hizi kushindwa kufanya kazi na kutekeleza majukumu yake kama ilivyotakiwa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaamini kwamba kwa mwenendo huu unazidi kuuwa ile dhana ya kugatua madaraka ya D-by-D?
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Chegeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza jukumu la msingi kubwa la Serikali ni kusimamia maendeleo ya wananchi wake wote kwa usawa. Kuna baadhi ya halmashauri unaweza ukakuta katika maeneo yao kuna vyanzo ambavyo vinaweza vikawa vinawapatia mapato ambayo kimsingi yakikusanywa kwa asilimia 80 hadi asilimia 100 yanaweza yakatoa mchango mkubwa sana katika pato la Taifa ili kuweza kuligawanya na halmashauri nyingine ambazo zina matatizo ziweze kupata japo kidogo. Kwa hiyo, huo ndiyo msingi wa baadhi ya kodi kuweza kuchukuliwa kukusanywa na TRA ili kusudi ule mgawanyo wa mapato kitaifa uweze kuwa mzuri zaidi kwa halmashauri zote au kwa maeneo yote, hilo ndio jambo la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na changamoto ambazo zipo katika halmashauri jambo la kwanza ambalo tumewashauri na Kamati ya Bunge imetoa ushauri ndani ya Bunge hili ni kwamba, kila halmashauri wakae chini katika vikao vyao vya mabaraza watathmini vyanzo vya mapato walivyonavyo kwa sababu halmashauri nyingi tu vipo vyanzo vya mapato ambavyo hawavikusanyi. Kwa hiyo, watathmini vyanzo vya mapato walivyonavyo na wanavyokusanya walete Mheshimiwa Waziri aweze kuwapitishia ili kusudi waweze kuongeza wigo wa mapato. Ahsante sana.
Name
Cecilia Daniel Paresso
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. OMAR A. KIGODA) aliuliza:- Kumekuwa na utekelezaji hafifu wa kusaidia akinamama na vijana kutoka kwenye ile asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri:- Je, Serikali ina tathmini yoyote ya jinsi gani agizo hilo limetekelezwa kwa kila halmashauri?
Supplementary Question 5
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu ambayo yamewasilishwa hapa Bungeni na Serikali muda huu yanaeleza kwamba Ofisi ya Rais – TAMISEMI inatengeneza kanuni za kulazimisha halmashauri iweze kutenga hizo fedha kwa ajili ya mfuko huu. Suala si kuwa na kanuni na sheria kali, suala ni kwamba vyanzo vingi vya halmashauri vimechukuliwa na Serikali Kuu hivyo halmashauri inashindwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwapa mikopo wanawake na vijana. Ni kwa nini Serikali sasa, kwanza iache kutengeneza kanuni hizo lakini itenge fedha hizo kutoka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwa sababu mapato yote imeyachukua?
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Paresso na Bunge lako Tukufu kwamba agizo la kutenga asilimia 10 linahusu makusanyo ya ndani. Kama wamekusanya Sh.100 basi asilimia 10 ya Sh.100 watenge hiyo hiyo. Hatujasema kwamba mtu amekusanya Sh.100 atenge Sh.200, hapana. Amekusanya Sh.100 basi atoe asilimia 10 ya hiyo Sh.100 ili kusudi aweze kutoa mikopo kwa vikundi vya vijana na wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri ambayo imekusanya Sh.100,000,000 inatakiwa itoe Sh.10,000,000 kwa ajili ya vikundi vya vijana na wanawake. Kwa hiyo, kama kuna changamoto nyingine, taratibu za mawasiliano ndani ya Serikali Wakurugenzi wa Halmashauri wanazifahamu sana. Ahsante sana.