Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Cecilia Daniel Paresso
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CECILIA D. PARESSO – (K.n.y. MHE. JULIUS K. LAIZER) aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatoa fidia stahiki kwa wananchi ambao mazao yao yaliharibiwa na wanyamapori tangu mwaka 2010 hadi 2017 katika maeneo ya Mswakini, Makuyuni, Naiti, Mbuyuni, Lokisale na maeneo mengine Wilayani Monduli?
Supplementary Question 1
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa, kila mwaka wananchi wa Monduli wamekuwa wakipoteza mali lakini pia kupoteza maisha kutokana na uharibifu huu; na Mheshimiwa Naibu Waziri kutokana na takwimu ulizoziwasilisha hapa si kweli kwamba ni vijiji vyote vimelipwa. Kuna vijiji vya Moita, Naiti, Mswakini, Makuyuni na Isilalei wananchi hawa hawajalipwa fidia kwa mwaka 2014/2015, 2015/2016, 2016/2017. Je, ni lini sasa Serikali mtawalipa wananchi hao ambao wamepata uharibifu mkubwa na wamesubiri kwa muda mrefu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kanuni hii ya Kifuta Jasho na Kifuta Machozi ambayo imekuwa ikitumika kwa wananchi ambao kwa namna moja ama nyingine mazao yao au mali zao zimeharibiwa na wanyamapori katika nchi hii imepitwa na wakati na kwa kweli imewaletea wananchi usumbufu mkubwa sana kwa sababu wananchi hao mali zao zinaharibika kwa kiwango kikubwa na wanachokuja kulipwa hakilingani na uhalisia. Je, Serikali sasa haioni ni wakati mwafaka kuendana na hali ya sasa na thamani ya fedha ya sasa kubadili kanuni hii ili kulipa uhalisia wa uharibifu unaofanywa na wanyamapori?
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba si vijiji vyote ambavyo vimeshalipwa fidia. Hivi sasa naomba nilitaarifu Bunge lako tukufu kwamba madai ambayo yamepokelewa kutoka katika wilaya mbalimbali hapa nchini yalifika takribani 15,370 na madai ambayo yameshalipwa tayari ni 6,185. Kwa hiyo, utaona kwamba kuna madai karibu 9,562 ambayo bado hayajahakikiwa na bado hayajalipwa, hivi sasa zaidi ya shilingi milioni 828 zinadaiwa. Kwa hiyo, baada ya zoezi la uhakiki kukamilika vijiji vyote hivyo vitapata fidia na kifuta machozi hicho ambacho tumekisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kulitaarifu Bunge lako tukufu kwamba hivi sasa tunafanya mapitio ya Kanuni za Kifuta jasho na Kifuta Machozi za Mwaka 2011. Mara tu zitakapokamilika kupitiwa na kuidhinishwa, basi haya masuala yote ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyasema yataangaliwa. Ahsante sana.
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. CECILIA D. PARESSO – (K.n.y. MHE. JULIUS K. LAIZER) aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatoa fidia stahiki kwa wananchi ambao mazao yao yaliharibiwa na wanyamapori tangu mwaka 2010 hadi 2017 katika maeneo ya Mswakini, Makuyuni, Naiti, Mbuyuni, Lokisale na maeneo mengine Wilayani Monduli?
Supplementary Question 2
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, nimshukuru kwanza Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana, lakini kwa ujumla niwashukuru watu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Waziri na viongozi wake wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili la wanyama waharibifu, hasa tembo, katika Jimbo la Bunda na kwa kata tatu ambazo zina vijiji 18 ni kubwa sana. Nikiangalia toka tuanze kulipa haya malipo ya fidia, ni mabilioni ya hela yanaenda na nimeona hapa tumekuwa na mikakati mingi, kuweka ukuta, kuweka pilipili na kuchimba mitaro na wengine huko vijijini kwenye Jimbo la Bunda wanasema tembo hawa hawana uzazi wa mpango, mnasema tembo wamepungua lakini ni wengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuuliza, ni lini sasa mikakati halisi ya Serikali itakuwepo ya kuzuia mnyama tembo ili kutoleta umaskini kwenye maeneo ya kwetu? Ahsante.
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba katika eneo la Serengeti, na hasa katika Jimbo la Bunda kumekuwa na matatizo hayo na changamoto hizo ambazo zimekuwa zikijitokeza. Suala ni lini hasa tutakuja na mipango, sasa hivi tunakuja na mpango mkakati ambao tutausema tutakapokuwa tunawasilisha bajeti yetu ya mwaka 2018/2019, ni hatua gani ambazo tunategemea kuchukua katika maeneo mbalimbali ya Hifadhi za Taifa na maeneo mengine ya mapori ya akiba ili kukabiliana na changamoto hizi za wanyama waharibifu.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba tu aendelee kutusubiri, pale tutakapowasilisha bajeti yetu basi atuunge mkono ilia one hizo hatua ambazo tunakwenda kuchukua ambazo ndizo zitakazokuwa suluhu ya changamoto mbalimbali.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved