Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Primary Question

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. ESTHER M. MATIKO) aliuliza:- Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limejitwalia maeneo ya wananchi wa Kenyambi na Bugosi kinyume kabisa na sheria baada ya kukaribishwa kwa hifadhi ya muda kufuatia kukatika kwa mawasiliano kati ya kambi yao iliyopo Kata ya Nyandoto na Tarime Mjini:- a) Je, ni kwa nini Serikali imeshindwa kuwalipa fidia wananchi hao waliochukuliwa ardhi yao na JWTZ tangu mwaka 2007? b) Je, ni kwa nini JWTZ wasirudi kwenye kambi yao iliyopo Kata ya Nyandoto yenye eneo kubwa kuliko kuchukua maeneo yaliyo katikati ya makazi?

Supplementary Question 1

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wananchi wa Kenyambi na Bugosi huko Tarime wameanza kukata tamaa baada ya huo uthamini uliofanyika tangu mwaka 2013, ni miaka mitano sasa. Bajeti iliyotengwa ya mwaka 2017/2018 ni shilingi bilioni 20, je, katika mwaka huu unaoisha fedha hizi kama zikipatikana wananchi wa Kenyambi na Bugosi huko Tarime watalipwa fidia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa muda mrefu Serikali imekuwa na kawaida wanapochukua maeneo ya wananchi kwa matumizi ya jeshi hawalipi fidia, wanafanya hivyo kwa sababu wananchi hawana cha kufanya. Serikali ituambie, ni kwa nini tangu mwaka 2006 imekuwa ikitoa taarifa ya utekelezaji wa kupima maeneo, kuthamini na kutoa fidia lakini haifanyi hivyo? Ni kwa nini Serikali isifanye utaratibu wa kufanya matembezi ya hisani ili wananchi wapate fidia zao kwa sababu Serikali inaonekana imeshindwa? Nashukuru sana.

Name

Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi kwamba fedha zikipatikana ndiyo kipaumbele kitatolewa kwa wananchi wa eneo hili tunalolizungumzia kwa sababu tumewapa ahadi muda mrefu, tangu mwaka 2013 uthamini umefanyika. Mheshimiwa Mbunge anayehusika, mwenye jimbo lake, mara nyingi amekuwa akiniuliza na mimi huwa nampa majibu kwamba fedha tukizipata basi kipaumbele kitatolewa kwa eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pilli, kwamba Serikali huwa hailipi fidia, kwa kweli lengo la kulipa fidia lipo, lakini kama mnavyotambua kuna changamoto za kibajeti. Ni mategemeo yetu kwamba fedha hizi zikipatikana kwa kweli tutapunguza maeneo mengi sana ambayo yanatudai, kwa sababu hizi shilingi bilioni 20 zikipatikana siyo kwamba tutaweza kufikia maeneo mengi. Ni mategemeo yetu kwamba fedha hizi zitapatikana kama ambavyo Wizara ya Fedha ilishatoa ahadi hapa. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna sababu ya kufanya matembezi ya hisani katika hili, tutakachofanya ni kuendelea kuhimiza wenzetu wa Wizara ya Fedha wakiweza kupata fungu hili basi watupatie ili na sisi tuweze kutimiza ahadi zetu.