Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Prof. Jumanne Abdallah Maghembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Primary Question
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE aliuliza:- Awamu ya III ya REA ilizinduliwa Wilayani Mwanga mnamo Julai, 2017 lakini hadi sasa utekelezaji wake haujaanza; Je ni lini utekelezaji wa mradi huo utaanza?
Supplementary Question 1
MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Spika, kwanza naishukuru sana Wizara na Waziri wa Nishati na Madini, kwa jibu zuri sana ambalo ametupatia.
Mheshimiwa Spika, nina maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, katika maeneo ambayo tayari yamepatiwa umeme kule vijijini, wako wananchi wengi sana ambao bado hawajapatiwa umeme kinyume na ahadi ambazo tumepewa hapa Bungeni kwamba kila mmoja atakayepitiwa na nguzo au waya za umeme na yeye atapata umeme. Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba hawa watu ambao wamepitwa bila kufungiwa umeme wanafungiwa umeme kama wenzao waliofungiwa awali?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Tarafa yetu ya Jipe ambayo ina urefu wa kilomita 70 kuanzia mwanzo mpaka mwisho, viko vijiji viwili ambavyo bado havijahudumiwa na mradi wa REA ambavyo ni Vijiji vya Kwanyange na Karambandea. Serikali ina mpango gani wa kuvihudumia vijiji hivi na kuvipatia umeme?
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayofanya katika Jimbo lake. Nilifanya ziara mwaka jana mwezi kama huu niliona namna ambavyo anashughulika na kero za Nishati katika Jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni kwenye maeneo ambayo yamepitiwa na miundombinu ya umeme mkubwa lakini baadhi ya wananchi hawajapata kuunganishiwa umeme, napenda nimtaarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imepanga Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili baada ya mafanikio ya Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Kwanza.
Mheshimiwa Spika, Mradi huu wa Ujazilizi Awamu ya Pili ambao utaanza Machi, 2019 unahusisha mikoa tisa ya awali ikiwemo Mkoa wa Kilimanjaro lakini baadaye mwezi Julai, 2019 tutaanza Awamu ya Pili katika mikoa iliyosalia. Kwa hiyo, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi ambao hawajapata umeme katika vijiji ambavyo miundombinu ya umeme imefika kupitia Mradi wa Ujazilizi watafikiwa na huduma hii ya nishati.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili linahusiana na vijiji katika Tarafa ya Jipe ambapo Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, Mbunge wa Jimbo la Mwanga anasema bado havijafikiwa na miundombinu ya umeme. Nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba licha ya Mradi wa Ujazilizi, Serikali pia kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza Mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa pili ambapo upembuzi yakinifu umeanza na hivyo vijiji viwili vitafikiwa na miundombinu ya umeme baada ya mradi huo kuanza. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved