Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Musa Rashid Ntimizi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Primary Question
MHE. MUSA E. NTIMIZI aliuliza:- Katika mradi wa kupeleka umeme vijijini, Jimbo la Igalula limepitiwa na umeme katika baadhi ya maeneo ya Kata za Kigwa, Igalula, Goweko na Nsolola tu kati ya Kata kumi na moja za Jimbo hilo:- a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka umeme katka Kata na Vijiji vya Jimbo la Igalula vilivyobaki? b) Katika Kata ya Igalula, Kijiji cha Igalula ambapo kuna bwawa la maji kuna hitaji la nguzo kumi tu kwa ajili ya kusaidia kusukuma mitambo ya maji. Je, Serikali itasaidiaje kupeleka nguzo hizo ili kutatua tatizo hilo?
Supplementary Question 1
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Kwanza nitoe shukrani za dhati kwa ziara ya Mheshimiwa Waziri, alipokuja Jimboni kwangu nilimweleza shida ya umeme katika bwawa la maji na sasa tayari transforma imefungwa na umeme unawaka. Nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina masikitiko kidogo, REA awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu katika Jimbo la Igalula lenye vijiji takriban 98 ni vijiji sita tu ndivyo vimepata umeme katika Jimbo la Igalula; na katika vijiji hivyo sita ni baadhi tu ya maeneo ya vijiji ambavyo vimepata umeme maeneo mengine hayajapata umeme. Kwa mfano, katika Kata ya Igalula, yenye vijiji sita ni kijiji kimoja tu ndiyo kimepata umeme. Je, Serikali haioni usambazaji wa umeme katika Jimbo la Igalula unasuasua na hauridhishi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Waziri alikuja kwenye ziara katika Jimbo la Igalula, alitembelea Kata ya Miswaki, Loya na Lutende. Alijionea hali ya uzalishaji mpunga mkubwa katika eneo lile na halmashauri ilivyowekeza mashine za kisasa za kukoboa mpunga katika eneo lile; akaahidi kupeleka umeme katika kata hizo tatu za Lutende, Loya na Miswaki. Je, ni lini zoezi hili litakamilika na wananchi wa kule waweze kupata umeme? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, kama ambavyo ameeleza kwenye kusoma majibu ya Mheshimiwa Mbunge. Pili, nimpongeze sana Mheshimwa Ntimizi anavyofuatilia maendeleo ya nishati katika Jimbo lake. Sambamba na hilo nipokee shukrani alizotupatia kwa kupeleka maji katika Kata yake ya Igalula na wananchi zaidi ya 1,000 wanapata maji kupitia mradi huo.
Mheshimiwa Spika, na sasa nijielekeze katika maswali yake mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni kuhusiana na vijiji vitano vya Igalula. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge, hivi mkandarasi sasa hivi yuko katika kijiji cha pili katika Kata ya Igalula na vijiji vyote vitano katika Kata ya Igalula vitapelekewa umeme kupitia mradi huu unaoendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, suala la pili; Mheshimiwa Mbunge ni kweli nilitembelea kata ya Lutende, Miswaki pamoja na Loya. Ni maeneo ambayo yana makazi mengi na yana uchumi mzuri. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge, Mradi huu wa kupeleka umeme katika kata hizo tatu tutautoa katika Jimbo la Manonga, Kata ya Simbo na mkandarasi ameshaanza kazi; ingawa kutoka Simbo kuelekea Lutende ni kilometa 20 lakini wakandarasi wameshaanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, kutoka Lutende kwenda Miswaki ni kilometa 27, kutoka Miswaki kwenda Rorya ni kilometa 13 na kuna jumla ya vijiji 14. Nimpe taarifa kwamba transfoma 17 zimeshapelekwa katika kata hizo tatu na wananchi wa kata hizo watapatiwa umeme ndani ya miezi sita ijayo. (Makofi)
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. MUSA E. NTIMIZI aliuliza:- Katika mradi wa kupeleka umeme vijijini, Jimbo la Igalula limepitiwa na umeme katika baadhi ya maeneo ya Kata za Kigwa, Igalula, Goweko na Nsolola tu kati ya Kata kumi na moja za Jimbo hilo:- a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka umeme katka Kata na Vijiji vya Jimbo la Igalula vilivyobaki? b) Katika Kata ya Igalula, Kijiji cha Igalula ambapo kuna bwawa la maji kuna hitaji la nguzo kumi tu kwa ajili ya kusaidia kusukuma mitambo ya maji. Je, Serikali itasaidiaje kupeleka nguzo hizo ili kutatua tatizo hilo?
Supplementary Question 2
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kwanza kabisa ya kuuliza swali katika Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana wana-CCM wote popote walipo kwa kunikaribisha Chama cha Mapinduzi. Nawashukuru wananchi wa Ukonga kuendelea kuniamini, pia namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini kwa kuchukua baadhi ya maeneo ya Jimbo la Ukonga kuingiza kwenye umeme wa peri-urban; eneo la Mbondole, Kitonga, Chanika, Kibanguro, Viwege, Zingiziwa na Buyuni, Mgeule na Mgeule Juu vimeingizwa kwenye peri-urban. Sasa ningependa nijue, ni lini sasa maeneo hayo muhimu katika Jimbo la Ukonga kwa kuwaheshimu watu waliounga mkono juhudu za CCM watapata umeme haraka iwezekanavyo? Ahsante. (Makofi)
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwita, Mbunge wa Jimbo la Ukonga kupitia Chama Cha Mapinduzi na nimpongeze sana kwa kushinda kwa kishindo katika uchaguzi huo. Kwanza ameishukuru Wizara yetu kwa namna ambavyo tumeingiza maeneo ya Jimbo lake la Ukonga kwenye mradi wa peri-urban.
Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Mwita Waitara atakubaliana na mimi tulifanya ziara katika maeneo hayo katika maeneo mbalimbali ambayo ndiyo imekuwa kivutio cha kuipigia kura Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi uliopita. Sasa kazi imeanza ya kupeleka umeme katika maeneo hayo kupitia TANESCO na kwa kupitia mradi wa peri-urban tuko katika hatua za kumpata mkandarasi na hivi karibuni kazi ambazo zimesalia katika maeneo mbalimbali zitakamilika. Hata baada ya Bunge hili pamoja na Mheshimiwa Mbunge tutawasha umeme katika maeneo ya Zingiziwa, Buyuni na Mbondole kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Shirika la Umeme la TANESCO. Ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved