Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Innocent Sebba Bilakwate
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyerwa
Primary Question
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:- Wilaya ya Kyerwa ina Vituo vitatu vya Afya, lakini kituo kimoja ndicho kina uhakika wa kutoa huduma, vilevile kuna uhaba wa watumishi ambao wanafanya kazi kwenye mazingira magumu pamoja na ukosefu wa nyumba za watumishi:- Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na nyumba za watumishi ili kutekeleza Ilani ya CCM na kuondoa adha wanayoipata akina mama, watoto na wananchi wengine kwa ujumla?
Supplementary Question 1
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kututengea hizi pesa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya, lakini kipekee nachukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Jafo kwa jinsi ambavyo nimekuwa nikimsumbua kuhusiana na Vituo vya Afya na Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, kulingana na jiografia ya Wilaya yangu, ninaomba kuuliza swali. Kwa kuwa tuna vituo vitatu kwenye Tarafa nne na kwenye Kata 24: Serikali iko tayari kututengea kituo kingine kimoja? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kyerwa tuna upungufu mkubwa wa watumishi. Kwenye kituo kingine unakuta kuna watumishi wawili kwenye Zahanati moja: Je, Serikali iko tayari kututengea watumishi wa kutosha ili wananchi waweze kupata huduma? (Makofi)
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kwa niaba ya Serikali nipokee pongezi kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge. Katika hali ya kawaida, mtu anayeshukuru tafsiri yake ni kwamba anaomba kingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunaendelea kujenga Vituo vya Afya kwa kadiri nafasi ya kibajeti itakavyoruhusu. Jiografia ya Kyerwa hakika ni jiografia ambayo ina utata mkubwa, Jimbo ni kubwa. Naomba aendelee kuiamini Serikali, kwa kadiri bajeti itakavyoruhusu na tutakavyokuwa tunaendelea kujenga Vituo vya Afya, naye tutamkumbuka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna swali lake la pili; anaomba kuongeza idadi ya watumishi ili waweze kutoa huduma ambayo inastahili kwa wananchi wake. Sasa hivi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeomba kibali cha kuweza kupata nafasi za kuajiri. Kwa kadiri nafasi zitakavyokuwa zimepatikana, hakika katika usambazaji tutahakikisha maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa yanazingatiwa. Naamini na eneo lake ni miongoni mwa maeneo hayo. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika,
kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, ninaomba kutoa maelezo ya nyongeza kuhusu uhaba wa watumishi, hasa afya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, sasa hivi Serikali inafanya jitihada za kujenga Vituo vya Afya na Zahanati nchi nzima. Tunakiri kwamba watumishi hawatoshi, ndiyo maana kwa kushirikiana na TAMISEMI tunafanya utaratibu wa kuongeza. Nimesimama hapa kueleza kwamba, sisi upande wa Wizara ya Utumishi na Utawala Bora tutaweka kwanza kipaumbele katika Zahanati na Vituo vya Afya vipya ambavyo havijaanza kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Viongozi wa Mikoa, Waheshimiwa Wabunge mkiwasimamia, kuhakikisha wanapoleta maombi watuletee kwamba Zahanati mpya inahitaji watumishi kadhaa, Kituo cha Afya kipya kinahitaji watumishi kadhaa. Pamoja na uhaba uliopo, lengo ni kwamba Vituo vyote vya Afya na Zahanati zote mpya zifunguliwe mara moja, ndiyo tutawapa kipaumbele, kwa sababu sehemu nyingine huduma bado zitaendelea kutolewa japo kwa upungufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, labda kwa ruhusa yako pia, nijibu suala la uhaba wa Walimu. Sasa hivi baada ya kufungua mwaka mpya huu wa masomo, Walimu wengi wamestaafu mwaka 2018, wengine wamefariki. Sisi upande wa Utumishi tutaanza kwanza kujaza idadi ya Walimu waliostaafu mwaka 2018, ili tuwe na kiwango cha Walimu kama waliokuwepo mwaka 2018, baada ya hapo tutaendelea na zoezi la kuajiri Walimu wapya.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved