Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Silvestry Fransis Koka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Mjini

Primary Question

MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:- Mradi wa Umeme mkubwa wa msongo wa KVA 400 toka Kinyerezi kupitia Pwani, Morogoro, Singida na Arusha umechukua maeneo ya wananchi kwa muda mrefu bila kuwalipa fidia:- Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kulipa fidia hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. SILYVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nichukue fursa hii kwa dhati kabisa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kazi kubwa anayoifanya katika miradi ya umeme na hususan mradi mkubwa wa Stiegler’s gorge ambao unakwenda kutuondolea gharama kubwa ya umeme hakika ni neema. Nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri ameshatutembelea zaidi ya mara tatu katika Jimbo langu, anachapa kazi na kwa pamoja Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza, pamoja na kuchukua muda mrefu katika fidia hii, lakini wananchi wa Kibaha wana taarifa kwamba wenzao wa Arusha na Singida walikwishakupata malipo, kama hivi ndivyo, je, wanapata malipo kwa ubaguzi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika miradi ya ujazilishaji katika Mji wa Kibaha yaani densification Mitaa ya Muheza, Mbwate, Lumumba, Sagale, Mkombozi, Mbwawa Hekani, Kumba na Mtakuja miradi hii bado haijaanza utekelezaji kama ilivyokuwa imeahaidiwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha miradi hii ambayo wananchi wanaisubiri kwa hamu ili waweze kupata umeme na kukidhi mahitaji yao ya kiuchumi?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Silvestry Koka, ndugu yangu kutoka Jimbo la Kibaha Mjini kuwa kwanza tumepokea pongezi na nichukue fursa hii kumpongeza yeye binafsi Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini pamoja na Waheshimiwa Wabunge wenzake wa Mkoa wa Pwani ambao wanapitiwa na mradi huu akiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Kibaha Vijijini, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze pamoja na dada yangu Mheshimiwa Bonnah, Mbunge wa Jimbo la Segerea kwa kazi ya kuwasemea wananchi wao na kufuatilia masuala ya fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema nimefanya ziara katika maeneo yao mbalimbali, lakini nataka niseme moja ya jambo ambalo limejitokeza baada tu ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano chini ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuja na mapinduzi ya kutaka kutekeleza mradi wa Rufiji Hydro Power Stiegler’s, njia hii ya msongo wa kilovoti 400 ilikuwa inaitwa Kinyerezi – Chalinze - Tanga. Kwa hiyo baada ya kuja na ule mradi ilikuwa lazima sasa kuwe na line ya kilovoti 400 kutoka Rufiji mpaka Chalinze ambayo inaunganishwa na Dodoma na kimsingi kwa ajili pia ya kuwezesha treni yetu ya umeme ambayo kama maelezo yalitolewa inatarajia kuanza kazi Novemba, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na wananchi, nami mwenyewe pia ni muhanga kwa sababu nawakilisha wanawake wa Mkoa wa Pwani. Nataka niseme kwa kweli kwa kuwa mradi huu wa ujenzi wa njia hii ya msongo wa kilovoti 400unaanza kutekelezwa Januari, 2020, hatuwezi kuanza mradi huu bila kuwalipa wananchi fidia. Kwa hiyo kiwango kilichotajwa kwenye jibu langu la msingi cha bilioni 36 na kwamba ndio wakati wake muafaka sasa wa kulipa kwa sababu hata fidia inayolipwa maeneo ya Singida, maeneo ya Mkoa wa Manyara kwa ajili ya njia ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Singida mpaka Namanga ni kwa sababu mradi umeanza kutekelezwa na ndio maana lazima ulipe fidia maana yake ni moja ya masharti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa maeneo haya niliyoyataja, tunawashukuru na tunawaomba radhi kwamba wamechukua muda mrefu lakini wamekuwa na subira, waendelee na kwamba sasa kwa kweli mchakato wa malipo upo mbioni kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ametaja maeneo ya Muheza, Lumumba, Madina, Mtakuja, Mbwawa kote huku mimi na Mheshimiwa Mbunge tulifanya ziara pamoja, nataka niwathibitishie wananchi kwa kazi ambayo Mheshimiwa Mbunge alikuwa anafanya kwamba maeneo haya tuliahidi kuyapelekea umeme kwa mradi wa Peri-urban na huo mradi wa Peri-urban pia unagusa Jimbo ya Ukonga kwa ndugu yangu Mheshimiwa Waitara pia kwa ndugu yangu Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya maeneo ya Kigamboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwa hatua iliyofikiwa, mradi huu unaanza mwezi wa Nne kwa sababu taratibu zote za manunuzi zimekamilika na kwa sasa wakandarasi wale au wale ambao wametenda ipo hatua ya post qualification. Kwa hiyo Serikali imedhamiria kwa dhati kabisa maeneo ambayo yanakua kwa kasi kupelekea mradi wa Peri-urban. Naomba tu waendelee kuvumilia mwezi wa Nne mwishoni utaanza huu mradi. Ahsante sana.

Name

Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Primary Question

MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:- Mradi wa Umeme mkubwa wa msongo wa KVA 400 toka Kinyerezi kupitia Pwani, Morogoro, Singida na Arusha umechukua maeneo ya wananchi kwa muda mrefu bila kuwalipa fidia:- Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kulipa fidia hiyo?

Supplementary Question 2

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona swali hili la Mheshimiwa Koka, tena hili la juzi, lakini katika Jimbo la Mlimba kuna mradi mkubwa wa umeme mkubwa ulikuwa unapelekwa kutoka Kihansi Jimboni Mlimba kwenda Wilaya ya Malinyi, katika mwaka 2014 na mpaka 2016 TANESCO ikakubali kwamba wale watu wanatakiwa walipwe, lakini mpaka leo unavyozungumza wengine wameshakufa, wengine wameshazeeka hawajalipwa hata senti tano. Je, ni lini sasa Serikali itawalipa hawa wananchi au kwa vile wako mbali sanahakuna barabara jamani kosa, letu nini wananchi wa Mlimba?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Susan, Mbunge wa Jimbo la Mlimba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nipokee hii changamoto ambayo ameielezeaMheshimiwa Suzana na nikitambua kwamba kwa kipindi cha Bunge hili la Kumi na Moja, awamu ya kwanza alihudumu Kamati ya Nishati na Madini na nimwahidi kwamba tutaenda kufuatilia kwa sababu maeneo haya anayoyataja na kwa kuwa mradi mkubwa wa Kihansi unaozalisha umeme zaidi ya megawati 180 ni ya wananchi wa maeneo hayo, hivyo tunawategemea sana na wamekuwa watunzaji wazuri wa mazingira na mpaka sasa hivi hatujawahi kupata changamoto yoyote ya kusema labda maji yamepungua katika uzalishaji wa umeme. Kwa hiyo nimwahidi Mheshimiwa Mbunge baada tu ya hapa naomba tufuatilie, kwa sababu hata jana aliniambiakuhusu hili suala ili kuona fidia imefikia wapi, lakini nihakikishe kwamba kama haki hiyo ipo na tahmini ilifanyika Serikali ya Awamu ya Tano inalipa fidia. Ahsante sana.

Name

Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza:- Mradi wa Umeme mkubwa wa msongo wa KVA 400 toka Kinyerezi kupitia Pwani, Morogoro, Singida na Arusha umechukua maeneo ya wananchi kwa muda mrefu bila kuwalipa fidia:- Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kulipa fidia hiyo?

Supplementary Question 3

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nataka kuuliza kuhusu suala la fidia; wananchi wa Mkuranga, Kibiti na Rufiji wanadai fidia zaidi ya miaka mitatu kutoka TANESCO. Sasa kutokana na mradi huu wa umeme wa Kinyerezi, je, ni lini wananchi hawa watalipwa hizo fidia?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mama yetu Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, Mbunge wa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, lakini anahudumu Mikoa ya Pwani na Lindi kama ambavyo ameuliza masuala ya fidia ya mradi wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Somangafungu Kinyerezi. Kimsingi mradi huu fidia yake inalipwa na TANESCO na maeneo ambayo yalipitiwa na mradi huu kuanzia Kilwa, Kibiti, Rufiji, Mkuranga na maeneo ya Mbagala na Ilala Dar es Salaam, nataka nikiri kwamba kutokana na mradi huu takribani gharama yake kama isiyopungua bilioni 50 hivi, lakini TANESCO mpaka sasa hivi wamelipa zaidi ya bilioni 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti,natambua kwamba zipo changamoto za baadhi ya wananchi wachache na hata hivi karibuni tulipanga na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mkuranga kufanya kikao na Menejimenti ya TANESCO ili kuweza kutambua mpango wao mkakati wa kumalizia malipo ambayo yamesalia. Kwa hiyo, nimshukuru kwamba na tunamwalika Mheshimiwa Mbunge, Mama yetu Mama Salma Kikwete na Mheshimiwa Mbunge wa Rufiji na Mheshimiwa Mbunge wa Kilwa katika kikao hiko ili kutambua akina nani wamelipwa, akina nani hawajalipwa kwa sababu zipo changamoto pia katika suala zima la wanaojitokeza. Hata hivyo, nimwahidi kabisa kwamba TANESCO kwa kweli wamejipanga kulipa kwa sababu mradi huu ni lazima utajengwa kutokana na uwekezaji unataka kufanyika Mkoa wa Mtwara wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha megawati 300 na Somangafungu yenyewe wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha megawati 330. Kwa hiyo nimshukuru na kumpongeza kwa swali lake zuri hili. Ahsante sana.