Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Primary Question

MHE. MAULID S. MTULIA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha Sekta ya Michezo kwa kuandaa Wakufunzi wa Michezo, kujenga viwanja vya kisasa na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya michezo?

Supplementary Question 1

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali madogo mawili ya nongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, hivi sasa kuna mwamko mkubwa sana Nchini Tanzania kwa wazazi kutaka watoto wao washiriki kwenye michezo hasa ikichagizwa na mafanikio aliyoyapata kijana wetu Mbwana Samatta kucheza katika ligi ya Uingereza na mimi sasa hivi timu yangu ni Aston Villa, lakini kuna tatizo kubwa la vifaa vya michezo kwa wananchi wetu ili kuweza kushiriki vizuri michezo.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha vifaa vya michezo yote Tanzania vinapatikana kwa urahisi ili wazazi wachochee mchakato huu wa kuwa na wana michezo wengi Nchini Tanzania?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wizara imesema suala la ujenzi wa viwanja ni la wadau na halmashauri na Halmashauri ya Kinondoni imeitikia wito huo kwa kuja na ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu pale Mwenge na vilevile kuna mchakato wa kujenga kituo cha malezi ya watoto ili tupate wachezaji bora kabisa. Serikali inatoa kauli gani kusaidia juhudi hizi ili wanaoonesha nia ya kuleta mabadiliko ya soka wapate kusaidiwa?

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kwa sababu amekuwa ni mdau mkubwa sana wa masuala ya michezo, lakini nadhani hiyo inatokana na kwamba Jimbo lake ni Jimbo ambalo lina wanamichezo wengi pamoja na wasanii wengi. Kwa hiyo naamini kwamba Mheshimiwa Mbunge anafanya kazi nzuri sana na wananchi wake wanajivunia hilo.

Mheshimiwa Spoika, nikija sasa kwenye maswali yake mawili ya nyongeza; swali lake la kwanza amezungumza kwamba ipo changamoto ya vifaa vya michezo; na mimi nikiri kwamba ni kweli kumekuwepo na changamoto ya vifaa vya michezo, lakini kama Serikali hatujakaa kimya na tunayo Sera yetu ya Michezo ya Mwaka 1995 ambayo inazungumza kwamba suala zima la ujenzi wa viwanja pamoja na miundoimbinu yote ya michezo ni suala la Serikali lakini vilevile kwa kushirikiana na wadau.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa upande wetu sisi kama Serikali sasa hivi kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara tumekuwa tukihamasisha sana wafanyabiashara mbalimbali waendelee kuagiza vifaa vya michezo kutoka nje. Kama hiyo haitoshi kama Wizara vilevile kwa kupitia Sera yetu ya Awamu ya Tano ambayo ni Sera ya Viwanda tumekuwa pia tukihamasisha sana wawekezaji wa ndani pamoja na wawekezaji wa nje kuanzisha viwanda vya vifaa vya michezo kwa sababu tunatambua pamoja na kwamba vifaa vinakuwa ni adimu lakini pia changamoto kubwa imekuwa ni masuala ya kodi. Kwa hiyo hakuna namna nyingine ambayo tunaweza tukafanya kuondokana na tatizo hili, ni lazima sisi kama nchi tuhakikishe kwamba tuna viwanda ambavyo vinahusiana na uchakataji wa hivi vifaa vya michezo. Kwa hiyo, mikakati ipo na sisi kama Wizara tunaisimamia hiyo mikakati na tunamwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, tatizo hili kwa kadri miaka inavyozidi kwenda tunaendelea kulifanyia utatuzi.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili amezungumza namna gani ambavyo Halmashauri ya Kinondoni imeonesha jitihad. Nikiri kwamba ni kweli Halmashauri ya Kiondoni imekuwa ni mfano katika kuweka miundombinu ya michezo na natambua kwamba pia Halmashauri hiyo sasa hivi inamiliki timu ya KCMC, kwa hiyo ni namna gani ambavyo wanaonesha kwamba wana jitihada kubwa ya kukuza sekta hii ya michezo. Kwa hiyo, niseme sisi kama Wizara kwa kupitia TFF tumekuwa tukiunga mkono jitihada kama hizi za wadau kwa kuwapatia vifaa mbalimbali pamoja na nyasi na vifaa vingine na hayo tayari yameshafanyika kwenye baadhi ya maeneo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana pia na Halmashauri ya Kionondoni wapeleke maombi TFF ili waone ni namna gani ambavyo wataweza kusaidia hivyo vifaa ili huo uwanja uweze kukamilika na nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, sisi kama Wizara tutakuwa pamoja naye kuhakikisha kwamba uwanja huo unakamilika, lakini vilevile support ya Serikali kupitia TFF iweze kuonekana. Ahsante sana.

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MAULID S. MTULIA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha Sekta ya Michezo kwa kuandaa Wakufunzi wa Michezo, kujenga viwanja vya kisasa na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya michezo?

Supplementary Question 2

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni kweli siyo Mwanamichezo, lakini nawakilisha wanamichezo. Watanzania wote leo tunamshangilia na kumfurahia Samatta kwa kusajiliwa na hiyo timu ya Uingereza. (Kicheko)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, wanataka kujua tu ni timu gani hiyo. Inaitwaje hiyo? (Kicheko)

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, Aston Villa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, amesajiliwa kwa sababu ya jitihada zake mwenyewe, sasa inatuambia Watanzania kwamba tunaweza kuwa na Samatta wengi kwa kadri inayowezekana kama Serikali ikiwezekeza vya kutosha kwenye michezo. Sasa kwa nini Serikali isianzishe Sports Arena kwenye Majiji Makuu kama ambavyo wanafanya Nchi ya Rwanda ili kuwatoa Samatta wengi?

Name

Dr. Harrison George Mwakyembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Answer

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu maswali vizuri sana ya michezo. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kutokana na juhudi za Serikali pamoja na wananchi wenyewe, tuna wachezaji 22 wanacheza nje ya nchi yetu, wanacheza Kimataifa siyo Samatta peke yake na hii inatokana na uelewa tulioupata Watanzania kwamba vipaji hivi havipatikani ukubwani unaanzia huku chini ndiyo maana Serikali inaingia gharama kila mwaka kuendesha mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA kwa shule za Msingi na shule za Sekondari.

Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kwa kusema, sasa hivi wito wetu wa kushiriki kila mtu kujenga viwanja, miundombinu siyo tu Kinondoni imeitikia hata vilabu binafsi kama Simba Sports Club wamejenga viwanja viwili Dar es salaam vya nyasi bandia pamoja na nyasi za kawaida, viwanja vizuri nimeenda kuvitembelea. Siyo hivyo tu, Mkoa wa Arusha unaongozwa unastahili pongezi, Halmashauri ya Jiji la Arusha sasa hivi imejenga Ngarenaro kiwanja changamani kizuri ambacho kina Netball, Basketball pia Soccer lakini vilevile katika Kata nafikiri ya Sinoni kuna Mtanzania ambaye anaishi Marekani anajenga kiwanja kizuri sana kimefikia asilimia 90. Nitoe wito kwa vijana wetu pia wanaoishi Ulaya, nje ya nchi waige huo mfano, wasishinde tu kwenye mitandao ya kijamii. Ahsante sana.