Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Primary Question

MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:- Maboma mengi ya maabara kwenye Shule za Sekondari za Kata nchini hayajakamilika na hata pale yanapokamilika hakuna vifaa vya maabara na tunahitaji sana wanasayansi kuelekea uchumi wa viwanda:- (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha maabara hizo na lini zitakamilika? (b) Je, ni lini vifaa vitapelekwa katika maabara zilizokamilika?

Supplementary Question 1

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimwa Spika, nakushukuru. Labda tu kabla ya kuuliza maswali yangu ya nyongeza, nikuombe tu univumilie kidogo kwa sababu haya majibu ya Serikali sioni matumaini kabisa.

Mheshimiwa Spika, kwanza tunazungumzia uchumi wa viwanda na tegemeo kubwa lazima tuweze kuzalisha wanasayansi wa kutosha kabisa. Sasa mimi natoa mfano tu wa Mkoa wetu wa Dodoma tulikuwa kwenye vikao vya ALAT hata kwako Mheshimiwa Spika tuko chini ya 20% ya ukamilishaji wa maboma ya maabara. Sasa huu uchumi wa viwanda unakwenda kulishwa na watu kutoka wapi kama tunawapeleka watu wa masomo mengine na siyo wanasayansi?

Mheshimiwa Spika, unapozungumzia shilingi milioni 8 ambazo Halmashauri ya Mji Kondoa tumeidhinisha hizi ni zile fedha ambazo nimezitoa mimi kupitia Mfuko wa Jimbo mwaka jana na tulikwishazitoa. Boma moja la darasa linajengwa kwa shilingi 25 sisi tunazungumzia shilingi milioni nane. Hebu Serikali ione ni namna gani tunakuja na mkakati wa dharura sasa kama ambavyo tumefanya kwenye maboma ya madarasa na kwenye nyumba za walimu ili tuweze kukamilisha hizi maabara nchi nzima. Swali la kwanza hilo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, walau mimi nina maabara moja tu kati ya sekondari nane (8) ambayo imekamilika na yenyewe haina vifaa. Ni lini tutapata angalau hivyo vifaa vya maabara kwenye hata hiyo moja ambayo mpaka sasa imeshakamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba majibu ya Serikali tafadhali.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFlSI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ameuliza maswali mawili, moja anauliza mkakati wa Serikali wa kumalizia maabara ambazo wananchi wameweka nguvu zao lakini jambo la pili anataka kujua ni lini tutapeleka vifaa katika shule yake.

Mheshimiwa Spika, tulisambaza vifaa vya maabara kwenye shule na maabara mbalimbali. Nafikiri baada ya kutoka hapa mbele tuwasiliane tuone ni kwa nini maabara yako moja ambayo imekamilika haikupata vifaa ili tuweze kupeleka vifaa katika shule yako hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini nikupongeze sana kwa swali muhimu, ni kweli kwamba tunahitaji uchumi wa viwanda na tunahitaji zaidi wanafunzi wetu wasome masomo ya sayansi na huwezi kusoma sayansi kama hauna maabara zenye vifaa na wale wataalam wa maabara ili waweze kufanya mazoezi kwa vitendo. Tunampongeza Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine ambao kwa kupitia Mfuko wa Jimbo wamepeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha maabara. Najua wengine wamejenga madarasa, wengine wamenunua madawati na wengine wamejenga nyumba katika maeneo ya jirani ili walimu wetu waweze kupanga kwa bei nafuu sana.

Mheshimiwa Spika, nilichosema hapa ni kwamba Serikali ina mpango, kwenye bajeti hii Waheshimiwa Wabunge wote tumetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maabara. Tulishatoa taarifa kwenye Halmashauri walete taarifa ya maabara ambazo zimekamilika, vifaa vinanunuliwa na vinasambazwa katika maeneo yale. Tunaendelea kutoa wito tupate hizo taarifa ili tuendele kukamilisha zoezi hili.

Mheshimiwa Spika, umesema vizuri hapa kwamba hapa tunazungumzia maabara katika shule za sekondari na katika mpango wetu ule wa kupata fedha zile ambazo zina kizungumkuti huko na wenzetu wameshiriki, katika mpango ule nilisema juzi hapa tunajenga shule mpya za watoto wa kike maalumu 26, tunajenga madarasa na mabweni kwa maana ya mabwalo zaidi ya 300 na tunakamilisha maabara zaidi ya 400. Kwa hiyo, huenda hii fedha ingekuja kwa wakati na ndiyo ulikuwa mpango wa Serikali hii kazi ya kulalamikia maabara hata kama isingeisha ingepungua sana. Tutoe wito Waheshimiwa Wabunge kama nilivyosema juzi hii kazi Serikali ni yetu sote tulishirikiane fedha zikitafutwa tunapeleka fedha Halmashauri, tunapeleka fedha kutoka Mfuko Mkuu lakini pia tunatumia wadau mbalimbali ili tuweze kupata fedha tuweze kukamilisha miundombinu mbalimbali ya elimu.

Mheshimiwa Spika, tushirikiane katika jambo hili na kama ambavyo umeshazungumza katika Bunge hili. Pia sisi kama Wizara tunakwazwa sana na mambo haya kwa sababu tunaweka mipango na Wabunge wameleta maombi mbalimbali pale Wizarani, fedha zimeiva halafu kuna watu wanaweka kitumbua mchanga. Ahsante sana.

Name

Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:- Maboma mengi ya maabara kwenye Shule za Sekondari za Kata nchini hayajakamilika na hata pale yanapokamilika hakuna vifaa vya maabara na tunahitaji sana wanasayansi kuelekea uchumi wa viwanda:- (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha maabara hizo na lini zitakamilika? (b) Je, ni lini vifaa vitapelekwa katika maabara zilizokamilika?

Supplementary Question 2

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Ukiangalia malengo endelevu ya dunia yanaenda kwa vipaumbele. Kipaumbele cha Nne ni elimu bora, sawa Jumuishi/Shirikishi kwa wote. Kipaumbele cha Tisa ni viwanda, ubunifu na miundombinu. Serikali imekuwa ikiwekeza kwa kasi kubwa kwenye miundombinu lakini ili uweze kutekeleza na kusimamia vizuri miundombinu yafaa kuwekeza zaidi ya mara mbili kwenye elimu kabla ya miundombinu. Serikali haioni umuhimu wa kuja na mpango mkakati bila kupepesa macho ili wawekeze kwenye elimu na hasa sayansi ili maabara zetu zikiwa kwenye hali nzuri ikiweko ya Rasesa ambayo Mbunge naijenga kule Vunjo waweze kuwekeza na watoto wetu wawe wabunifu waweze kuendesha karne ya sanyansi na teknolojia na hasa viwanda?

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFlSI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa James Mbatia, Mbunge Vunjo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maoni na mawazo yake mazuri na ya kisayansi. Nimhakikishie kwamba mpango wa Serikali upo mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba tunaondoa changamoto hii. Tunaweka mpango mzuri wa kumalizia maabara zetu, kupata mabweni ya kutosha kwa watoto wa kike lakini kupata walimu wa sayansi hasa masomo ya hesabu, fizikia, kemia na biolojia ili masomo hayo yaweze kufundishwa.

Mheshimiwa Spika, lakini wakati tunatekeleza mkakati wa muda mrefu tunao mpango wa muda mfupi. Kama nilivyosema kwenye bajeti hii tunazo fedha na vyanzo vipo katika maeneo mbalimbali. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kabla ya mwezi wa pili au wa tatu tutakuwa tumepeleka fedha katika majimbo yetu ili kukamilisha miundombinu ya elimu. Mpango wa mwaka huu tumeelekeza Wakurugenzi na nyie Waheshimiwa Wabunge hakikisheni kwenye mpango mnaoanzisha pale kuwe na kipengele hicho cha kuwekeza katika walimu na madarasa lakini pia maabara katika halmshauri zile.

Kwa hiyo, tukishirikiana na Halmashauri zetu sisi Wabunge na wadau mbalimbali wa maendeleo na Serikali Kuu jambo hili linawezekana. Hatuwezi kuwa na viwanda halafu wageni ndiyo waje kufanya kazi hapa kwetu lazima tuwe na viwanda na vijana walioandaliwa vizuri wafanye kazi katika viwanda hivyo ili tuweze kuwekeza katika uchumi wa viwanda na uchumi wa kati.