Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:- Je, kwa sasa Tanzania ina aina ngapi za madini?

Supplementary Question 1

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, anakiri kabisa kwamba madini haya ni muhimu katika kujenga uchumi wa taifa. Mheshimiwa Waziri, ningependa kukuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; tumeshuhudia bei ya tanzanite ikiendelea kushuka kila siku. Ningependa kujua mkakati wa Serikali; mna mkakati gani wa ziada wa kuendelea kulinda thamani ya tanzanite?

Swali la pili; katika aina ya tano ya madini umezungumzia madini ya nishati ambayo ni makaa ya mawe pamoja na gesi. Mkoa wetu wa Rukwa tuna aina ya madini ambayo ni helium, tangu imegundulika ni muda mrefu sasa. Kama ulivyosema dhana ni kujenga uchumi, ningependa kujua na Wanarukwa wafahamu; ni lini madini haya yataanza kuchimbwa ili yawasaidia Wanarukwa na uchumi wa taifa kwa ujumla? (Makofi)

Name

Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Answer

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni lile analoulizia madini ya gesi ya helium yataanza kuchimbwa lini. Naomba nimhakikishie kwamba Serikali tulishatoa leseni ya kuchimba madini ya helium katika Ziwa Rukwa. Tatizo tulilonalo pale ni kwamba katika eneo hilo ambalo tumetoa mashapo ya kuchimba helium ipo pia leseni ya kampuni nyingine ya Heritage ambayo inachimba madini ya gesi ambayo ipo inasimamiwa na Sheria ya Mafuta na Gesi.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali tunachofanya ni ku-harmonize hawa watu wa Heritage pamoja na helium ili waweze kukubaliana tuweze kuanza kuchimba. Hata hivyo, tumeshawapa maelekeo watu wa Helium One waanze kuchimba kwenye eneo ambalo halina mgogoro na watu wa Heritage na mashauriano yanaendelea ndani ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, la pili ni hili alilozungumzia, kuhusu madini ya nishati. Naomba nimhakikishie kwamba Serikali tunaendelea kuwasimamia watu waweze kuchimba haya madini ili yaweze kuongeza uchumi wa nchi yetu.