Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Dalaly Peter Kafumu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igunga
Primary Question
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:- Madini ya Tanzanite yanapatikana nchini Tanzania pekee, juhudi za kufanya madini haya kuchimbwa na Watanzania pekee kwa Kanuni za Madini za mwaka 2004 na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 hazijaweza kuzaa matunda:- (a) Je, kwa nini Tanzania isiyatangaze madini ya Tanzanite kuwa ni Nyara za Taifa itayovunwa na Serikali pekee ili kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa Taifa letu? (b) Je, kwa nini Serikali isiende kujifunza nchini Zimbabwe kuona jinsi ilivyofanikiwa kuyafanya madini ya Almasi kuwa Nyara ya Serikali na hivyo kuleta manufaa makubwa sana kwa nchi hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mwaka 2002, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, kanuni ililitangaza eneo lile kuwa eneo maalum lakini pia iliamua kujengwe ukuta na mwisho tanzanite itangazwe kuwa nyara. Naishukuru sana Serikali kwa kutekeleza hasa ujenzi wa ukuta, Serikali inayoongozwa na jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, wanafanya vizuri sana kuiendeleza sekta hii ya madini.
Mheshimiwa Spika, naomba basi niulize swali dogo la nyongeza; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekubali ushauri wangu, ni lini basi ushauri huu atautekeleza? Ahsante sana.
Name
Doto Mashaka Biteko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukombe
Answer
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, mjiolojia mbobezi hapa nchini wa madini; nataka tu nimtoe wasiwasi kwamba jambo hili ndani ya Serikali tumeanza kulijadili kwa muda mrefu na katika hatua mbalimbali tulizowahi kufikia ni pamoja na mashauriano ya kuona namna gani ili tuweze kuyafanya madini haya ya tanzanite kuwa nyara ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie kwamba tunalichukua kwa uzito wake, lakini ilikuwa lazima tuanze kwa hatua ya kwanza ya udhibiti, na hatua ya kwanza ya udhibiti ilikuwa kujenga ukuta na kuweka mifumo ya usimamizi wa madini ya tanzanite.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo unakumbuka, katika madini ambayo yalikuwa hayajawahi kusimamiwa vizuri hapa nchini ni madini ya tanzanite yaliyopelekea kiasi cha madini ya tanzanite ambayo tulikuwa tunayaona kwenye mfumo rasmi wa Kiserikali ilikuwa ni asilimia tan tu ya madini yaayochimbwa.
Mheshimiwa Spika, sasa nafurahi kusema kwamba hatua ya mwanzo ya kuweka mifumo imeshakamilika, hatua ya pili ilikuwa kujenga masoko ili tuwe na uhakika wa mahali pa kuyauza, hatua ya tatu ni kuweka mitambo au viwanda kwa ajili ya kukata madini ili uongezaji wa thamani uweze kufanyika ndani ya ukuta.
Sasa hatua ya mwisho ni hiyo sasa ya kutangaza haya madini kuwa nyara ya Serikali, hili na lenyewe Serikali inalitafakari, baada ya muda wakati wa mashauriano Mheshimiwa Dkt. Kafumu na yeye tutazingatia kuchukua ushauri wake.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved