Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Amb. Adadi Mohamed Rajabu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Primary Question
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:- Katika Kata ya Mbomole maeneo ya Sakale Wilayani Muheza kuna madini ya dhahabu ambayo wananchi wamekuwa wakichimba bila vibali na hivyo kukamatwa kwa kuharibu chanzo cha maji cha Mto Zigi:- (a) Je, ni lini Serikali itatuma watalaam ili kuweza kujua eneo hilo lina madini gani? (b) Je, Serikali ipo tayari kuweka utaratibu mzuri ambao utahakikisha kuwa wachimbaji hao wanachimba eneo ambalo hawatasumbuliwa?
Supplementary Question 1
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza ninapenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu alifika eneo la Sakale na akazungumza na wananchi wa Sakale, na pili haikuchukua muda mrefu akawatuma hao wataalam mbalimbali ambao walikwenda wakaangalia hiyo sehemu.
Mheshimiwa Spika, tulishakubaliana na Mheshimiwa Waziri kwamba sehemu hiyo hatutaingilia eneo la Bonde la Mto Zigi ili kuepuka chanzo cha maji, na tulikubaliana kwamba tutafute wawekezaji wakubwa ambao wanaweza kuchimba eneo lile.
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu ni, taarifa nzuri ni wawekezaji wameanza kupatikana lakini kuna tatizo la wawekezaji kuruhusiwa kuanza kuchukua sample pale na kuweza kujua kuna madini ya kiasi gani. Je, Wizara iko tayari kurahisisha utaratibu huo ili wawekezaji wale waweze kuangalia kuna madini ya kiasi gani pale Sakale?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ni la ujumla tu la kutaka kujua. kwamba mpaka sasa hivi Wizara ina utaalam gani ambao unaweza kujua mgodi fulani kuna madini ya kiasi gani pale, kama ni dhahabu au almasi; je, utaalam huo tunao au bado hatuna?
Mheshimiwa Spika, ni hayo tu, ahsante sana.
Name
Doto Mashaka Biteko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukombe
Answer
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kwa moyo wa dhati kabisa ninaomba nikiri kwamba Mheshimiwa Balozi Adadi kwa watu wa Muheza na kwenye hilo eneo alilolitaja la uchimbaji, yeye amekuwa champion mkubwa wa kuhakikisha kwamba uchimbaji unaanza kwenye kazi hiyo kwa sababu wananchi wa pale kwa kweli ukienda wanategemea sana hilo eneo ili waweze kuchimba na kujipatia mapato na kubadilisha maisha yao.
Mheshimiwa Spika, changamoto iliyokuepo ni kwamba eneo hilo haliwezi kuchimbwa kwa uchimbaji mdogo kwa maana ya matumizi ya mercury ambayo yanaweza kingie kwenye Mto Zigi na kuathiri chanzo cha maji ambacho kwa kweli katika Bwawa la Mbayani ambalo linapeleka maji kule Tanga Mjini, Korogwe pamoja na Muheza, ukiruhusu hiyo watu wote wale maji yale yataweza kuchafuliwa na mazingira. Uchimbaji ambao unaweza kuruhusiwa pale ni ule tu uchimbaji wa kati ambao unakuwa na EIA ambayo NEMC wataitoa.
Mheshimiwa Spika, sasa kama kuna wataalam ama kuna watu wanaotaka kuchukua sampuli, hakuna mahali popote wanazuia, kwa mujibu wa sheria wanaweza kuchukua sampuli na kupima na kuweza kujua kuna madini kiasi gani. Kwanza ni jambo la faida kwetu kwa sababu wanafanya utafiti kwa niaba ya Serikali na hivyo wanaweza kuchukua wakati wowote. Kama kuna mtu yeyote anawazuia kuchukua sampuli naomba nitoe wito wafuate taratibu zote zilizowekwa wachukue sampuli waweze kwenda kupima na hatimaye wapate taarifa wanazozihitaji.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni je, Wizara tuna utaalam wa kujua kuna kiasi gani cha madini mahali fulani? Naomba nijibu tu kwa kifupi kwamba Serikali inayo huo uwezo kupitia Shirika letu la Serikali la GST, tuna uwezo wa kutambua kuna kiasi gani cha mashapo na kuna kiasi gani cha madini kinachoweza kuchimbwa. Kama kuna eneo ambalo analo, kwa kutumia Shirika letu la STAMICO, nimuombe Mheshimiwa Mbunge awasiliane na STAMICO waweze kujua ni kitu gani kinaweza kufanyika.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved