Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Michael Mkundi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Primary Question

MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:- Je, ni vikundi au wavuvi wangapi katika Kisiwa cha Ukerewe wamepewa elimu na mitaji ili waweze kufanya uvuvi wenye tija?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu la msingi la Mheshimiwa Naibu Waziri limeonesha wavuvi na wadau 520 wamepata elimu hiyo lakini pamoja na kuwapa elimu watu hawa 520 hakuna mfumo rasmi unaoweza kusaidia hii elimu waliyoipata ku-disseminate kuwafikia wadau wengine ambao ni sehemu kubwa ya wakazi wa Jimbo la Ukerewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri mwaka jana alitembelea Jimbo la Buchosa akatumia mfumo mzuri sana kutoa elimu kwa wavuvi wa eneo lile. Swali la kwanza, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuja Ukerewe ili kwa pamoja tushirikiane kuwapa elimu wadau wetu hawa wavuvi waweze kujua hasa nini kinachopaswa kufanyika kwenye eneo la uvuvi kuwaondolea adhabu wanazopata bila kuwa na elimu ya msingi kujua wajibu wao ni upi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, hatua iliyofikiwa na kikundi hiki cha Bugasiga ni nzuri na ilipelekea kupata mkopo wa shilingi milioni 250 na nina kila sababu ya kuipongeza Serikali kuwezesha jambo hili. Changamoto zilizopo ni kwamba mkopo huu unatolewa kwa ushirika unaolazimisha sasa dhamana inayotakiwa iwe ni kwa mtu mmojammoja na matokeo yake sasa mkopo unaonekana kama ni wa mtu mmoja na sio ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali kwa nini isitengeneze mfumo kwamba wadau hawa kupitia ushirika wapewe mikopo lakini sasa wao wenyewe waunde SACCOS ili SACCOS zile zikopeshe mdau mmoja mmoja na wawajibike kwa SACCOS halafu SACCOS ndio iwajibike kwenye ushirika? Nashukuru sana. (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa shukrani kwa Mheshimiwa Mbunge kutupongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kazi nzuri tuliyoifanya katika eneo la Kanda ya Ziwa ya kutoa elimu na akatolea mfano wa Jimbo la Buchosa ambalo hivi sasa tunacho Chama cha Ushirika cha Zilagula Fisheries Cooperative ambacho na chenyewe kimeomba mkopo wa shilingi milioni 300 na kitakwenda kupata kupitia TADB lakini na vyama vingine takribani milioni 50 kila chama shilingi milioni 10. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi la utoaji elimu ni endelevu na sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tupo tayari tutakwenda Ukerewe mara tu baada ya kuahirishwa kwa Bunge hili kwenda kutoa elimu ile kwa wavuvi wa pale Ukerewe ili waweze kunufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili linahusu juu ya mfumo wa mikopo kupitia ushirika na SACCOS. Naomba tulichukue wazo lake hili ni ushauri mzuri ambapo Wizara tutaufanyia kazi. Kwa kuwa tayari tunalo Dawati letu la Sekta Binafsi linalofanya kazi nzuri sana ya kuratibu mikopo hii na kuratibu namna ya kuweza kuwasaidia vyama vya ushirika, nataka nimhakikishie kwamba ushauri huu tunauchukua na tunakwenda kuufanyia kazi kwa maslahi mapana ya wadau wetu wa uvuvi ili waweze kusonga mbele. (Makofi)

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:- Je, ni vikundi au wavuvi wangapi katika Kisiwa cha Ukerewe wamepewa elimu na mitaji ili waweze kufanya uvuvi wenye tija?

Supplementary Question 2

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo kuna wavuvi ni pamoja na Jimbo la Bunda Mjini, wapo wavuvi ambao wanavua kupitia Ziwa Victoria. Hakika vijana wengi wa Jimbo la Bunda Mjini wamehamasika kujiajiri wenyewe kupitia Sekta ya Uvuvi lakini changamoto ni zana za uvuvi nyavu pamoja vitu vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningependa Serikali inijibu ili kuwapa moyo vijana ambao wameamua kujiajiri wenyewe kutokana na uvuvi kupitia Ziwa Victoria, ni lini sasa watawawezesha mitaji ili waweze kuvua kisasa waache ugomvi na DC Bupilipili ambaye anawakamata kila siku?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inayo progamu kama nilivyojibu katika majibu ya msingi ya kuwawezesha wavuvi. Kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, moja ya jambo ambalo tuliligundua ni kwamba wavuvi na hata wafugaji wetu hawakopesheki. Ndiyo maana vijana wengi wanaojihusisha na shughuli hizi wamekosa fursa ya kuweza kupata mikopo na hatimaye kuweza kuboresha shughuli zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kubwa za kukosa mikopo zipo mbili; ya kwanza mabenki yanataka dhamana na pili ni bima kwa maana shughuli za mifugo na uvuvi hazina bima. Nataka niwahakikishie Wabunge wote wa Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzana, Wizara imefanya kazi nzuri na sasa mabenki yametukubalia.

Naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa Benki ya Posta Tanzania imefungua na kuanzisha Akaunti Maalum ya Wavuvi (Wavuvi Account) yenye lengo mahsusi la kuweza kuwasaidia kwa unafuu sana wavuvi wote. Kwa hiyo, nitawaelekeza Benki ya Posta waje pale Bunda Mjini waweze kuwapata vijana na waweze kushirikiana nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la pili la dhamana, tumefanya kazi kubwa ya kuhakikisha tunalishawishi Shrika letu la Bima la Taifa na limekubali mwezi huu wa pili tutasaini nao mkataba maalum utakaowawezesha sasa kuwa na bima ya mifugo na uvuvi. Hii itakuwa ni hatua kubwa sana kuelekea katika kuhakikisha wavuvi na wafugaji wetu wote wanaweza kupata mikopo katika benki kama vile ambavyo wanaweza kupata Watanzania wengine baada ya kuwa na uhakika wa dhamana na bima.

Name

Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Primary Question

MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:- Je, ni vikundi au wavuvi wangapi katika Kisiwa cha Ukerewe wamepewa elimu na mitaji ili waweze kufanya uvuvi wenye tija?

Supplementary Question 3

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Matatizo ya wavuvi wa Ukerewe yanafanana sana na matatizo ya wavuvi wa Kisiwa cha Mafia. Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana mezani kwake kuna barua kutoka kwangu na kwa wavuvi wangu tukiomba ruzuku ya msaada wa zile mashine.

Je, ni lini majibu yake yatatoka?

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Answer

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake hili la nyongeza akiulizia suala la zile mashine za ruzuku, tukitoka hapa Bungeni aje pale ofisini kwa ajili ya utaratibu wa kupata zile mashine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala hili la vijana na wavuvi wetu kuhakikisha wanaheshimika katika mabenki na mahali popote pale, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeandaa Uvuvi Database ambapo ndiyo kilikuwa kipengele kikubwa sana kilichokuwa kinawafanya wavuvi wetu wasiaminike kwenye mabenki kwa sababu ya shughuli zao za kuhamahama na kila mtu mwenye benki anakuwa na mashaka juu ya fedha zake atakapozipeleka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipoanzisha Uvuvi Database sasa hivi benki yotote ile ikitaka kumkopesha mvuvi ambaye yupo Buchosa, Ukerewe, Mafia na maeneo mengine watamuona mpaka na kazi zake anazozifanya. Hii inaenda kuongeza imani kubwa kwa wavuvi wa nchi yetu na ile dharau iliyozoeleka ya kwamba wavuvi hawakopesheki sasa itakuwa mwisho. (Makofi)