Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Primary Question

MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani kwa sasa kutatua kero ya maji kwa uhakikia katika Jimbo la Momba?

Supplementary Question 1

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Serikali kuonyesha baadhi ya miradi ambayo inayofanyika katika Jimbo la Momba lakini bado tatizo la maji ni kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Maji inataka kwamba mwananchi achote maji umbali wa mita 400 na Jimbo la Momba lina zaidi ya vitongoji 400 na kiukweli mpaka sasa hivi tukienda katika level ya vitongoji peke yake vyenye maji haviwezi kufika hata 30. Kwa hiyo, nilichokuwa nataka kabla ya kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu Serikali watupe hapa jibu la uhakika ni lini wananchi wa Momba maji yatatoka? Kwa sababu wananchi wanachohitaji pale ni maji pekee. Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, sisi kama Bunge hapa tuliitaka Serikali iongeze tozo kwenye mafuta kwa lengo moja tu la kupata fedha kwa ajili ya kupeleka kwenye miradi ya maji. Je, ni kwa nini ile tozo ambayo Bunge tuliipendekeza mpaka sasa Serikali haijaitekeleza? Ahsante. (Makofi)

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai na sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji tunafanya jitihada kubwa sana za usiku na mchana katika kuhakikisha tunatatua tatizo hili la maji. Tumebainisha Mikoa 17 na Halmashauri 86 ambazo zimekuwa na changamoto kubwa sana ya maji ikiwemo Jimbo la Momba. Zaidi ya Sh.5,641,000,000 tumezipeleka kwenye Mkoa wa Songwe na katika Jimbo lake zaidi ya shilingi bilioni 1.3 zipo kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa mitano katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Azma ya Mheshimiwa Rais ni kumtua mwanamama ndoo kichwani, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutajipanga kuhakikisha miradi hii kwa wakati ili wananchi wake waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kutoa fedha nyingi sana, moja ya changamoto kubwa sana ya Wizara ya Maji ilikuwa katika suala zima la usimamizi wa miradi ya maji na uendeshaji. Miradi ilikuwa ikitekelezwa kwa gharama kubwa sana zaidi ya mfano wake. Mfano, ukienda katika Jimbo la Nkasi kulikuwa na mradi ambao unatekelezwa estimation yake ni shilingi bilioni 6 lakini Mheshimiwa Makame Mbarawa na timu ya Wizara imepitia na kugundua mradi ule unatakiwa kutelezwa kwa shilingi bilioni 3.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumeona kwamba pamoja na utekelezaji wa miradi lakini kwenye estimation za utekelezaji wa miradi zimekuwa kubwa sana. Sisi kama Wizara ya Maji tumepanga miradi yote kutekelezwa kwa Force Account kwa maana ya kutumia wataalam wetu wa ndani. Kwa hiyo, zile fedha ambazo tutakazopatiwa na Serikali zitatuwezesha kutekeleza miradi kwa wakati na tuta-save gharama kubwa sana. Kwa hiyo, nina imani fedha hizi zitaweza kutusaidia kutekeleza miradi mingi kwa kutumia wataalam wetu wa ndani na kuzuia ubadhirifu unaofanywa na wataalam wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.