Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Yussuf Haji Khamis

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Nungwi

Primary Question

MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS Aliuliza:- Kumekuwa na matukio ya watoto kuokota mabomu wakidhani ni vyuma chakavu na kisha kuwalipukia na kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo. Hivi karibuni watoto watano wamepoteza maisha na zaidi ya watoto 40 kujeruhiwa katika Shule ya Msingi Kihanga iliyopo Ngara Mkoani Kagera. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti na kukomesha tatizo hili?

Supplementary Question 1

MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Waziri anakiri katika masuala yake kwamba elimu ilitolewa baada ya vita vya Kagera, lakini waathirika wakubwa katika kadhia hii ya mabomu ni watoto wadogo hasa wanafunzi wa shule za msingi. Inaonekana kabisa kwamba elimu hawajapatiwa ya kutosha au hata kama inapelekwa haiwafikii. Sasa swali langu lipo hapa; je, Serikali iko tayari kuingiza kipindi maalum katika masomo yao wanafunzi wa shule za msingi ili wapatiwe elimu ya kujikinga na mabomu na athari zake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, umiliki na udhibiti wa silaha za mabomu pamoja na silaha nyingine ni jukumu la vyombo vya ulinzi na usalama. Kwa hiyo, kutapakaa hovyo kwa mabomu kumepelekea wanafunzi wa Shule ya Kihanga, Ngara, Kagera kupoteza maisha na wengine wengi wao kujeruhiwa. Je, Serikali iko tayari kuwalipa fidia wale waliopata janga hili? Ahsante.

Name

Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kwanza kwamba Serikali iwe tayari kuingiza somo maalum katika mitaala ya shule za misingi, hili ni wazo zuri na linazungumzika na sisi tutaendelea kuzungumza na wenzetu wa Wizara zinazohusika na elimu ili kuweza kuona uwezekano wake. Wakati hayo yanaendelea, elimu imekuwa ikitolewa katika maeneo hususan yale maeneo ambayo yanaonekana yana matatizo na lengo ni kuwapa elimu wahusika na wao waweze kupeleka katika shule zinazopatikana katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la kwamba inapotokea kwamba mtu amepata tatizo linalohusiana na mabomu au silaha nyingine mbalimbali basi walipwe fidia, niseme tu kwamba kwa kiwango kikubwa ili kuweza kuondoa tatizo hili, ni muhimu kuhakikisha kwamba elimu inatolewa. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba wahandisi wetu wa medani mara zote wamekuwa tayari kwenda katika maeneo yenye mashaka, yenye matatizo ili kuweza kuondoa mabomu haya ili kuepuka athari badala ya kujikita katika suala la kusubiri watu wapate matatizo halafu fidia zitolewe. Hata hivyo, ikithibitika kwamba aliyepata madhara haya yametokana na mabomu ya kutupwa kwa mkono ambayo hayakuweza kuondolewa kwa wakati, basi kwa kawaida fidia huwa zinatolewa.

Name

Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Primary Question

MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS Aliuliza:- Kumekuwa na matukio ya watoto kuokota mabomu wakidhani ni vyuma chakavu na kisha kuwalipukia na kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo. Hivi karibuni watoto watano wamepoteza maisha na zaidi ya watoto 40 kujeruhiwa katika Shule ya Msingi Kihanga iliyopo Ngara Mkoani Kagera. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti na kukomesha tatizo hili?

Supplementary Question 2

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inapotokea athari ya vifo au majeruhi kwa wananchi waliopata milipuko ya mabomu au kuokota mabomu, Serikali mara nyingi huwa wanatoa fidia kama kule Mbagala na Gongo la Mboto. Mheshimiwa Waziri utakumbuka kwamba kule Tunguu kuna watoto waliokota mabomu na walifariki wawili na wananchi wengine walipata majeruhi. Narudia hili kwa Mheshimiwa kwamba wale watu wataweza kupewa fidia. Ni kwa nini basi hadi leo wale watoto wawili au na majeruhi kule Tunguu ambao walipata athari hii hawajapata fidia? Na ni lini watapata fidia yao?

Name

Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea tatizo hili lililotokea Tunguu, nitamuomba Mheshimiwa Mbunge anipe uhakika wa suala lenyewe kwa maandishi ili liweze kufanyiwa kazi. (Makofi)