Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Anatropia Lwehikila Theonest
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:- Je, Megawati moja ya umeme inazalishwa kwa bei gani na inauzwa kwa bei gani (unit cost)?
Supplementary Question 1
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Wanaozalisha umeme ni TANESCO na wanaopanga bei ya kuuza umeme ni EWURA. Kwa muda mrefu TANESCO imekuwa haipati faida, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ni mwaka 2008 na mwaka 2014 waliweza kuzalisha bila hasara.
Je, Serikali haioni ni wakati muafaka kuwa inatoa ruzuku ya upungufu wa gharama katika uzalishaji wa umeme pale ambapo TANESCO wanakuwa hawapati faida kutokana na mauzo yao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; wanunuzi wa umeme wanaoomba kuunganishiwa umeme wakati mwingine hulazimika kununua nguzo na pale maeneo ambako mpango wa Serikali haujaanza, wamekuwa wakitumia kuanzia 500,000 mpaka milioni kununua nguzo lakini nguzo zinabaki kuwa mali ya TANESCO.
Kwa nini wale wanaojinunulia nguzo na kuunganishwa wasiwe wanapewa units za umeme sambamba na ile gharama waliyotumia kununua nguzo ambazo ni mali ya TANESCO? (Makofi)
Name
Eng. Stella Martin Manyanya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nyasa
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. kimsingi Shirika la Umeme TANESCO ni Shirika la Serikali na kwa kweli kwa mara nyingi sana ingekuwa limeachiwa lijiendeshe lenyewe bila kusaidiwa kabisa na Serikali labda sasa hivi lingekuwa limefungwa. Lakini kwa kutambua kwamba hilo ni shirika pekee ambalo pia linachochea uchumi katika nchi yetu kwa maendeleo ya Watanzania kwa ujumla, Serikali yenyewe imekuwa pia ikitoa fedha kwa ajili ya kulisaidia shirika hili pamoja na misaada mbalimbali ikiwemo ya kuanzisha vituo vya kuzalishia umeme, kurekebisha mifumo kwa mfano kujenga line ya msongo wa kv 400 ambao unatoa Iringa mpaka kwenda Mwanza, na sasa hivi unategemea tena kujengwa mwingine wa kv 400 kutoka Iringa mpaka Mbeya, Tunduma, Sumbawanga, Mpanda, Kigoma ambayo ni 400 na kutoka pale kv 220 kwenda mpaka Nyakanazi.
Mheshimiwa Spika, lakini pia kuanzisha uzalishaji katika maporomoko ya maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya aina mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, katika swali la pili kuhusiana na kwa nini mwananchi anapokuwa amelipishwa nguzo hiyo nguzo inatakiwa iwe ni mali ya TANESCO; sio nguzo tu, hata transfoma, akifungiwa transfoma ambalo amelinunua mwenyewe bado anashauriwa kuwa ni mali ya TANESCO. Kuna faida kubwa sana kwa kufanya hivyo kwa sababu nguzo ikishakuwa imejengwa pale utatumia lakini ikitokea imeoza kama umeshairejesha kuwa ni mali ya TANESCO inakusaidia kwamba hata wewe usiweze tena kununua nguzo, ile kazi ya ukarabati inafanyika na TANESCO.
Mheshimiwa Spika, lakini siyo hivyo tu, pale nguzo inapokuwa imefika maeneo hayo inawezesha pia kumfanya mwananchi mwingine aweze kuunganishiwa ikizingatiwa kwamba hatuwezi kuweka nguzo nyingi katika mtaa mmoja. Ileile line moja inayokuwa imenda inasaidia na hata hivyo hizo bei zinakuwa siyo bei kamili, zinakuwa zimezingatia sana kumfanya mwananchi aweze kununua kwa bei anayoimudu.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved