Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph Michael Mkundi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Primary Question
MHE. JOSEPH M. MKUNDI Aliuliza: - Pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya kusambaza umeme vijijini kupitia Mradi wa REA bado kuna shida kubwa katika maeneo ya vitongoji kwenye vijiji hivyo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa umeme unasogezwa kwenye maeneo ya vitongoji ambavyo havijapata huduma hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, katika vitongoji 514 vilivyoko Jimboni Ukerewe vitongoji 238 bado havina umeme, lakini hata vile vitongoji 276 ambavyo tayari vina umeme, umeme wake unakuwa una matatizo makubwa, umeme unakatika mara kwa mara kwenye Jimbo la Ukerewe na hii inatokana na cable inayosafirisha umeme kutoka Kisorya kwenye Lugezi kuchoka.
Mheshimiwa Spika, nataka kujua sasa Serikali ina mpango gani ili kuweka cable nyingine mpya iliyo sahihi ili kurekebisha hali hiyo na kusababisha wananchi wa Ukerewe kupata umeme wa uhakika?
Lakini swali langu la pili, kupitia mradi huu wa REA Serikali iliingia mkataba na makampuni binafsi kusambaza umeme kwenye maeneo ya visiwa, baadhi ya makampuni yalifanya kazi muda mfupi lakini hayakukamilisha kazi kwenye baadhi ya visiwa kwa mfano Visiwa vya Ghana, Visiwa vya Bulubi; makampuni yalisimika nguzo lakini wananchi hawakuweza kupata umeme. Lakini baadhi ya visiwa makampuni yalitowa umeme kwa mfano Kisiwa cha Ukala, Kisiwa cha Ilugwa lakini umeme ule ukawa unauzwa kwa bei ghali na baada ya Serikali intervene gharama ile ilishuka lakini wananchi wakawa wanapata umeme kwa mgao.
Nini kauli ya Serikali sasa ili iweze kutoa faraja kwa wananchi wa maeneo haya ya Visiwa vya Ukerewe? Ahsante sana.
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, jimbo la ukerewe ni moja wapo majimbo ambayo yako katika miradi ni jimbo linalopata umeme kwa miradi ya TANESCO ya Gridi na miradi ya off grid. Kwa hiyo ni kweli kwamba kuna tatizo la umeme ambalo linafahamika katika maeneo ya Ukerewe na hasa shida ni kama alivyosema kwamba hiyo kebo inayopeleka umeme kule imekuwa ikipata matatizo.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Ukerewe linapata umeme kutoka sub station yetu ya Kibara iliyopo pale Bunda na umeme ukitoka pale unasafirishwa kwa waya za kawaida kuelekea kisolia baada ya Kisorya unaenda kupitia kwenye maji kwenda Igongo na baada ya Igongo unaingia Lugezi ambacho ni kisiwa chenyewe cha Ukerewe. Kutoka Bunda kwenda mpaka Igongo siyo shida tena, lakini kutoka Igongo kwenda mpaka Lugezi kuna mita 700 ambapo ndiyo sasa ile cable inayopitisha umeme inapita majini na imekuwa ikipata shida kwa sababu siyo ile cable ambayo inatakiwa kupita kwenye maji.
Mheshimiwa Spika, tayari Serikali kupitia TANESCO imeshaanda mazingira ya kufanya njia ya muda mfupi na njia ya muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba basi inawekwa sub-marine cable kwa hizo mita 700 kuhakikisha kwamba sasa umeme utakuwa ni wa uhakika kwa Jimbo la Ukerewe.
Mheshimiwa Spika, shida nyingine iliyokuwepo ni kwamba nguzo ambazo zimekuwa zikishikilia umeme kwenye eneo la Igongo nguzo zinazotembea kwa kilometa angalau moja zimekuwa zikijaa zikiingia kwenye maji kwa hiyo zinaharibika kwa hiyo mradi wa muda mfupi tutaweka pale nguzo za zege kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mradi wa umeme unaweza kuwa wa uhakika kwenye jimbo letu la Ukerewe. Lakini njia ya muda mrefu inayotarajiwa kufanyika kuanzia mwezi Januari mwakani itakuwa ndiyo hiyo hiyo ya kuweka marine cable ambayo itaanzia kutoka Jimbo la Bunda pale kwenda mpaka Ukerewe itakuwa ni mradi wa uhakika ambao utafikisha sasa umeme kwenye jimbo letu la Ukerewe bila wasiwasi wowote na tunatarajia labda mwakani ndiyo serikali itajipanga kutekeleza mradi huo ambao utagharimu takribani bilioni 12.
Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili kuhusiana na wale wanaopeleka umeme ambao walikuwa siyo wa TANESCO. Serikali kupitia REA ilipata watu wakandarasi mbalimbali wa kupeleka umeme kwenye maeneo ambayo Gridi ya Taifa haijafika na umeme wa jua tunaita nishati mbadala, nishati jadidifu. Ni kweli kwamba maeneo ya ukerewe na maeneo mengine ya visiwa vilivyopo Muleba na Geita vimekuwa vikipata shida ya bei na shida kubwa ya bei ilisababishwa na wakandarasi waliotengeneza hiyo miradi kuwa na gharama kubwa ya uuzaji wa umeme kuzidi kile kiwango ambacho TANESCO inakielekeza.
Mheshimiwa Spika, TANESCO inauza unit moja kwa shilingi mia moja lakini wenzetu walikuwa wanauza unit moja hadi kufikia shilingi 3,500 na Serikali Mheshimiwa Waziri Mkuu alielekeza mwaka jana kwamba gharama hizo zishuke kuja kwenye gharama ambazo ni za kawaida ili kuepusha kuwa na gharama ya double standard kwenye maeneo yale yale ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, tunavyofahamu ni kwamba maelekezo hayo yalitelekezwa kama alivyosema Mheshimiwa Mkundi lakini yale maeneo mbayo bado maelekezo hayo hajatekelezwa basi tunaomba taarifa hizo zifikishwe ili tuweze kuchukuwa hatua.
Mheshimiwa Spika, lakini pia wazabuni hawa ambao walikuwa wanatoa umeme huo tumekuwa tukizungumza nao na majadiliano yanaendelea na tutahakikisha kwamba wanaendelea kupeleka umeme wa uhakika kwa gharama nafuu na kuwafikia wateja wote muda wote ili adhima ya Serikali ya kufikisha umeme kwa ajili ya maendeleo ya viwanda kuwa salama yaweze kufikiwa.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved