Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. SAASISHA E. MAFUWE Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi aliyotoa Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni ya kuongeza watumishi 403 wa afya?
Supplementary Question 1
MHE. SAASISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, majibu ambayo kimsingi yatapunguza maumivu makubwa waliyopata wananchi wa Hai tarehe mbili kutokana na majibu ya swali lao kuhusu suala la ushirika. Niwaambie wananchi wa Hai watulie Serikali yao inawapenda sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niulize swali la nyongeza la kwanza; kwa kuwa hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na kwa kuwa wananchi wa Hai tarehe 28 walifanya jambo lao kwa asilimia kubwa sana na kuleta utulivu humu Bungeni na huko nje; je, ni lini sasa Serikali itatekeleza kwa kiwango angalau cha asilimia 50 ya ahadi ya Mheshimiwa Rais?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, ni lini Serikali italipa madeni ya watumishi wa afya na Walimu ambao ni wastaafu, deni ambalo mimi mwenyewe nimeshaliwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri la milioni 171 ili watumishi wa afya waendelee kufanya kazi yao kwa uaminifu? Ikizingatiwa miongoni...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa umeshauliza swali.
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saasisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi ya kuajiri watumishi wa afya japo kwa asilimia 50. Bunge lako Tukufu na Wabunge wote humu ni mashuhuda wa jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali katika kujenga Hospitali za Wilaya, kuongeza vituo vya afya na zahanati. Hivyo basi, pale ambapo bajeti itaruhusu, tutaendelea kuajiri watumishi katika Idara ya Afya; na hawa 75 wanaokwenda Hai, ni sawa na asilimia 18.6 ya watumishi wote ambao wameajiriwa hivi sasa. Kwa hiyo, kadri uwezo utakavyoruhusu, tutaendelea kuleta watumishi katika Wilaya ya Hai.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili juu ya madeni ya watumishi, Mheshimiwa Mbunge kwanza amekuwa mstari wa mbele kupigania haki za hawa watumishi na ili jambo amenieleza mimi mwenyewe zaidi ya mara mbili. Tayari tunashughulikia, ukiacha deni ambalo alikuwa analizungumzia la shilingi milioni 171, tayari yalikuja maombi 137 katika Ofisi ya Rais Utumishi yenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 246 ili yaweze kushughulikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa madeni yaliyolipwa ni Sh.50,690,000/= na madeni yenye thamani ya shilingi milioni 148 ambayo ni sawa na watu 88, yamerudishwa kwa mwajiri ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hai kwa sababu yalikuwa na dosari mbalimbali. Pale ambapo Mkurugenzi wa Hai atarekebisha dosari zile na kuzileta katika Ofisi ya Rais Utumishi, basi nasi tutazifanyia uhakiki tuweze kulipa madeni hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna madeni ya watu 27, sawa na shilingi milioni 33 na kitu hivi, tayari yameshafanyiwa uhakiki na yametolewa katika Ofisi ya Rais, Utumishi na sasa yapo Wizara ya Fedha, tayari kwa malipo muda wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. SAASISHA E. MAFUWE Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi aliyotoa Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni ya kuongeza watumishi 403 wa afya?
Supplementary Question 2
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Lushoto ina uhaba mkubwa sana wa watumishi katika sekta ya elimu na afya. Katika sekta ya elimu, msingi peke yake ambapo tuna shule 168, tuna uhaba wa watumishi 1,274. Tuna vituo 63 vya kutoa huduma za afya lakini tuna uhaba wa watumishi 1,218. Ni lini Wizara hii itaiangalia Halmashauri ya Lushoto kwa jicho la huruma na kutuondoa katika kadhia hii ambayo wananchi wanaendelea kupata?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shangazi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuajiri walimu kadri bajeti itakavyoruhusu. Katika bajeti ya mwaka 2021, Serikali ilitenga bajeti ya ajira 9,500 kwa walimu na watumishi katika kada ya afya 10,467. Hivyo basi, pale Serikali itakapoanza kuajiri hawa, tutaangalia pia na Mlalo kule ili aweze kupata watumishi hawa. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved