Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Primary Question
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza:- Umeme wa msongo mkubwa wa KV 400 toka Singida hadi Namanga umepita katika baadhi ya maeneo ya wazi na malisho ya mifugo 6 kwenye Vijiji vya Engikaret, Ranchi, Orbomba, Kimokouwa na Eorendeke; na fedha za fidia ilipendekezwa zitolewe kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ya Vijiji husika pamoja na watu binafsi ambao umeme huo umepita kwenye makazi yao:- Je, ni lini fedha hizo zitatolewa?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Kabla sijauliza maswali yangu, naomba tu niweke wazi kwamba sijaridhishwa na majibu ya Serikali kwa swali langu kwa sababu nilitegemea kwamba nitapewa mchanganuo wa hii bilioni 11.33 kwa kuonesha katika kila kijiji ni watu wangapi wamefidiwa kiasi gani na kiasi gani kimekwenda kwenye maendeleo ya vijiji husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini haiishii hapo Kijiji hiki cha Engikaret mahesabu yake hayapo katika jibu moja kwa moja. Ukiangalia hiyo bilioni 11.33 kwa mchanganuo uliotolewa inaonesha ni shilingi bilioni 1.669 tu ndiyo imefika na hiyo bilioni 9.660 sijaelewa kwamba mahesabu yake yamekwenda wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo swali langu la kwanza la nyongeza ni kuhusu kijiji cha Engikaret. Kwa kuwa, kulikuwa na wananchi 46 ambao walileta malalamiko yao kwamba wako kwenye njia ya umeme na wakaenda wakafanyiwa tathmini na kuna wengine 66 waliletwa hivi karibuni.
Je, watu hawa ambao kwa ujumla wao sasa ni zaidi ya watu 112 watalipwa lini hiyo fidia?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna umeme ambao ulielekezwa Tarafa ya Ketundeine, umeme wa REA ukifanywa na kampuni yetu ya TANESCO. Kasi ya umeme huo ni ndogo sana na tulitegemea mwezi Julai mwaka jana ungewashwa katika vijiji 10 vya awali kwenye Tarafa hiyo yenye vijiji 19. Je, umeme huu wa Ketundeine utakamilishwa lini? Ahsante sana.
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Steven, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji mkubwa ambao ameendelea kuufanya katika eneo lake. Niseme tu kwamba huo mchanganuo aliousema wa item moja moja kwa ajili ya wananchi baada ya hapa nitauagiza utengenezwe na nitaweza kumpatia kwa ajili ya kuona nani amelipwa nini ili aweze kuwasemea wananchi wake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika eneo la malipo nieleze tu kwamba tulipata changamoto kidogo. Katika kijiji cha Engikaret tulivyofanya tathmini mara ya kwanza ilionekana kwamba ni eneo la kijiji lakini wakati pesa imekwenda kulipwa wakaja wananchi wengine takriban 40 na zaidi wakasema wana haki katika eneo hilo na sisi tukawafanyia tathmini kutoka kwenye ile ya kijiji ili wao walipwe. Kabla ya pesa ile haijalipwa wakajitokeza wananchi wengine zaidi ya 50 wakiwa na malalamiko hayo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, yakawepo makubaliano kati ya TANESCO na Ofisi ya Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya kwamba kwa kuwa lile eneo lote lilifanyiwa tathmini likiaminika ni la Serikali basi Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Halmashauri zitathmini ni nani anastahili kulipwa nini katika eneo hilo na pesa ile ambayo tayari ipo katika akaunti ya Halmashauri iweze kutumika kwa ajili ya malipo hayo. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, pesa tayari imeshalipwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri na yeye anaendelea na utaratibu wa kuhakiki ni nani anastahili kulipwa kama mmojawapo wa wale ambao wako katika eneo hilo.
Katika swali la nyongeza la pili, ni kweli kwamba mradi huo wa vijiji 19 umechelewa. Tulikubaliana na mkandarasi ukamilike kabla ya mwezi Juni mwaka huu na siku siyo nyingi Mheshimiwa Waziri wa Nishati atakuja kuzindua mradi huo kabla ya Mwaka huu wa Fedha kuisha.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved