Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MARIAM N. KISANGI) aliuliza:- Wajasiriamali katika Mkoa wa Dar es Salaam hususan Machinga na Mama Lishe wamekuwa wakisumbuliwa sana na Mgambo wa Jiji hali inayowafanya kushindwa kujitafutia riziki ya kila siku:- Je, Serikali inawasaidiaje Wajasiriamali hao wadogo wodogo ambao hujipatia riziki zao kupitia biashara ndogo ndogo?

Supplementary Question 1

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya namna ambavyo Serikali imejipanga katika kuhakikisha wafanyabiashara ndogo ndogo, machinga, mama lishe na wengine wanaofanana na biashara hizo wanatengenezewa mazingira mazuri ya kibiashara; lakini tungependa hasa kufahamu kwa mfano, habari za uwezeshaji wa mitaji inawezekana ikawa ni njia rahisi sana ya kuwa-contain machinga hawa pamoja na maeneo wanayopewa ili waweze kufanya biashara zao kwa uhakika kwa sababu tayari wanakuwa na kipato kizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu matatizo ya haya ya Dar es Salaam yanafanana sana na matatizo yaliopo Jiji la Mwanza, Wilayani Nyamagana, ambako pia kumekuwa na changamoto kubwa sana. Pamoja na maeneo mengi kupangwa, lakini Halmashauri zimefika sehemu zinakuwa zinabeba mzigo mzito kuona namna ya kuwawezesha hawa wafanyabiashara ndogo ndogo. Yako maeneo mengi yamepangwa, lakini uwezo wa wafanyabiashara hawa kwenda kule kutokana na miundombinu ambayo inakuwa siyo rafiki sana, maana Halmashauri inaweza ikatengeneza eneo vizuri, lakini miundombinu mingine ili iweze kufikika sawasawa inahitaji nguvu ya ziada.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali na Wizara inatuhakikishia kwamba iko tayari kushirikiana na Halmashauri hizi kuwatengenezea wafanyabiashara ndogo ndogo, machinga na mama lishe ili waweze kupata kipato na maeneo yao yawe sahihi?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabla sijajibu swali hili, napenda kumpongeza kwanza Mheshimiwa Stanslaus Mabula na Mheshimiwa Angelina Mabula. Siku sita zilizopita, nilikuwa Mkoani Mwanza, lakini jukumu langu kubwa kule lilikuwa ni suala zima la kuwa cheque ya karibu shilingi milioni 900 wajariamali wa Mwanza ambao wamejiunga pamoja kwa ajili ya kuhakikisha kwamba katika makampuni yao walioyaanzisha yalikuwa takribani 24 waweze kufanya kazi vizuri. Mheshimiwa Mabula naomba niwapongeze sana, mmefanya kazi kubwa sana! (Makofi)
MheshimiwaNaibu Spika, sasa katika suala la mitaji, naomba niseme kwamba mitaji hii malengo yetu katika Serikali ya Awamu ya Tano itatoka katika maeneo tofauti. Eneo kubwa kwanza la mtaji katika hivi vikundi vidogo vidogo, tulisema hata katika bajeti yetu ya TAMISEMI kwamba mwaka huu tumeelekeza asilimia tano ya vijana na asilimia tano ya akina mama ambao takriban kuna karibuni shilingi bilioni 56.4. Imani yangu ni nini? Imani yangu ni kwamba, kama Halmashauri zetu zitahakikisha zile own source, ile ten percent ambayo tano kwa akina mama na tano kwa vijana, tukizielekeza vizuri shilingi bilioni 56.4, zitaleta mafanikio makubwa sana katika Halmashuri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili ni eneo moja la mtaji. Sambamba na hilo katika Ofisi ya Waziri Mkuu, kuna suala zima la uwezeshaji. Eneo hili nalo litaweza kufanya kazi kubwa kuwawezesha vijana waweze kuwa na skills za kutosha katika suala zima la uwekezaji katika maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, Serikali imejipanga na juzi tulikuwa na Benki moja inaitwa Covenant Bank, ambayo iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali. Lengo kubwa ni kukuza mitaji kwa watu wa eneo la chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikiri kwamba, sasa tunahakikisha kwamba hii mitaji sasa, wananchi wapate fursa, lakini sambamba na kupata elimu ilimradi waweze kupata mitaji kuweka uchumi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo la pili, kwa suala zima la kuboresha miundombinu. Ni kweli, maeneo mengine miundombinu inakuwa ni changamoto kubwa.
Kwa hili, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wote, lakini nawapongeza wale ambao tayari wameshajenga masoko kuhakikisha kwamba wanawa-accommodate wafanyabiashara mbalimbali. Sambamba na hilo, tubainishe; inawezekana kweli maeneo mengine masoko yapo, lakini hayapitiki vizuri, barabara siyo rafiki na hata maeneo ya mama ntilie hayajakuwa sawa sawa. Basi naomba tuibue mambo haya katika Halmashauri zetu, tushirikiane kwa pamoja, bajeti zetu zinazokuja tuweke kipaumbele jinsi gani tutafanya hawa akina mama ntilie, wauza mitumba na watu wa kada mbalimbali waweze kupata fursa kwa ajili ya uchumi wa nchi yao na maendeleo yao binafsi.

Name

Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MARIAM N. KISANGI) aliuliza:- Wajasiriamali katika Mkoa wa Dar es Salaam hususan Machinga na Mama Lishe wamekuwa wakisumbuliwa sana na Mgambo wa Jiji hali inayowafanya kushindwa kujitafutia riziki ya kila siku:- Je, Serikali inawasaidiaje Wajasiriamali hao wadogo wodogo ambao hujipatia riziki zao kupitia biashara ndogo ndogo?

Supplementary Question 2

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hii Awamu ya Tano, kila siku namsikia Mheshimiwa Rais anazungumza haya mambo, kwamba ukinunua kitu dukani omba risiti; ukienda hotelini, omba risiti, je, Serikali imejipangaje kuhusu hawa wauza mitumba na wanaotembeza mali (machinga) na mama ntilie kwa ajili ya kutoa risiti ili tupate kodi ya Serikali yetu? Serikali imejipangaje hapo?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Keissy, kwa nyakati tofauti amekuwa akihimiza sana suala la ulipaji kodi. Naomba tukiri kwamba hii nchi haitaweza kwenda bila watu kulipa kodi. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, 2015 ametudokeza sehemu moja, mfanyabiashara mmoja anaingiza karibu shilingi milioni saba kila dakika. Kwa hiyo, kuna watu wakubwa wanakwepa kodi na wadogo wakati mwingine kodi hazikusanywi vizuri.
Mheshimiwa Keissy naomba nikuhakikishie, Ofisi ambayo inaongozwa na kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mpango imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba inafanya utaratibu mzuri, kila mtu atalipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize tena; na sababu ni kwamba katika kada zote, kila mtu atawekewa utaratibu mzuri ilimradi kodi tupate shilingi trilioni 29.54 kutimiza matakwa ya bajeti yetu. Naomba tushirikane na Serikali kwamba wale wenye sheli za mafuta waweke mashine za mafuta na kila mtu atumie mashine za EFD katika Halmashauri zote, tutumie elektroniki na kila utaratibu, kwamba Mheshimiwa Dkt. Mpango ametuwekea utaratibu kuona jinsi gani tutafanya tukusanye kodi kila mtu alipe kodi bila kukwepa kodi.

Name

Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MARIAM N. KISANGI) aliuliza:- Wajasiriamali katika Mkoa wa Dar es Salaam hususan Machinga na Mama Lishe wamekuwa wakisumbuliwa sana na Mgambo wa Jiji hali inayowafanya kushindwa kujitafutia riziki ya kila siku:- Je, Serikali inawasaidiaje Wajasiriamali hao wadogo wodogo ambao hujipatia riziki zao kupitia biashara ndogo ndogo?

Supplementary Question 3

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Tatizo la kusumbuliwa akina mama lishe limekuwa kubwa sana katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu. Siyo siri, tunapozungumzia mama lishe, sana tunawagusa akina mama na wale wajasiriamali wadogo wadogo. Wewe, mimi na Waheshimiwa Wabunge wote tutakuwa mashahidi kwamba hawa akina mama ndio wapigakura wa Chama cha Mapinduzi. Ni nini sasa agizo la Serikali kuhakikisha hawa akina mama lishe wanatengewa maeneo maalum ya kufanyia biashara zao katika Halmashauri zote ndai ya nchi yetu?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli akina mama lishe wakati mwingine wanapata changamoto kubwa sana. Kibaya zaidi ni pale utakapoona Mgambo anakwenda kuchukua jungu la mama lishe halafu wanakusanyika pembezoni wanakwenda kula kile chakula cha mama lishe. Hili jambo linakera sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana siku moja nilipokwenda katika Soko lile la Ilala pale nilitoa maelekezo kwamba tuone jinsi ya kuwarasimisha vizuri tuwaweke katika utaratibu mzuri. Hilo ni moja.
Sehemu nyingine hata wakati mwingine kunaweza kuwa na utaratibu mzuri, Halmashauri zimejenga vibanda kwa akina mama lishe, lakini kuna baadhi ya watumishi wasiokuwa waadilifu, wanatumia vile vibanda wanakodisha akina mama lishe kwa pesa kubwa sana. Jambo hili tumelikemea pale Ilala na sehemu mbalimbali, lakini suala la upangaji wa haya maeneo ni kama nilivyosema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba ndugu zangu, Waheshimiwa Wabunge, tushirikiane na Halmashauri zetu, tutenge haya maeneo, tuyaweke vizuri ilimradi kwanza wale akina mama waliokuwa wanafanya kazi zao katika maeneo ya jua; waliokuwa wanafanya kazi zao katika maeneo yasiyo rafiki; bajeti zile zikifika katika mwaka huu wa fedha tutakaokuja nao, katika Ofisi ya Rais TAMISEMI ambao ndiyo jukumu letu kubwa kuzisaidia Halmashauri, hatutasita kuipa mipango ili kipaumbele ilimradi hawa akina mama waweze kupata fursa ya kufanya kazi zao katika mazingira rafiki; kwa sababu hata katika suala zima la afya itasaidia kupambana na magonjwa ya kipindupindu.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Sikudhani, naomba nikwambie kwamba nitashirikiana na wewe na ninajua kwamba Tunduru ndiko unakotoka, kule bainisheni hilo, tutaweka kipaumbele ilimradi wananchi waweze kupata fursa na akina mama wapate fursa nzuri za kiuchumi.

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MARIAM N. KISANGI) aliuliza:- Wajasiriamali katika Mkoa wa Dar es Salaam hususan Machinga na Mama Lishe wamekuwa wakisumbuliwa sana na Mgambo wa Jiji hali inayowafanya kushindwa kujitafutia riziki ya kila siku:- Je, Serikali inawasaidiaje Wajasiriamali hao wadogo wodogo ambao hujipatia riziki zao kupitia biashara ndogo ndogo?

Supplementary Question 4

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na jitihada nzuri za Mheshimiwa Rais wetu; na pia pamoja na harakati kubwa ya kuwajengea Watanzania nia njema ya kulipa kodi; kwa kuwa Mheshimiwa Rais wakati wa Uchaguzi na katika Kampeni zake aliahidi kuondolewa kwa tozo ndogo ndogo kutokana na wafanyabiashara wadogo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni kuwa ina kila sababu ya kutazama upya Ilani ya Chama cha Mapinduzi na makundi gani yanasamehewa katika hizo tozo ndogo ndogo?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, katika vipindi tofauti, Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais na timu zote tulipokuwa tukinadi ilani na Mheshimiwa Rais aliahidi kundoa hizi tozo ndogo ndogo ambazo zimekuwa kero kwa wananchi; kwamba mboga mboga, nyanya nini imekuwa ni kero kubwa zaidi. Kwa sababu kodi hizi zinatozwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa Sura Na. 290, ndiyo maana tumefanya maelekezo sasa; kuna mchakato unakwenda kwa ajili ya kurekebisha sheria zetu tuone ni jinsi gani sasa tutakusanya katika kodi zile kama crop cess na maeneo mengine lakini kuondoa usumbufu kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili lipo katika mchakato na wadau mbalimbali ndiyo wanaweka maoni yao sawasawa na mwisho wa siku sheria hiyo itakuja katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; tuipitishe sisi sote kwa pamoja, tufanye amendments, tushauri, turekebishe, mwisho wa siku ni kwamba mwananchi wa kawaida atakuwa ameguswa na matamko ya Mheshimiwa Rais alipokuwa akinadi na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kama tulivyoelekeza.