Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Hamida Mohamedi Abdallah
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Lindi Mjini
Primary Question
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kusaidia ujenzi wa Chuo Kikuu cha Uvuvi na Usafiri Baharini Lindi?
Supplementary Question 1
MHE. HAMIDA M. ABDHALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu hayo yenye matumaini lakini pia nishukuru Serikali kwa kutenga fedha 5.8 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kampasi ya Lindi. Pia, nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ziara ambayo ameifanya Lindi wiki mbili zilizopita kwa kuja kukagua maeneo haya ambayo yatajengwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kampasi ya Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
(i) Kwa kuwa Kampasi hii ambayo itajengwa ya Lindi itakuwa mahususi kwa ajili ya kozi ya ufugaji wa nyuki, kilimo, uchumi na biashara, sayansi na teknolojia. Kwa nini Serikali isipanue kwa kuongeza kozi ya uvuvi pamoja na kilimo cha mwani?
(ii) Ningependa sasa kujua kwa sababu kanda nzima ya kusini tuna uhitaji mkubwa wa chuo hiki cha usafiri na usafirishaji baharini, ni lini sasa Serikali itafanya utafiti kuhakikisha kwamba tunapata ujenzi wa chuo hiki cha usafiri na usafirishaji kwa ajili ya kuongeza ajira kwa vijana lakini kuendelea kukuza uchumi na kuwekeza wataalam kama rasilimali watu katika nchi yetu ili waendelee kukuza uchumi kupitia bahari yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa karibu wa suala hili. Amekuwa akifika Ofisini kwetu mara kwa mara na alikuwa akiliulizia mara kwa mara lakini sasa mwarobaini au majawabu ya suala lake hili linakwenda kufikia ukingoni. Kwa hiyo, nikushukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji huo wa karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama nilivyojibu kwenye swali la msingi kwamba Serikali inakwenda kujenga Kampasi hii ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Mkoa huo wa Lindi na tutaanza na kozi hizo na tathmini tutafanya iwapo kama tutaona uhitaji wa kuanzia hizi kozi za uvuvi pamoja na Kilimo cha Mwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Mbunge nikutoe wasi wasi baada ya kufanya market survey na need assessment na kujiridhisha kozi hizo zitakapoanzishwa zitapata wanafunzi basi tutakwenda kuzianzisha kozi hizo kwa kadri ya mahitaji yatakavyookuwa yanaruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili kuhusiana na uanzishwaji wa chuo cha usafiri, nimtoe wasi wasi Mheshimiwa Mbunge kwa vile tunaenda kuanza ujenzi wa chuo hiki katika kampasi hii. Ni utaratibu wa vyuo vyote duniani, tutafanya tathmini ya kuanzisha kwanza kozi za usafirishaji katika chuo hiki au katika Kampasi hii. Badaaye katika upanuzi iwapo kama tutaona uhitaji tunaweza sasa kwenda kuanza majengo au chuo kingine katika maeneo ambayo yatakuwa yanapatikana. Ndiyo utaratatibu wa vyuo vyote duniani hata uanzishaji wa Chuo Kikuu cha Muhimbili ulianzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Ardhi kilianzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hata hiki baada ya kuanzisha na kuona kwamba uhitaji unazidi kupanuka tutaweza kufika katika maeneo hayo Mheshimiwa Mbunge anapendekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Name
Dr. Christine Gabriel Ishengoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kusaidia ujenzi wa Chuo Kikuu cha Uvuvi na Usafiri Baharini Lindi?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi kwa kuuliza swali. Ningelipenda kujua Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere kinachojengwa Butiama ni lini kitaanza kufanya kazi? Ahsante sana.
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Ishengoma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna Kampasi ya Mwalimu Nyerere kule Butiama na ilianzishwa toka mwaka 2014 lakini bado ilikuwa haijanza kufanya kazi, lakini naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge tulifanya ziara na Kamati yako ya Bunge hili mwezi uliopita na tulikwenda pale kwa ajili ya kufanya tathmini na naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, chuo kile kitaanza kufanya udahili katika mwaka huu ili kuweza kuanza kutoa mafunzo katika eneo lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved