Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Busanda

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo la maji katika Jimbo la Busanda katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita?

Supplementary Question 1

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kupeleka hizo fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi. Hata hivyo, wananchi wa Busanda wangependa kujua kwamba ni lini sasa miradi hii itakamilika, maana imekuwa ni miradi ya muda mrefu sana na utekelezaji wa miradi hii ya Benki ya Dunia imekuwa ni ya muda mrefu sana?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa, Jimbo la Busanda linagusa Ziwa Viktoria katika maeneo ya Bukondo na sehemu zingine, ningependa kujua sasa mkakati wa Serikali, ni lini mtahakikisha wananchi wanapata maji ya uhakika kwa kuvuta maji kutoka Ziwa Viktoria?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwa suala la lini naomba nizungumze wazi, bahati nzuri tumeshapeleka fedha nilivyozungumza pale awali, shilingi bilioni 1.144. na hili naomba nimuagize Mkurugenzi wa Halmashauri husika kuhakikisha katika Mwaka huu wa Fedha, kwa sababu fedha zimeshafika hakuna sababu ya wananchi kuendelea kupata shida.
Hili Mheshimiwa Mbunge naomba nikwambie, nadhani tulikuwa pamoja katika kuzindua mradi mkubwa wa maji pale Geita. Katika hili nasema kwamba, tutarudi tena kule Geita kuangalia tatizo hili la maji, kama pesa zimefika nitashangaa sana kuwaona Wataalam wetu wanashindwa kuzitumia fedha hizi vizuri ili wananchi wapate huduma ya maji.
Mheshimiwa Spika, lakini ajenda ya pili, ni kwa nini sasa tusitumie suala la Ziwa Viktoria, nadhani siku ile ya Mkutano Mkubwa tulisema wazi kwamba wale wananchi wote wanaopakana na Ziwa Victoria, Serikali katika awamu ya pili itaangalia ni jinsi gani ya kufanya badala ya wakati mwingine kuchimba bore hole, twende sasa kutumia hii rasilimali adimu tuliyokuwanayo ya Maziwa yetu.
Mheshimiwa Lolesia nikwambie kwamba, Serikali katika huu mpango wa maji wa awamu ya pili ambao ulianza Januari iliyopita, tunajipanga kuhakikisha kuwa tutafanya matumizi mazuri ya Ziwa Victoria, siyo Busanda peke yake bali vijiji vyote na maeneo yote yanayozunguka Ziwa Viktoria, wakiwepo ndugu zangu wa Magu ambao mwezi uliopita nilikuwa kule.

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo la maji katika Jimbo la Busanda katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita?

Supplementary Question 2

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la maji ni tatizo kubwa tuseme nchi nzima, lakini hata Karagwe tuna shida sana ya maji. Wakati wana-Karagwe wanasubiri mradi wa Rwakajunju, Serikali ina miradi ya Benki ya Dunia, lakini kote Jimboni hii miradi haijakamilika. Napenda kuiomba Serikali ieleze wananchi wa Karagwe hii miradi itakamilika lini?
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana.
Mheshimiwa Spika, kuhusu miradi ya Benki ya Dunia, tulikuwa na hiyo awamu ya kwanza ya program ambayo imekwisha Disemba tarehe 30. Sasa tunaingia awamu ya pili ya program ya miaka mitano katika kutekeleza vijiji vile ambavyo havikupata awamu ya kwanza na ile miradi ambayo iko inaendelea. Sasa hivi Serikali imeshapata fedha za kuweza kusukuma miradi ya kwanza ile iliyokuwa imeanza ili iweze kukamilika.
Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, azma ya Serikali ni kuhakikisha vijiji vyote vilivyokuwa ndani ya program tunakamilisha ili wananchi wetu waweze kupata maji.