Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Prof. Patrick Alois Ndakidemi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Primary Question
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI K. n. y. MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuingia kwenye biashara ya Gesi Joto (Carbon Trading)?
Supplementary Question 1
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ninamshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nina swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa, biashara hii huwa inahusisha upandaji na utunzaji wa miti. Je, Serikali haioni umuhimu wa kusukuma hii biashara iende katika maeneo ya Kilimanjaro inayopakana na Mlima Kilimanjaro ili kwanza tutunze ule msitu ili Mlima usiharibike na wananchi wa Kilimanjaro wajipatie kipato?
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Ndakidemi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri na niseme kwamba ipo haja ya mradi huu kwenda Kilimanjaro kwa lengo na madhumuni ya kuhifadhi na kutunza mazingira.
Mheshimiwa Spika, pia kuna haja ya mradi huu kupelekwa Kilimanjaro na tutakwenda kuhakikisha tunapeleka ili lengo na madhumuni wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na vijiji vilivyomo ndani ya Mkoa huo waweze kunufaika, kwa sababu mradi huu si kwamba tu unanufaisha Serikali Kuu lakini hata vijiji vidogo vidogo vinanufaika kupitia mradi huu, kwa sababu kuna asilimia maalum huwa inapangwa kwenye mradi huu.
Mheshimiwa Spika, tayari tumesha-practice katika Mkoa wa Katavi, Manyara na Mikoa mingine. Tumeona tayari zipo shule, yapo maji safi, zipo zahanati zilizojengwa kutokana na asilimia ya mradi huu. Ninakushukuru. (Makofi)
Name
Justin Lazaro Nyamoga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Primary Question
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI K. n. y. MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuingia kwenye biashara ya Gesi Joto (Carbon Trading)?
Supplementary Question 2
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kilolo yupo mwekezaji anaitwa Udzungwa Corridor na tayari anapanda mashamba makubwa ya miti kwa ajili ya biashara hiyo. Kwenye vivjiji vinavyozunguka kuna misitu mingi ya asili inayofanana na hiyo hiyo inayopandwa.
Je, Serikali sasa ina mpango gani wa kuhakikisha ile misitu ambayo wanavijiji wameitunza na yenyewe inaingia kwenye huo mfumo wa biashara badala ya kutegemea tu ile ambayo Mwekezaji anawekeza na anapanda miti ile ile? (Makofi)
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lazaro Nyamonga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza katika kitu ambacho tunakithamini sana ni upandaji wa miti. Pili tunashughulika na suala zima la kuishughulikia miti. Kwa hiyo, kikubwa nimwambie misitu yote ya asili kama ambavyo nimeeleza katika jibu la msingi kwamba sasa hivi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, tumeshaandaa muongozo wa usimamizi wa misitu yote ili lengo na madhumuni tuingize kwenye mpango huo pia tuweze kunufaisha vijiji vilivyozunguka na pia tunufaishe Serikali, pia tutunze na tuhifadhi mazingira. Ninakushukuru. (Makofi)
Name
Asya Mwadini Mohammed
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI K. n. y. MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuingia kwenye biashara ya Gesi Joto (Carbon Trading)?
Supplementary Question 3
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kama tunavyotambua huu mradi wa uvunaji wa hewa ya ukaa ni muhimu sana kwa Taifa letu, inasaidia kupunguza masuala mengi ambayo yanasababishwa na uchafuzi wa kimazingira.
Mheshimiwa Spika, swali langu, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia akinamama ambao wamejitolea kwa makusudi kupanda miti ya mikoko Zanzibar katika Vijiji vya Bwimbwini, Bweleo na maeneo mengine na hawa wanawake wanapata changamoto mbalimbali kuhusu kupata miti na mambo mengine ili ile miti kuweza kustawi vizuri. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia akinamama hawa? (Makofi)
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, asante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asya, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Asya amekuwa mmoja wa miongoni mwa vinara ambao wanapambana na suala zima la uhifadhi wa mazingira katika Mkoa wa Kaskazini. Kikubwa tuna mikakati mingi ya kuhakikisha kwamba tunawasaidia akinamama kwa sababu tumegundua kwamba ni moja ya miongoni mwa vinara wazuri wa uhifadhi wa mazingira na kupambana dhidi ya mabadiliko ya tabia ya nchi.
Mheshimiwa Spika, la kwanza, kuwapa elimu kwa sababu tumegundua kwamba akinamama wengi wana juhudi, wana jitihada na wana hamu ya kuhifadhi mazingira, lakini tumegundua utaalam kidogo umepungua, kwa hiyo tunawapa taaluma.
Mheshimiwa Spika, la pili, tumefikiria pia kuona namna ya kuwasaidia kuweza kupata mitaji ili lengo na madhumuni yaweze kufanya hizo kazi zao za uhifadhi wa mazingira vizuri. Nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved