Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Primary Question

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: - Je, Serikali inatumia vigezo gani kuanzisha vituo vya polisi katika maeneo ambayo idadi ya watu na vitendo vya uhalifu vinaongezeka?

Supplementary Question 1

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Donge wanatembea masafa marefu kufuata huduma za kipolisi katika Vituo vya Polisi vya Mkokotoni na Kituo cha Polisi cha Mahonda na kwa kuwa uhalifu na halikadhalika idadi ya watu wameongezeka katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Donge. Je, Serikali haioni haja ya kufanya kazi na wananchi wa Jimbo la Donge kuweza kujenga kituo katika maeneo hayo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Kituo cha Polisi cha Mahonda ni kituo kikongwe toka kipindi cha ukoloni na kituo hiki hakijafanyiwa ukarabati mkubwa kwa kipindi kirefu. Je, Serikali ina mpango gani wa kukifanyia marekebisho makubwa Kituo cha Polisi cha Mahonda pamoja na nyumba za wafanyakazi ili kuweza kukidhi kupambana na masuala ya uhalifu ambayo yanaongezeka siku hadi siku? Ahsante.

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Soud, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu umuhimu wa kujenga Kituo cha Polisi eneo la Donge ambalo ametaja vigezo vitatu vya masafa marefu lakini kuwepo kwa uhalifu, kujenga kituo pale tutawasiliana na Kamisheni ya Polisi Zanzibar wafanye utafiti kuona umuhimu wa kujenga pale ili iweze kuingizwa kwenye bajeti hatimaye ujenzi uweze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la kuchakaa kwa Kituo cha Polisi Mahonda, namwomba Mheshimiwa Mbunge, tutaituma Polisi Kamisheni Zanzibar kwa kauli yangu niombe Polisi Zanzibar wafanye uthamini wa Kituo cha Polisi Mahonda kwa madhumuni ya kubaini mahitaji ili tuweze kuingiza kwenye mpango wa ukarabati. Nashukuru.

Name

Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: - Je, Serikali inatumia vigezo gani kuanzisha vituo vya polisi katika maeneo ambayo idadi ya watu na vitendo vya uhalifu vinaongezeka?

Supplementary Question 2

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kata ya Soya, Wilaya ya Chemba ni kati ya Kata ambayo inahudumia wafanyabiashara wa mazao pamoja na wafanyabiashara wa mifugo, lakini Kata hii haina kituo cha polisi pamoja na kwamba kutokuwepo kwa kituo cha polisi michakato aliyoisema Naibu Waziri hapo tulishaikamilisha. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka kituo cha afya, samahani, Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Soya ili kukidhi mahitaji na matakwa ya usalama wa Jeshi la Polisi ya kulinda raia na mali zao? Ahsante.

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru maana mwanzoni afya ilinichanganya kidogo. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti Majala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ikiwa kuna mahitaji makubwa ya kujenga Kituo cha Polisi Kata ya Soya, nishauri mamlaka za utawala, kwa maana ya Serikali ya Mtaa Chemba lakini na uongozi wa Wilaya kupitia Kamati yao ya Usalama wajenge hoja hii kama nilivyoeleza, wanyambue mahitaji yao ili wawasilishe kwa IGP, then taratibu ya kuingiza kituo hiki katika mpango wa ujenzi iweze kufikiriwa. Hata hivyo, kama tulivyokwishasema kwenye majibu ya maswali yaliyotangulia, tunahamasisha ushiriki wa Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na wananchi waanze ujenzi ili Serikali isaidie kukamilisha vituo hivi wakiwa na haja ya kuwa na kituo cha polisi. Ahsante.