Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Lucy John Sabu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. LUCY J. SABU aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito?
Supplementary Question 1
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada zinazochukuliwa na Serikali za kupunguza vifo vya wajawazito, lakini kasi ya upunguaji hairidhishi: Je, Serikali imefanya tathmini ya sababu zake?
Swali la pili; kwa kuwa vifo vingi vya wajawazito vinatokana na uzazi pingamizi na majengo mengi yaliyojengwa hususan majengo ya upasuaji hayana wataalamu na vifaa tiba: Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya jambo hilo? Ahsante. (Makofi)
Name
Ummy Ally Mwalimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Answer
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Lucy Sabu kwa suala hili kubwa na nyeti ambalo lote linatugusa wanawake, akina baba na wanaume. Kwa suala la vifo vitokanavyo na uzazi ni kipaumbele cha Serikali kuhakikisha tunavipunguza kadiri inavyowezekana. Sababu za vifo hivi tunazifahamu Mheshimiwa Lucy, ni pamoja na uchungu pingamizi, kutokwa na damu kabla, wakati na baada ya kujifungua. Pia kuna suala la kifafa cha mimba na kuna maambukizi pia ya bakteria.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Lucy pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inayo mikakati mingine ya ziada ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Kuanzia Julai tutatekeleza mradi mkubwa chini ya ufadhili wa World Bank wa Shilingi bilioni 460 ambazo tunazielekeza kwenye huduma za akina mama wajawazito na watoto wachanga.
Mheshimiwa Spika, tutajenga vyumba vya wanawake wajawazito mahututi katika hospitali za wilaya, tutawajengea uwezo watumishi wa afya ili waweze kutoa huduma bora za uzazi wakati wa kujifungua, tutaweka vifaa tiba pamoja na dawa za kuzuia vifo vya akina mama wajawazito ikiwemo dawa ya oxytocin pamoja na dawa ya kuzuia kifafa cha mimba Magnesium Sulphate.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba taarifa rasmi kuhusu vifo vitokavyo na uzazi tutazipata mwezi Oktoba, 2022 baada ya Tanzania National Bureau of Statistic kukamilisha taarifa au utafiti kuhusu hali ya afya na demografia nchini Tanzania. Ndiyo tutaona vifo vinapungua kwa kasi ya aina gani. (Makofi)
Name
Lucy Thomas Mayenga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. LUCY J. SABU aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito?
Supplementary Question 2
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Wizara hii kwa Mheshimiwa Ummy ameitendea haki sana kwa kufanya kazi kubwa sana; na kwa kuwa akina mama wengi wale ambao wanajifungua kwa operation wamekuwa wakilalamika kuhusu maumivu makubwa sana kutokana na zile sindano ambazo wamekuwa wakichomwa mgongoni; na kwa kuwa kuna pesa hizi Shilingi bilioni 460 za World Bank; na kwa kuwa Mheshimiwa Ummy nakuamini una wataalamu na watafiti wa kutosha: -
Je, kwa nini Serikali isifanye utafiti na kujua ni nini hasa kinachosababisha akina mama hawa wapate maumivu ambayo almost yatasababisha ulemavu mara baada ya kujifungua hapa Tanzania? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Ummy Ally Mwalimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Answer
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Lucy Mayenga, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Shinyanga kwa swali lake lakini kwa jinsi anavyowapambania wanawake wa Mkoa wa Shinyanga ikiwemo akina mama wajawazito.
Mheshimiwa Spika, nalipokea swali la Mheshimiwa Lucy Mayenga, ndiyo maana nimesema, Rais Samia ameruhusu mradi huu wa investing in people na focus yake ni afya ya uzazi, mama na mtoto. Fedha zote hizi tutazipeleka katika kuboresha huduma za uzazi. Kwa hiyo, hiyo sindano ambayo wanachomwa akina mama wajawazito ni dawa ya usingizi ili waweze kufanyiwa upasuaji. Tutafanya tathmini kama alivyoshauri.
Mheshimiwa Spika, pia nataka kuwaahidi, tunakwenda kuhakikisha tunatumia huduma za ubingwa za uzazi katika mradi huu ambao tunautekeleza. Vile vile tutajenga hospitali ya mama na mtoto katika Mkoa wa Dodoma ya kwanza ya Kitaifa ili kujenga uwezo wa afya ya uzazi, mama na mtoto katika nchi ya Tanzania. Kwa hiyo, suala hili tunalibeba, tutalifanyia kazi. (Makofi))
Name
Catherine Valentine Magige
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. LUCY J. SABU aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito?
Supplementary Question 3
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, Serikali ilichangia ujenzi wa vituo viwili vya afya Wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha; Kituo cha Engarinaibo na kituo kingine kilichopo mpakani mwa Namanga na Kimokoa, lakini hadi sasa vituo hivi havijakamilika: -
Je, ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha vituo hivi vimekamilika?(Makofi)
Name
Ummy Ally Mwalimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Answer
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Catherine Magige, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha kwa swali lake naye tunatambua jitihada zake anazombana katika kutatua changamoto za wanawake wa Mkoa wa Arusha ikiwemo kuimarisha huduma za mama na mtoto.
Mheshimiwa Spika, suala la vituo vya afya ambavyo havijakamilika, Wizara ya Afya inashirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhakikisha kwamba tunakamilisha ujenzi wa vituo vyote vya afya vilivyojengwa, pia Waheshimiwa Wabunge pamoja na kuviwekea vifaa na vifaa tiba.
Nimeshamuelekeza Katibu Mkuu wangu, anakutana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tufanye tathmini ya vituo vya afya vyote ambavyo vimejengwa, havijakamilika na ambavyo havina vifaa.
Ninawaahidi Waheshimiwa Wabunge fedha hizi ambazo ninazitaja zinakwenda kujikita katika kuweka au kuboresha huduma katika ngazi ya msingi. Kwa sababu asilimia 80 ya wanawake wanajifungulia katika zahanati na vituo vya afya. Kwa hiyo, fedha tutazielekeza nyingi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kukamilisha miundombinu.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved