Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Justin Lazaro Nyamoga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Primary Question
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kufuta Hati ya Umiliki wa Shamba la Mwekezaji katika Kijiji cha Mawalla - Kilolo ambalo limetelekezwa?
Supplementary Question 1
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza: Serikali haioni haja ya kufanya tathmini ya mashamba yote yaliyotelekezwa na kupata orodha yake ili taratibu za kubatilisha ziweze kufanyika katika Wilaya ya Kilolo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, hili shamba limetelekezwa tangu mwaka 1980, lakini hadi sasa halijaweza kubatilishwa: Je, Serikali haioni umuhimu wa kulibatilisha kwa haraka ili liweze kukabidhiwa kwa Halmashauri na kupangiwa matumizi mengine ili wananchi waweze kunufaika? (Makofi)
Name
Geophrey Mizengo Pinda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mashamba ambayo yametelekezwa kwa muda mrefu ni mamlaka za Halmashauri kubaini hayo maeneo na kuyaanzia michakato ya kuomba yabatilishwe. Hivyo, nitoe wito kwenye Halmashauri zote hapa nchini, kupitia maeneo ambayo yamesahauliwa na wale ambao walimilikishwa huko nyuma ili sasa hii michakato ya haraka iweze kufanyika na kubadili yale matumizi ya maeneo kupitia hizi mamlaka za juu.
Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la pili, kwa kuwa jambo hili lilichukua muda mrefu, kama nilivyosema mwanzo, inawezekana Halmashauri ilikuwa haijabainisha na kuanza ile michakato, lakini kwa sasa kwa hatua tulipofikia, hili jambo linakwenda kukamilika kwa sababu mwenye maamuzi ya mwisho katika ubatilishaji wa maeneo haya ya ardhi ni Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, tutakapomfikishia, tunaamini wazi kwamba atalitolea maamuzi ya haraka kadri inavyowezekana, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved