Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaajiri watumishi wa kada ya ulinzi, upishi na makatibu muhtasi katika shule za sekondari za kata nchini?

Supplementary Question 1

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Samahani sana, naona hata majibu yaliyotolewa hayana uhalisia kabisa. Nafasi tano kwa wapishi nchi nzima na nafasi 200 za makatibu muhtasi kwa ajili ya shule ya sekondari. Katika maelezo yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema pia eneo hili la ajira kwa halmashauri zimepewa nafasi. Hakuna Halmashauri hata moja nchini inaajiri kada hizo.

Mheshimiwa Spika, maswali yangu madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa sasa wazazi wengi nchini wamebeba mzigo mkubwa wa kulipa michango kupitia watumishi hawa ambao wanalipwa kwa michango ya wananchi; na kwa kuwa katika shule zetu familia moja inaweza kuwa na watoto wawili, watatu mpaka wanne, Serikali haioni kuwa ni wakati muhimu na muafaka wa kuweza kuongeza ikama ya ajira hii kwa ajili ya watumishi hawa ili kupunguza mzigo kwa wazazi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika kibali cha ajira kilichotolewa juzi Serikali haikutoa kipaumbele kwa ajili ya Walimu wa kada ya kilimo…

SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, je, ni kwa nini Serikali haiweki kipaumbele kutoa kibali kwa Walimu wa mchepuo wa kilimo ili vijana wetu waweze kupata stadi za klimo kutoka shule za sekondari nchini?

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba takwimu tulizotoa ni takwimu sahihi na usahihi wake unakuja kutokana na ukweli kwamba, Mheshimiwa Mbunge ajira hizi zinatokea kwenye halmashauri zetu. Halmashauri ndizo zinazoomba na sisi kama Ofisi ya Rais, Utumishi, tunapokwenda kuomba Kibali tunaomba kwa ikama iliyoombwa tukiangalia na Bajeti ambayo imepitishwa na Bunge lako. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwanza apate kufahamu kwamba kilichoelezwa hapa ni kutokana na taarifa zilizoombwa kutoka katika maeneo yetu ya halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, pia pamoja na hilo tunakubaliana kiukweli kwamba hitajio la kuongeza ikama kwa ajili ya ajira hizi ambazo zimeelezwa ni jambo la msingi na sisi kama Serikali tumelisikia. Pia nimwombe tena Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako, tunapokwenda kutaja vipaumbele vya maeneo yetu ya kiutawala kwa maana ya halmashauri, basi tuangalie kwamba hii ni sehemu moja wapo ya eneo muhimu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la pili, juu ya walimu wa mchepuo wa kilimo. Ameeleza hapa Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, wakati anatoa taarifa juu ya idadi ya nafasi za ajira zilizotolewa, iko nafasi ya ajira za Walimu, ziko nafasi za eneo la afya. Katika eneo hili la elimu naamini kabisa kama kipaumbele ndani ya halmashauri zetu kitaainishwa wazi, kwamba tunahitaji Walimu watakaokwenda kusaidia kusimamia eneo la kilimo, basi sisi kama Serikali sikivu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tuko tayari kwenda kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba malengo ya kuhudumia wananchi wetu yanakamilika. Ahsante.

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaajiri watumishi wa kada ya ulinzi, upishi na makatibu muhtasi katika shule za sekondari za kata nchini?

Supplementary Question 2

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Tuna walinzi katika shule zetu za msingi, sekondari, vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya lakini hakuna…

SPIKA: Swali.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, je, kada hizi zinalipwa na Mamlaka ipi hasa kwa sababu kuna mkanganyiko mkubwa?

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, juu ya ajira hizi za walinzi na kada mbalimbali kama ulivozitaja walipaji ni halmashauri kutokana na ikama ambayo wamejipangia.

Name

Agnes Elias Hokororo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaajiri watumishi wa kada ya ulinzi, upishi na makatibu muhtasi katika shule za sekondari za kata nchini?

Supplementary Question 3

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itaweka kipaumbele kuajiri Maafisa Mipango na Maendeleo ya Jamii ili kupanga na kuchechemua maendeleo katika halmashauri zetu?

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Hokororo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuajiri Maafisa Mipango na kada mbalimbali katika Serikali kama ambavyo imekuwa inaombwa vibali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Vile vile, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetoa vibali 30,000 vya kuajiri kada mbalimbali. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama eneo hilo alilolieleza na uhitaji ambao tunaufahamu, nataka nimhakikishie kabla ya mwisho wa mwaka jambo hilo tutalifanyia kazi tuweze kuhakikisha kwamba hiyo kada imeenea kama ambavyo imeombwa. (Makofi)