Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza: - Je, ni kwa kiasi gani Mkoa wa Mtwara umewekeza na unanufaika na uchumi wa Bluu?

Supplementary Question 1

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza; miongoni mwa watu wanaolima chumvi kwa wingi ni wakazi wa Mkoa wa Mtwara, changamoto kubwa wanayoipata ni soko la uhakika. Nataka kujua mkakati wa Serikali ni upi kuhakikisha wakulima wale wa chumvi wanapato soko la uhakika?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, ili kuchochea uchumi wa bluu; uwepo wa dhana bora za uvuvi ikiwemo meli ya uvuvi ya kisasa ni jambo la muhimu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuleta meli ya kisasa ya uvuvi katika Bahari ya Hindi iliyopo Mkoa wa Mtwara?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA:
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli moja ya changamoto kubwa tuliyonayo kwa wazalishaji wa chumvi hasa wadogo ni changamoto ya soko la uhakika kwa chumvi yao na hasa ambayo ni malighafi kwa maana ya kuwa siyo finished product.

Mheshimiwa Spika, moja ya mikakati ya Serikali tumeshaanza kutekeleza na kuzuia uingizaji wa malighafichumvi au chumvi ambayo inatumika kuzalisha chumvi ya kula kutoka nje. Hili tumeshalisema na tunaamini viwanda vya ndani vinavyozalisha chumvi vitatumia malighafi zilizopo kwa maana ya chumvi inayozalishwa na wakulima wadogo wadogo wakiwemo wa Mkoa wa Mtwara.

Mheshimiwa Spika, zaidi tunahamasisha katika masoko ya kikanda kwa maana ya Afrika Mashariki na SADC ili tuone nchi ambazo zinakosa au hazina malighafi ya chumvi zinatumia malighafi ya chumvi yetu ikiwemo inayotoka katika Mkoa wa Mtwara ambao tunaamini itakuwa ni chumvi ambayo inapelekwa kwenye masoko hayo ili waweze kunufaika zaidi na uzalishaji wa chumvi katika maeneo haya ya Mtwara.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa meli ya kisasa ya uvuvi kama nilivyosema Serikali tunaedelea kuhamasisha uwekezaji katika maeneo yote ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uchumi wa bluu ambayo nayo inahusisha kuwa na meli za kisasa ambazo zingeweza kusaidia kuwa na uvuvi wa kisasa zaidi wenye tija. Serikali pia kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea na mikakati mbalimbali ambayo mojawapo ni kuona namna gani ya kutafuta wawekezaji wengi ambao wanaweza kuvua kwa tija katika bahari yetu.