Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Neema Kichiki Lugangira
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: - Je, Serikali imejiandaaje kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji nchini?
Supplementary Question 1
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali ni vyema tutambue kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaweka jitihada kubwa sana kuimarisha mazingira wezeshi na kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi na hiyo imeenda sambamba kabisa na Mheshimiwa Rais kuamua kuchukua jukumu la uwekezaji na kuweka chini ya Ofisi ya Rais, pamoja na kuteua Katibu Mkuu wa Uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Blueprint imeelekeza kwamba ili kuimarisha mazingira wezeshi lazima tuwe tuna ardhi inayojulikana kwa ajili ya uwekezaji kwa maana ya kwamba ardhi hiyo ipimwe na iainishe ni uwekezaji gani ambao uatafanyika sasa je, mpaka hivi sasa Serikali imepima kiwango gani cha ardhi na ramani ya ardhi hiyo kwa ajili ya uwekezaji inapatikana wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; pamoja na kwamba Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 2022 ilipitishwa ndani ya Bunge lako Tukufu kwenye blueprint imeelekeza zaidi ya sheria 20 ambazo zinatakiwa zifanyiwe maboresho.
Kwa hiyo ningependa kufahamu kutoka kwa Serikali, je, ni lini Serikali italeta hizo sheria zingine zaidi ya 20 ili zifanyiwe maboresho ili kuhakikisha kwamba tunaimarisha mazingira wezeshi hapa nchini na hivyo kuunga mkono na kutokufifisha jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha na kuleta wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi? Ahsante.
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi tumeshaanza kutekeleza MKUMBI au Blueprint na moja ya utelekezaji huo ni kuhuisha au kutunga Sheria mpya ya Uwekezaji lakini pia ninyi ni mashahidi katika Bunge liliopita tumepitisha maboresho ya sheria mbalimbali zaidi ya 19 ambazo ziligusa sekta tofauti tofauti.
Kama nilivyosema utekelezaji wa MKUMBI au blueprint sio kitu cha siku moja, kwa hiyo tunaendelea kutekeleza moja ya maeneo ambayo Mbunge ameyasema ni hayo ya kupitia baadhi ya sheria na kanuni lakini pia kuboresha baadhi ya taratibu ambazo zipo na tunazoona ni changamoto au kero kwa ajili ya kuboresha uwekezaji hapa nchini, nakushukuru.
Name
Ghati Zephania Chomete
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: - Je, Serikali imejiandaaje kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji nchini?
Supplementary Question 2
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Pamoja na uwekezaji mzuri kufanyika wa kujenga Kiwanda cha Nguo cha MUTEX Musoma, lakini mpaka sasa kiwanda kile hakifanyi kazi. Je, ni upi mkakati wa Serikali kufufua kiwanda hicho?
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli moja ya mikakati tunayoifanya Serikali ni kuona namna gani tunafufua viwanda ambavyo havifanyi kazi na sisi kama Serikali tumeshaanza kuona vile viwanda ambavyo vilikuwa vimepewa watu binafsi na hawaviendelezi kuvirudisha Serikalini na hatua ya pili sasa ni kuvitafutia wawekezaji ili waweze kuwekeza katika viwanda hivyo na kimojawapo ni kiwanda hiki cha MUTEX kilichopo kule Musoma, nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved