Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. David Mathayo David
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Same Magharibi
Primary Question
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: - Je, ni kero zipi za Muungano zimetatuliwa na zipi zimebaki?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; kero za Muungano zimechukua muda mrefu sana na sasa hivi tuko Awamu ya Sita lakini bado kuna kero na zingine mpya zinajitokeza. Ningependa kuuliza ni mambo gani ambayo yanakwamisha kukamilika kwa kero zote za Muungano?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Sheria Mama ni Katiba na katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania suala la uchimbaji na utafutaji wa mafuta na gesi vimeorodheshwa kama masuala ya Muungano na jibu la Serikali linaonesha kwamba changamoto hii imemalizika. Je, suala hili kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano limefutwa kwa sheria gani?
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa David Mathayo, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie Mbunge na Watanzania kwa ujumla kwamba suala la utatuzi wa changamoto za Muungano halijakwama wala halijasuasua, ni suala ambalo linakwenda kwa sababu mpaka hivi tunavyozungumza asilimia ya changamoto zilizotatuliwa ni nyingi tofauti na zilivyokuwa. Vile vile, katika orodha ya mambo yaliyotatuliwa yapo mengi, tulikuwa tuna changamoto nyingi, lakini sasa hivi kama atarejea kwenye jibu langu la msingi jumla ya changamoto 22 zimekwishatatuliwa. Zilizobakia ni changamoto ambazo Kamati zinazohusika ziko mbioni na zinakaa kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hizi na Muungano huu uendelee kudumu kama kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili, ni kweli kwamba suala la utafutaji na uchimbaji wa gesi asilia lilikuwa ni changamoto, ilifika wakati lilikuwa Iina mvutano kidogo, lakini kwa sababu ya busara ya viongozi wetu wanaosimamia Muungano huu na Kamati zilizoundwa zikiwemo Kamati za Makatibu Wakuu, Kamati za Wataalam na Kamati zile za Mawaziri, zimefikia mahali pazuri katika kulitatua jambo hili, tena limetatuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zote na sasa hivi tayari Zanzibar iko vizuri na Muungano unakwenda vizuri katika suala hili la mafuta na gesi.(Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved