Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: - Je, ni lini Wananchi wa Kitongoji cha Nyamichele watalipwa fidia kutokana na madhila waliyoyapata kutoka Mgodi wa Barrick?
Supplementary Question 1
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru na nasikitishwa kwa majibu ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mgodi wa North Mara walifanya tathmini pamoja na kubomoa nyumba na mazao ya wananchi mwaka 2013, ambapo walifanya tathmini kwa phase sita, baadae baada ya miaka kadhaa wakaja wakasema wanahitaji phase nne tu ambazo wamelipa zikabaki phase mbili zenye wananchi 1,586 na wakasema kama walivyosema kwamba wangelipa kifuta jasho ambapo mpaka sasa hivi wananchi hawa hawajaweza kulipwa kifuta jasho takribani miaka kumi, ningependa kujua ni lini Serikali itahakikisha inasimamia sheria zile za madini na za ardhi kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanalipwa fidia yao stahiki ya kubomolewa nyumba, mazao na muda uliopotea kutofanya shughuli za maendeleo kwa muda wa miaka kumi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, mwaka 2018 baada ya wananchi hao kuona kwamba inachukua muda hawalipwi hicho kifuta jasho kinachosemwa waliifungua kesi Mahakama Kuu, ambapo Waziri wa Madini Mheshimiwa Biteko alienda kule Nyamongo akawasihi wananchi waondoe hii kesi mahakamani mwaka 2018 lakini mpaka sasa hivi wananchi hao bado hawajaweza kulipwa. Mwaka huu mapema walifuatilia kwa Mthamini Mkuu wa Serikali na akakiri kwamba hajapokea document yoyote ile au taarifa yoyote ile ya kutoka mgodini kuhakikisha kwamba wananchi wanaweza kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kujua ni kwa nini pale ambapo mgodi au ardhi ya wananchi inatwaliwa Serikali inashindwa kufuata sheria zilizopo kuhakikisha kwamba wananchi wanalipwa stahiki zao mara moja? (Makofi)
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya Mheshimiwa Esther Matiko, kama ifuatanyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali lake la kwanza kwamba ni lini hawa wananchi wanaokaa katika Phase Mbili zilizobaki ambazo hazijafidiwa watalipwa. Napende tu kumhakikishia kwamba baada ya kampeni kumwajiri Mkandarasi aliyefanya tathmini kufahamu watu wanostahili kulipwa na kufahamu kiwango ambacho kinastahili kutolewa kama kifutajasho kwa sasa hivi ndani ya miezi miwili ijayo utaratibu wa malipo hayo utaenda kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali lake la pili, kwamba ni kwa nini Serikali isisimamie sheria yake na kuhakikisha kwamba wananchi ambao waliondoa kesi Mahakamani mwaka 2018 wanalipwa, napenda tu kumhakikishia kwamba Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan ni Serikali inayopenda kutenda haki, nasi kama Wizara kwa niaba yake tunasimama kidete kuhakikisha kwamba wananchi hawa baada ya hizi tathmini kuwa zimeshafanyika na sasa tumeshafikia mwisho wake na wanakwenda kupata malipo yao, ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuweza kuongezea katika majibu mazuri ambayo ameyatoa Naibu Waziri wa Madini. Nilitaka kuzungumzia suala la fidia kwa nini fidia zinachelewa kulipwa na kwa nini pengine hali inatokea namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la fidia ucheleweshaji wa fidia wakati mwingine unatokana na udanganyifu unaokuwepo kwenye maeneo husika. Kwa mfano, katika masuala mazima ya kuwa na tuna lugha rahisi inaitwa tegesha, unakuta mazao yanaota kwa haraka kwa siku mbili mazao yapo ambayo yanakuwa ni pandikizi kwa hiyo katika suala zima la kufanya uthamini kadri unavyokwenda unakuta kuna mabadiliko kwenye lile eneo, lakini wanasahau kwamba Serikali huwa inachukua picha za anga kabla ya kufanya zoezi na inaangalia picha za nyuma na kuweza kujua kabla ya uthamini kuanza kulikuwa na nini pale na unapoanza uthamini unakuta kuna mali nyingi zinaongezeka, upandaji wa mazao ambayo mengine yanapandwa usiku na mchana. Kwa hiyo, wakati mwingine niwaombe tu wananchi ya kwamba Serikali ina nia na dhamira njema ya kuweza kulipa fidia, kwa hiyo tuache ule udanganyifu ambao unachelewesha haki za Watanzania katika kulipwa fidia zao.
Name
Agnes Mathew Marwa
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: - Je, ni lini Wananchi wa Kitongoji cha Nyamichele watalipwa fidia kutokana na madhila waliyoyapata kutoka Mgodi wa Barrick?
Supplementary Question 2
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uhalisia huohuo kwamba Serikali ilikwishafanya uthamini na ikaelewa kwamba ni watu wangapi wanahaki ya kulipwa maeneo yao katika maeneo yambayo wamechukua Wawekezaji.
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo hili kutokana na kwamba wao Wawekezaji wameshapata faida ya kutosha na sasa mashimo ndiyo yatakayobaki na wananchi wamesubiri kwa muda mrefu na ni tatizo la muda mrefu? (Makofi)
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kwamba tathmini zote zimeshafanyika na kiwango cha malipo kinachostahili kulipwa kimeshajulikana, mchakato unaoendelea kwa sasa ni huo wa kuhakikisha kwamba wanaostahili kulipwa, kiwango wananchostahili kulipwa na maelewano ya wao kukubali malipo hayo ndiyo yanayoendelea na Wizara tutaendelea kusimamia hilo liweze kutekelezwa.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved