Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rehema Juma Migilla
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Primary Question
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: - Je, Serikali imetoa mwongozo gani kuhusiana na kiwango cha ubora wa taa zinazowekwa barabarani?
Supplementary Question 1
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kutoa masikitiko yangu kwa Serikali, majibu yaliyotolewa na Serikali kiukweli hayaridhishi. Kama Serikali yenye wajibu wa kutoa mwongozo kuhusu namna gani taa za barabarani ziwekwe haijatoa mwongozo mpaka sasa, hali hii inasababisha mamlaka zilizokasimiwa kufanya shughuli hii kuweka taa za barabarani kwa utaratibu wanaotaka wao. Kwa sasa hivi ukiangalia maeneo mengi taa zilizowekwa barabarani ni hafifu mno, hazina ubora, lakini bado taa hizo hizo zilizowekwa barabarani zimewekwa aidha upande mmoja hali ya kwamba ikitokea labda zimeungua eneo hilo linabaki giza. Hata hivyo, taa hizo hizo hazifanyiwi maintenance kwa muda unaotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; je, Serikali iko tayari sasa kama yenye mamlaka kutoa waraka au mwongozo ili mamlaka zilizokasimiwa ziweze kuleta maana halisi ya uwekaji wa taa barabarani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Jimbo langu la Ulyankulu tangu kuundwa kwake halijawahi kuwa na barabara ya lami hata kilomita moja. Hata hivyo, kwa sasa kuna ujenzi wa kilomita moja na nusu ambao unatekelezwa kama ahadi ya Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Je, Serikali iko tayari kwanza kumalizia kilomita moja na nusu ya lami iliyobakia na kuweka taa za barabarani?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rehema Juma Migila, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba TEMESA ndiyo ambao wamepewa kazi ya kuweka na kusimamia taa za barabarani. Pia TEMESA ndio wataalam wa kufanya kazi hizo kwa upande wa Serikali. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pia kwamba taa kulingana na teknolojia inavyobadilika unaweza ukasema utaweka taa hizi lakini kadri teknolojia inavyobadilika taa zimeendelea kubadilika. Zamani tulikuwa tunatumia umeme sasa hivi tunatumia solar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama unaweza ukaweka Mwongozo unaweza pia ukawa unashindwa kwenda na teknolojia. Ndiyo maana katika jibu langu la Msingi nimesema wanakwenda kulingana na mabadiliko ya teknolojia na nini wenzetu duniani wanachofanya na wataalam ndicho wanachokifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kwamba pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna aina mbili ya barabara na tuna taasisi mbili zinazosimamia barabara. Katika Mkoa wa Tabora ambao Mheshimiwa Mbunge anatoka, katika mtandao wa taa mkoa mzima tuna taa 1,568 mpaka leo ninavyoongea ni taa 50 tu ambazo haziko katika mtaa mmoja ambazo ni mbovu. Kwa hiyo, inawezekana barabara anayoisema inawezekana si barabara ambayo pengine inasimamiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS). Hata hivyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama kuna changamoto ambayo mtaa mzima hauna taa nitaomba baada ya hapa tukutane naye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Ulyankulu tutakamilisha ujenzi na tutamwekea taa za barabarani 47 katika kituo chake hicho cha Ulyankulu, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved