Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Issa Ali Abbas Mangungu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbagala
Primary Question
MHE. ISSA A. MANGUNGU aliuliza:- Jimbo la Mbagala lina wakazi zaidi ya 800,000 kutokana na sensa ya watu na makazi lakini ina Mahakama ya Mwanzo Kizuiani tu. (a) Je, kwa nini Serikali imeshindwa kujenga mahakama katika Jimbo la Mbagala kwa kuzingatia idadi kubwa ya wakazi? (b) Kwa kuwa kuna mahitaji makubwa ya huduma za mahakama Jimbo la Mbagala katika Kata za Chamazi, Mbande, Kijichi, Kibungwa, Kibondemaji na Tuangoma; je, Serikali ipo tayari kujenga mahakama katika kata hizo hata kwa mpango wa dharura?
Supplementary Question 1
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru, na ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba, lakini ningependa kumuuliza maswali mawili.
Swali la kwanza; viwanja katika eneo la Kijichi, Tuangoma na Chamazi vipo na nitampelekea orodha hiyo baada ya kikao hiki, je, yupo tayari sasa kuanza mpango huo wa ujenzi haraka iwezekanavyo ili wananchi waweze kupata huduma hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mahakama ya Kizuiani ambayo iko moja inahudumia zaidi ya watu 800,000, haina choo, haijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu, ipo karibu na soko, uendeshaji wa kesi pale unakuwa ni mgumu, haki inachelewa kupatikana; je, Serikali ina mpango gani wa kufanya marekebisho na matengenezo ya dharura katika mahakama ile?
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kwa upungufu wa mahakama 102 kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Serikali yenyewe haioni kwamba inachelewesha haki na kusababisha vitendo viovu kama rushwa na mambo mengine?
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kwanza, anasema viwanja vipo, hiyo ni taarifa nzuri sana kwangu, namuomba sasa atuwasilishie rasmi hivyo viwanja ambavyo tayari vina nyaraka zake.
Mheshimiaw Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mangungu kwamba tuna pesa ya kujengea mahakama sasa, mkikumbuka mapema mwaka huu Mheshimiwa Rais aliagiza pesa yote ya maendeleo ya mahakama itolewe, kwa tuna shilingi bilioni 12.3 tayari, lakini vilevile Waheshimiwa Wabunge mmetuidhinishia shilingi bilioni 22 katika mwaka huu wa fedha, tuna jumla ya shilingi bilioni 34.3 na hizo pesa tunajenga Mahakama za Mwanzo 50, anayewahi kwa hoja za msingi tutampa hiyo mahakama, sasa nakuomba Mheshimiwa Mangungu badala ya kuongea jenga hiyo hoja kimaandishi.
Mheshimiwa Spika, tunajenga vilevile Mahakama za Wilaya 20 na tunajenga Mahakama Kuu mpya mbili katika mikoa ya Mara na Kigoma na vilevile Mahakama za Hakimu Mkazi tunajenga saba, tano katika mikoa hii mipya na mahakama nyingine mbili katika mikoa ya Ruvuma na Lindi.
Mheshimiwa Spika, la pili; Mheshimiwa Mangungu anasema mahakama yake haina choo, hilo ungelisema hata bila hapa mbele ya Bunge ningeweza tu kukusaidia naomba tuonane baadaye, ni vitu vidogo sana kuviongelea hapa. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved