Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Primary Question

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: - Je ni lini Serikali itafungua Ofisi ya Madini Liwale?

Supplementary Question 1

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaja na swali la nyongeza kwanza nisikitike kwa majibu ambayo hayajaridhisha. Hayajaniridhisha mimi wala wananchi wa Liwale. Nina sababu zifuatazo; kwanza Wizara haikuzingatia umbali uliopo kutoka Liwale kwenda Nachingwea lakini vile vile haikuzingatia miundombinu ya usafiri uliopo kutoka Liwale kwenda maeneo iliyotajwa. Hata Mkoa wenyewe wa Lindi ukiuangalia ukubwa wake Wilaya ya Liwale ndiyo yenye eneo kubwa Mkoa wa Lindi. Takriban theluthi moja ya Mkoa wa Lindi iko Liwale. Sasa kuniambia kwamba Wilaya ya Liwale ina shughuli pungufu ya uchimbaji wa madini napata shida kukubaliana na jambo hilo. Hii ni kwa sababu kuna eneo kubwa sana ambalo linazungumzwa Wilayani Nachingwea, eneo la Kitowelo. Eneo hili la Kitowelo liko mpakani na Liwale...

MWENYEKITI: Mheshimiwa uliza swali la nyongeza.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Swali langu: -

(a) Je, Wizara hii ya Madini haiko katika mfumo ule wa kusogeza huduma kwa wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana kama ingekuwa kwenye hiyo mpango wa kusogeza huduma kwa wananchi kwa karibu basi na sisi tungepatiwa Ofisi. Ile taasisi ya GST ilikuja Liwale ikakaa mwezi mzima ikakaa pale Liwale waliweka kambi Mpigamiti pale, mwezi mzima. Wamefanya utafiti wa madini lakini mpaka leo hatujapata sisi kama Wilaya, kupata hata kile kitabu cha matokeo yale ya uchimbaji wa madini. Matokeo yake sasa watu kutoka Kanda ya Ziwa ndio wanachukua vitalu kule kwa wingi sana kwa sababu matokeo yote yako hapa GST Makao Makuu.

(b) Je, Wizara ya madini iko tayari sisi kama Halmashauri kutupatia vile vitabu vya matokeo ya utafiti ule?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI K.n.y. WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kuchauka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la kwanza, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Serikali ya wananchi, na nia yake kubwa ni kupeleka huduma kwa wananchi. Kama tulivyosema kwenye jibu la msingi, ni kwamba, ofisi zitafunguliwa kulingana na Wingi na uhitaji wa ofisi hizo kwenye maeneo hayo. Lakini pia nimemalizia kwa kusema Wizara itaendelea kuboresha huduma kwa wadau wake kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimuhalkikishie Mheshimiwa Kuchauka, mpaka sasa Tanzania ina masoko 42 ya kununua na kuuza madini, ina vituo 93. Kadri maeneo yanavyozidi kuongezeka na uhitaji unavyotokea huduma hii inazidi kusogezwa kwa wananchi. Hata katika Jimbo la Liwale watakwenda kutizama na kuona wingi na upana wa mahitaji ya ofisi hizi, na zitapelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili; nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge; wananchi wa Liwale niliwashauri kutembelea ofisi za madini watapata hizo taarifa za madini yaliyopo kama ambavyo anasema, kwamba waliotoka sehemu za mbali wamepata taarifa hizo. Lakini pia ofisi itahakikisha inatoa taarifa hizo kwa sababu si za siri, kwa wananchi, ili waweze kuzi-access na kuweza kuingia kwenye maeneo hayo kuweza kuchimba madini ili kunufaika nayo. Sisi sote tunaohitaji kunufaika nayo.