Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: - Je, lini Serikali itahakikisha Watanzania wanaofanya kazi kwenye Kampuni za Kichina wanalipwa vizuri kwa mujibu wa sheria?

Supplementary Question 1

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Waziri kuna viwanda katika Mkoa wa Pwani sehemu za Mbagala na sehemu za Mkuranga wanawapa wafanyakazi shilingi 4,000 kwa siku. Mfanyakazi anaingia saa mbili asubuhi anatoka saa 11 jioni anapata ujira wa shilingi 4,000; je, hii ni sawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali mnasimamia vipi matajiri na waajiri wakubwa ambao wanadaiwa madeni na wafanyakazi kwa muda mrefu. Makampuni ya Chai ya Rungwe, Kampuni ya Kiwira Coal Mine na Kampuni ya TANESCO waliokuwa vibarua takribani sasa ni miaka mitano hawajapata fedha zao.

Je, Serikali mnasimamiaje suala hilo kuhakikisha watu hawa wanapata haki ambayo wanastahili waliyoitendea kazi? (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge ni kweli tumeendelea kufanya kaguzi, kwa mujibu wa sheria ipo namna na mikataba ya kazi ambayo inatambua aina ya ajira mtu anayoifanya. Wapo wanaofanya kazi kwa maana ya permanent and pensionable kwa maana ya mkataba unavyoeleza lakini pia wapo wanaolipwa kwa mpango wa wiki moja, kila baada ya wiki, wapo wanaolipwa kila baada ya mwisho wa mwezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maeneo hayo, imebainika ndiyo moja ya tatizo ambalo tumelibaini Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, wapo waajiri ambao wamekuwa wakikwepa kuwapa mikataba ya kazi wafanyakazi hawa ili kuendelea kuwaita vibarua na wakafanya kazi kwa muda mrefu. Huo ni unyonyaji mkubwa na Ofisi ya Waziri Mkuu tayari tumekwishaanza kuchukua hatua na tunafanya kaguzi, tunaenda kuangalia historia wafanyakazi wamefanya kwa kipindi gani na ni aina gani ya kazi anayoifanya ili kuweza kuhakikisha tunawaingiza kwenye mfumo wa kuwa na mikataba ya kazi ili haki zao ziweze kulindwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni lile linalohusiana na udhulumaji ambao unafanyika au kutokulipa maslahi ya wafanyakazi. Vivyo hivyo katika Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini inaeleza moja ya mambo ni kukubaliana katika mkataba, yaandikwe na yaainishwe wazi. Kitendo cha waajiri kutokuwalipa mishahara au maslahi yao ni kuvunja Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini lakini sambamba na hilo, ndani ya mkataba kuna masuala ya Pay As You Earn kwa maana ya kodi ya Serikali. Maana yake asipolipwa maana yake anakwepa pia kodi ya Serikali, pia kuna kipengele ambacho ni cha lazima cha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, asipolipwa mshahara maana yake anakwepa pia kupeleka fedha kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu kipo kipengele cha WCF kwa maana ya workers compensation. Kama halipwi mshahara maana yake hiyo pia ni eneo ambalo anakosa haki hiyo ya kuweza kulipwa, sambamba na hilo sheria nyingine tumeendelea kuzichukua na tunawapeleka mahakamani kwa summary suits maana yake hana muda wa kujitetea na hatua tunazichukua na sasa yapo mashauri ambayo tunaendelea nayo, hivyo kwenye maeneo hayo mahsusi nitaomba pia aniambie ni wapi ili tuweze kushirikiana naye kuweza kuchukua hatua. Ahsante. (Makofi)

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Primary Question

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: - Je, lini Serikali itahakikisha Watanzania wanaofanya kazi kwenye Kampuni za Kichina wanalipwa vizuri kwa mujibu wa sheria?

Supplementary Question 2

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mufindi Kampuni ya Ekaterra imeinunua Kampuni ya UNILEVER jambo ambalo limeacha malalamiko makubwa ya wananchi kukosa stahiki zao. Je, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu haioni umuhimu wa kuwasaidia wananchi hawa kumaliza malalamiko yao, ikiwa ni pamoja na kufika pale ili waendelee kunufaika na Taifa lao?

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kihenzile kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru kwamba suala hili Mheshimiwa Kihenzile amekuwa analifuatilia kwa muda mrefu la kampuni hiyo ya UNILEVER baada ya kuingia mkataba wa kwamba sasa kampuni inakuwa winded up na kuchukuliwa na kampuni nyingine. Utaratibu uliopo kampuni inaponunuliwa au inapoenda kufilisika wajibu wa kwanza ni kuhakikisha wametambua madeni lakini pia kwa maana ya liabilities pamoja na assets zilizopo. Kwa wafanyakazai hatua ya pili itakuwa sasa ni kulipa madeni ikiwemo madeni ya wafanyakazi kwenye kampuni husika, hata kama kuna transfer ya umiliki, jambo la kulipa madeni ambayo ni liabilities ni la msingi na ni la kuzingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo kwenye eneo hili la kesi ya UNILEVER Mheshimiwa Mbunge nimueleze tu kwamba kuna hatua mbili ambazo Ofisi ya Waziri Mkuu ilichukua. Hatua ya kwanza Kamishna wa Kazi alikutana na wafanyakazi hao na kuchukua malalamiko yao. Wapo ambao walifukuzwa kazi wakati huo bila kufuata utaratibu wa retrenchment tuliagiza warudishwe kazini. Pia lipo kundi la pili la wafanyakazi ambao walilipwa walikuwa zaidi ya 500 na hatua ya tatu kundi la tatu kwenye wafanyakazi hao ni wale ambao bado maslahi yao yalikuwa hayajaelezeka vizuri, wapo ambao walikuwa wana mikataba na wasiokuwa na mikataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ambayo tumeichukua tuliwaelekeza waende CMA ambapo shauri linaendelea mpaka sasa katika Mahakama ya Kazi na hatua ya tatu ambayo tunaenda kuichukua ni kuhakikisha baada ya maamuzi ya CMA na wale ambao walikuwa bado hawajaainishwa kwamba wako kwenye eneo gani la vipengele vya mikataba, wakutane na Kamishna wa Kazi ili haki zao ziweze kulindwa. (Makofi)