Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Benaya Liuka Kapinga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Vijijini
Primary Question
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: - Je, lini Serikali itapitia upya mipaka na kuweka alama za Hifadhi katika Vijiji vya Ndongosi, Mtunduaro, Litumbandyosi na Kiwombi?
Supplementary Question 1
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini niiombe uhakiki huu unaoshirikisha wananchi uhusishe pia Kijiji cha Chunya - Kata ya Mpapa; Kijiji cha Barabara - Kata ya Matili; lakini pia Kijiji cha Kimbindachini - Kata ya Muungano. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mbinga ni milimani, na kwa hiyo, sasa kutokana na uhifadhi maeneo mengi ya milimani tunapewa…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kapinga naomba uulize swali moja kwa moja. Swali la kwanza na la pili, tafadhali; uliza swali lako la msingi.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio nilikuwa nauliza swali hapo, kwamba basi acha ulivyonielekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kuwafanya wananchi hawa waweze kuishi na misitu katika milima iliyopo Wilaya ya Mbinga? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali inatoa kauli gani katika maeneo yaliyoanzishwa Miradi ya Panda Miti Kibiashara bila kushirikisha wananchi, ili kuwarejeshea maeneo haya wananchi husika? Ahsante.
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mpango wa kutoa elimu, nitoe tu maelekezo kwa watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii hususan Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, tunapoenda kuainisha hii mipaka wahakikishe kwamba tunashirikisha wananchi walioko katika maeneo hayo ili kuwepo na urahisi wa kutambua mipaka iliyopo na kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutalizingatia, lakini pia tutaendelea kutoa elimu ya namna ya uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la pili ambalo amelisema kwenye Mradi wa Panda Miti Kibiashara; kikawaida mradi huu unawawezesha wananchi kujiinua kiuchumi kupitia mazao ya miti, na mara nyingi tunashirikisha wananchi kabla ya mradi huu kufika katika eneo husika. Kwa hiyo, kama kuna maeneo ambayo tumepeleka mradi huu halafu hatukushirikisha wananchi, basi tumefanya makosa na tutaenda kupitia upya utaratibu uliopo ili wananchi waweze kufaidika na miradi hii ya Panda Miti Kibiashara.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved