Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Boniphace Nyangindu Butondo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kishapu
Primary Question
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: - Je, lini mabwawa ya mifugo yatachimbwa Kata za Lagama, Masanga Mwamalasa, Ngofila, Bunambiyu, Mwasubi na Somagedi – Kishapu?
Supplementary Question 1
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali yaliyotolewa. Ninaomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo jitihada kubwa ambazo zilishafanywa huko nyuma na wananchi kupitia utaratibu wa Vijiji vya Ujamaa na nguvu za wananchi kuhakikisha kwamba wanachimba mabwawa katika kipindi cha nyuma. Hapa miaka ya 90 mpaka 2000, Serikali iliweza kuchiba baadhi ya mabwawa, lakini mabwawa yale ni kama yalitelekezwa na baadaye yakawa yameharibika. Kuna uhitaji ama umuhimu wa kuyafufua yale mabwawa ambayo yalichibwa nyakati hizo, kabla ya kuweka mkakati wa muda mrefu ule wa kujenga mabwawa haya.
Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha mabwawa yaliyopo katika maeneo hayo yanafufuliwa kwanza?
Name
Alexander Pastory Mnyeti
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natumia nafasi hii kumpongeza sana Mbunge wa Kishapu, Mheshimiwa Boniphace Nyangindu, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kufatilia namna ambavyo wafugaji wake wanatakiwa wawe na maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyouliza swali lake la msingi, ni kweli kwamba Serikali ipo na mipango mingi ya kufufua mabwawa yote yaliyokufa. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge hili tutatuma wataalam kuja kufanya tathmini katika jimbo lake. Tujue tathmini hiyo, mabwawa yako mangapi na yanahitaji nini ili Wizara kamaSerikali Wizara iweze kutuma namna ya kuyafufua haya mabwawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua mabwawa ambayo yanahitaji kufufuliwa na Serikali yapo maeneo mengi. Serikali tunamuahidi Mheshimiwa Mbunge Serikali imejipanga vizuri. Tukishapata kujua gharama za shilingi ngapi inatakiwa kwenda kuyafufua hayo mabwawa tupo tayari kwenda kuyafufua mabwawa hayo kwenye Jimbo la Kishapu. (Makofi)
Name
Yahya Ally Mhata
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Primary Question
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: - Je, lini mabwawa ya mifugo yatachimbwa Kata za Lagama, Masanga Mwamalasa, Ngofila, Bunambiyu, Mwasubi na Somagedi – Kishapu?
Supplementary Question 2
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na migogoro mikubwa kati ya wafugaji na wakulima. Ndani ya Jimbo langu la Nanyumbu wakulima wa Kata ya Lumesule wana mgogoro mkubwa na wafugaji wa eneo hilo. Hii imepelekea kuhatarisha hata maisha yao. Hivi ninavyozungumza wakulima wako katika hali mbaya sana ya usalama kati yao na wafugaji.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri upo tayari mara baada ya kuahirishwa Bunge letu kesho kutwa, mimi na wewe tukafuatana tukaenda kwenye Kata husika kutatua mgogoro uliopo kati ya wakulima na wafugaji? (Makofi)
Name
Alexander Pastory Mnyeti
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kama Wizara iko tayari kuambatana naye baada ya Bunge hili. Wizara iko tayari kuandamana na Mheshimiwa Mbunge. Tuko tayari kwenda kuona mgogoro huu na kuutafutia ufumbuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla Wizara haijaenda kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huu Serikali hii ni kubwa, wapo viongozi ambao wanapaswa kuanza kuhangaika na migogoro hii kabla Wizara haijafika huko. Yupo Mheshimiwa DC, nitoe wito sana, Mheshimiwa DC na wataalam wote waliopo huko wa Mifugo na Kilimo kwenda kutatua mgogoro huu kabla Wizara haijafika huko kutafuta ufumbuzi wa kudumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ina Wataalam wa Kilimo na Mifugo, ina Mheshimiwa DC ambaye ni Kamisaa wao. Tunaomba kabla Wizara haijafika huko nitoe wito kwa wakuu wote waende kutatua mgogoro huu kabla hatujafika huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved