Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha kuwa wakulima wa korosho wanapata mikopo nafuu ili waweze kugharamia kilimo hicho?

Supplementary Question 1

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwanza baada ya Serikali kuanza kutoa ruzuku za pembejeo baadhi ya benki zimeacha kabisa kutoa mikopo kwa wakulima wakati gharama ya zao la korosho sio pembejeo tu, kuna gharama ya matayarisho ya mashamba na gharama za uvunaji.

Je, Serikali inatoa tamko gani kwa benki hizo? (Makofi)

Swali langu la pili, changamoto ambazo zinawakabili wakulima wa mazao ya kimkakati, pamba, korosho, chai, alizeti zingeweza kutatuliwa na mfuko wa maendeleo ya kilimo.

Serikali inaweza kutoa tamko, je, ni lini sasa Mfuko huo utaanza kufanya kazi rasmi ili kuwasaidia wakulima hawa. (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwezeshwaji wakulima kupitia taasisi za fedha, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi Serikali pamoja na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, tutakaa kwa pamoja na taasisi za kifedha kuona namna bora ya kuweza kuwawezesha wakulima hasa wa korosho na hivi sasa tumeanza hatua za awali, tumeshakaa na benki, ziko changamoto ambazo zimejitokeza hasa za urejeshaji wa mikopo hii, lakini hii ilitokana na changamoto kwamba wakulima wengi walikuwa hawajasajiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tumeanza kuwasajili wakulima, kila mkulima atatambulika eneo lake alipo, shamba lake lilipo na ukubwa wa shamba ili kuirahishia benki namna bora ya kuweza kuwapatia mikopo na tunaamini kupitia njia hii wakulima wengi zaidi watapata mikopo katika taasisi za fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa mujibu wa Sheria za Fedha za Umma Sura Namba 347 Kifungu cha 17 (1) cha Sheria ile, kimetoa amri ya uanzishwaji wa Mfuko wa maendeleo ya kilimo. Mfuko tayari tumeshapata amri ya kuanzisha, umeanza kazi na tumeshateua na Meneja wa Mfuko na Mhasibu Mkuu, punde tutaendelea kuhakikisha kwamba tunapata vile vyanzo vya kuutunisha Mfuko huu ili basi inapotokea changamoto mbalimbali na hasa katika kuwawezesha wakulima kuweza kupata huduma mbalimbali Mfuko huu uweze kutumika.