Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jerry William Silaa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukonga
Primary Question
MHE. JERRY W. SILAA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Pugu - Majohe - Viwege njia nne na Kampala - Bwera - Rada hadi Chuo?
Supplementary Question 1
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri ya kuona mahitaji ya barabara za lami kwenye Jimbo la Ukonga. Naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mvua zinazoendelea kunyesha Jijini Dar-es-Salaam zimeharibu sana miundombinu ya barabara ikiwemo Jimbo la Ukonga, barabara nyingi zimekatika ikiwemo barabara ya Banana – Kitunda – Kivule – Msongola. Nini mpango wa Serikali wa kuzikarabati kwa dharura, hasa kipindi hiki ambacho wananchi wanapata taabu na barabara hizi?
Swali la pili. Barabara ya Mwembe Supu – Kwakupepeteka – Bangulo CCM mpaka Mwembe Kiboko kwenye Kata ya Pugu Station haijawahi kutengenezwa kwa kiwango chochote. Je, Naibu Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kwenda kuona barabara hii na kuweza kutoa kauli ya Serikali mbele ya wananchi wa Kata ya Pugu Station? (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Jerry Silaa kwamba, Mheshimiwa Mbunge amekuwa akilifuatilia sana hili suala, hasa la kupata fedha kwa ajili ya emergency kwenye barabara zake Jimboni kule.
Ninalitaarifu Bunge lako tukufu kwamba Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Angellah Kairuki amekuwa akifanya vikao mbalimbali na wenzetu wa TARURA na Wizara ya Fedha kuhakikisha TARURA inaongezewa bajeti ya kutoka bilioni 11 ya emergency mpaka bilioni 46, niwatoe mashaka vikao hivyo vinaenda vyema na Wizara ya Fedha imeahidi kutafuta fedha hizo kwa ajitihada za Mheshimiwa Angellah Kairuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, nipo tayari kuongozana na Mheshimiwa Jerry William Silaa kuelekea katika Jimbo lake la Ukonga na kuzikagua barabara zake. Ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaangalia ratiba hata weekend tutoke hapa tuelekee Jimbo la Ukonga tuweze kukagua barabara hizo na kuona ni kipi Serikali inaweza ikafanya. (Makofi)
Name
Josephine Johnson Genzabuke
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JERRY W. SILAA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Pugu - Majohe - Viwege njia nne na Kampala - Bwera - Rada hadi Chuo?
Supplementary Question 2
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Halmashauri ya Kasulu Vijijini ipo barabara ya kutoka Mgombe kwenda Kagerankanda, barabara hiyo hutumika kwa wakulima kupitisha mazao kupeleka majumbani kwao.
Je, ni lini Serikali itatoa pesa kwa TARURA ili barabara hiyo iweze kutengenezwa?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Genzabuke kuhusu hii barabara ya Mgombe iliyopo kule Kigoma:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari inafanya jitihada kubwa sana za kuhakikisha TARURA inakuwa na fedha ya kutosha ya kufanya matengenezo ya barabara mbalimbali hapa nchini. Tukirudi katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 TARURA ilikuwa ina bajeti isiyozidi bilioni 226, lakini kwa jitihada za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, TARURA imeongezewa fedha zaidi ya mara tatu na kwenda kuwa na bilioni mia saba na sabini na kitu. Hivyo nimtoe mashaka Mheshimiwa Genzabuke kwamba, TARURA itafikia barabara hizi na kuhakikisha zinatengenezwa kwa wakati kadri ya upatikanaji wa fedha.
Name
Dr. Christine Gabriel Ishengoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JERRY W. SILAA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Pugu - Majohe - Viwege njia nne na Kampala - Bwera - Rada hadi Chuo?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Barabara ya kuanzia pale SUA mpaka Mzinga Jeshini - Magadu, katika Manispaa ya Morogoro Mjini? Ahsante sana.
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaangalia katika bajeti hii iliyopitishwa na Bunge lako tukufu ya 2023/2024 kwa TARURA, kuona kama barabara ya SUA kwenda Mzinga imetengewa fedha. Kama haikutengewa fedha katika mwaka huu wa fedha basi tutaiangalia ni namna gani inaweza ikatengewa fedha katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved