Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Iddi Kassim Iddi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Msalala
Primary Question
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza:- Je, lini Sheria italetwa kupunguza michakato ya utangazaji wa Miradi ya TARURA na fedha kusimamiwa na Mameneja wa Wilaya?
Supplementary Question 1
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kutangaza ajira ambazo zinatoka TAMISEMI na hivyo kukadiria watumishi kupelekwa TARURA: Kwa nini sasa Serikali isiruhusu TARURA wenyewe waweze kuajiri wakandarasi au wahandisi?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Kwa kuwa, Jimbo la Msalala liko katika mazingira magumu sana kwenye maeneo hayo kwa maana ardhi yake ni mbuga: Sasa Serikali haioni haja ya kuongeza bajeti ili iendane na uhalisia wa maeneo hayo kwenye Jimbo la Msalala? Ahsante. (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Iddi Kassim, la kwanza hili la kwa nini TARURA wasipewe vibali vya kuajiri wenyewe, ni kwamba ajira katika utumishi wa umma hutolewa kulingana na ukomo wa bajeti ambayo imepitishwa na Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. TARURA wenyewe wanaomba vibali kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Utumishi na tutaendelea kutoa kipaumbele ajira za ma-engineer kwenye taasisi hii ya TARURA kadiri ya fedha ambavyo inapatikana na bajeti ya Serikali inaruhusu.
Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la mgawanyo wa fedha, hasa kule Msalala kwa sababu ya mazingira magumu, kwa sasa tayari kuna review inayofanyika chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Kairuki, kuangalia ni namna gani mgawanyo wa fedha unakwenda katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo kule Msalala. Naomba Mheshimiwa Mbunge awe na Subira na muda siyo mrefu timu hii itawasilisha taarifa yake mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na baada ya timu hiyo kuwasilisha taarifa hiyo, tutaangalia upya formula inayotumika kwa ajili ya kupeleka fedha maeneo mbalimbali nchini.
Name
Timotheo Paul Mnzava
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Primary Question
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza:- Je, lini Sheria italetwa kupunguza michakato ya utangazaji wa Miradi ya TARURA na fedha kusimamiwa na Mameneja wa Wilaya?
Supplementary Question 2
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa, kwenye nchi yetu majira yanatofautiana: Je, Serikali haioni umuhimu wa kuiruhusu na kuielekeza TARURA juu ya muda wa kutangaza na kutekeleza miradi kwa kuzingatia majira ya maeneo husika? (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, TARURA inatangaza kazi zake hizi kote nchini mara baada tu ya bajeti yao kuidhinishwa. Ni kama hivi sasa bajeti ya Shilingi bilioni 776 imeidhinishwa na Bunge lako Tukufu, hivyo katika mwaka mpya wa fedha unaoanza mwezi Julai mwaka huu 2023, ndipo kazi zote zitaanza kutangazwa.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved