Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Taska Restituta Mbogo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa meli tatu kwa ajili ya Ziwa Tanganyika kama ilivyoahidi?
Supplementary Question 1
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza. Kwanza tunaishukuru Serikali kwa kutenga fedha za ujenzi wa meli mbili kwenye Ziwa Tanganyika, lakini mwaka 2022 Serikali ilitenga fedha, na mwaka huu Serikali imetenga fedha, lakini majadiliano bado yanaendelea: Je, nini mkakati wa Serikali wa kuharakisha ujenzi wa meli hizi mbili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa wananchi wa Mikoa ya Katavi, Kigoma na Rukwa wanategemea meli za MV Liemba na MV Mwongozo: Je, lini Serikali itamaliza ukarabati wa meli hizi ili ziweze kufanya kazi kwenye Ziwa Tanganyika?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka tunavyoongea hivi tuko kwenye hatua za mwisho kabisa, na wakandarasi wa kuanza kujenga hizo meli kubwa mbili katika Ziwa Tanganyika walishapatikana. Kwa hiyo, wananchi wawe na imani, na ndiyo maana tunategemea kwamba tunaweza hata tukasaini kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha ili tuanze ujenzi wa hizo meli. Mkataba wa ujenzi, tunategemea watajenga kwa muda wa miaka miwili hizo meli mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili, tunatambua kwamba kwa sasa hakuna meli ambayo inafanya kazi katika Ziwa Tanganyika. MV Liemba tunavyoongea imeshapata mkandarasi na mkataba ni kwamba ukarabati huo utachukua miezi minane na meli hiyo itakuwa imerudishwa majini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Meli ya Mwongozo, meli hii ina historia yake. Kilichokuwa kimesimamisha hiyo meli isifanye kazi, siyo kwa sababu ya ubovu, ila Serikali ilitaka ijiridhishe kuhusu stability ya hiyo meli. Tunavyoongea, tayari Serikali ilishamu-engage Mhandisi Mshauri ambaye ni Chuo chetu cha DMI kufanya tathmini, na kama kuna marekebisho, yafanyike. Yakishafanyika, hiyo meli pia itarudi majini muda siyo mrefu. Kwa hiyo, tunategemea katika kipindi cha karibuni meli mbili; MV Liemba na MV Mwongozo zitarudi majini kuanza kufanya kazi katika Ziwa Tanganyika kwa muda wa karibuni sana ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved