Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza:- Je, kuna mkakati gani kuhakikisha uwepo wa walimu wa kutosha wa masomo ya hesabu na fizikia katika elimu msingi hadi kidato cha tano na sita?

Supplementary Question 1

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa bado kuna idadi kubwa sana ya Walimu wa Masomo ya Sayansi ambao bado hawajapata ajira na Serikali ilikuwa inaendelea kuajiri kidogo kidogo.

Je, ni upi mkakati wa Serikali sasa kuhakikisha kwamba angalau inaongeza wigo wa ajira angalau kuchukua Walimu wote walioko katika soko ambao kwa sasa wako tu hawana shughuli za kufanya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa suala zima la sayansi pia linaendana na uwepo maabara na wananchi nchi nzima maeneo yote wamejenga sana maboma mengi ya maabara, lakini kulikuwa na kasi ndogo ya ukamilishaji wa miradi hiyo ya Maabara. Je, Serikali ina mpango gani mahususi kuhakikisha kwamba ndani ya kipindi kifupi maboma yote yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi yanakamilika?

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Shangazi kwa niaba ya Mheshimiwa Kapinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hii idadi ya Walimu ambao bado hawajapata ajira hawa wa sayansi, nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita itaendelea kutoa kipaumbele katika kuziba mapengo na kuajiri Walimu wengi zaidi kwa sababu kama walivyoona, Wabunge wote ni mashahidi, Serikali hii imejenga miundombinu mingi sana kwenye suala zima la elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa Walimu 13,130 ni kwenye mwaka wa fedha huu ambao tunaumaliza, kwa maana ilikuwa 2022/2023 na vilevile Serikali imetenga bajeti kwa ajili ya 2023/2024 na pale ambapo fedha zitaruhusu, basi Serikali itaendelea kuajiri Walimu wengi zaidi na kuwapeleka katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la uwepo wa maabara. Ni kweli Serikali iliweka kipaumbele katika ujenzi wa maabara katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kupeleka shilingi milioni 30, 30 katika shule nyingi sana hapa nchini kwa ajili ya ujenzi wa maabara hizi. Baada ya ujenzi huu kukamilika sasa Serikali iko katika harakati za kutafuta fedha kwa ajili ya kupeleka vifaa vya maabara hizi. Mara baada ya vifaa hivyo kufika kwenye maabara hizi, vilevile tutaangalia tena namna gani ya kupata fedha kuendeleza ujenzi wa maabara zingine kote nchini.