Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Primary Question

MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaongeza madaktari na watumishi wa kada nyingine katika Kituo cha Afya Mrijo chenye Daktari na Nesi mmoja?

Supplementary Question 1

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza; Hospitali ya Wilaya ya Chemba tayari imefungwa mashine za x-ray na ultra-sound lakini hakuna mtaalam hata mmoja. Naomba kujua ni lini Serikali itapeleka wataalam hao ili mashine hizo zifanye kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Kituo hicho hicho cha Afya cha Mrijo kinahudumia Kata nne zikiwemo Kata za Wilaya ya Kiteto. Naomba kujua ni lini sasa watapeleka gari la wagonjwa ili liweze kuhudumia kituo hicho?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Lujio Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza hili la wataalam wa mionzi katika Hospitali ya Wilaya. Nimtoe mashaka Mheshimiwa Monni, Serikali inaendelea kutafuta wataalam hawa hata katika ajira ambazo zilikuwa zimetangazwa na Serikali katika upungufu ambao tulipata kwa kutokuwa na watu walioomba nafasi, ni nafasi kama hizi za wataalam wa mionzi, lakini Serikali itaendelea kuweka jitihada kubwa kwa ajili ya kuajiri wataalam hawa ili Hospitali ya Wilaya ya Chemba nayo iweze kupata watumishi watakaosaidia katika kutumia mashine hizi za x-ray na nyinginezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la Kituo cha Afya Kata ya Mrijo ambacho kinahudumia kata nne kama alivyosema Mheshimiwa Monni. Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika sekta hii ya afya vilevile na tayari fedha imeshatolewa kwa ajili ya ununuzi wa magari ya kubebea wagonjwa ambapo kila halmashauri hapa nchini ikiwepo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba itapata magari mawili kwa ajili ya kubebea wagonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haikuishia hapo, Mheshimiwa Rais bado aliona kuna umuhimu wa kupata magari kwa ajili ya supervision, kwa ajili ya watalaam wetu kutembelea zahanati zetu na vituo vya afya ambavyo vipo katika Halmashauri hizi, kwa hiyo pia halmashauri hizi zitapata angalau gari moja kwa ajili ya supervision.